WATENDAJI katika halmashauri ya wilaya ya Mbeya
wamekumbushwa kuwa ofisi zao ni kule miradi iliko na si katika majengo ya
halmashauri yao.
Mkuu wa wilaya hiyo Norman Sigalla ameyasema hayo wakati akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha kawaida cha
baraza la madiwani ambacho miongoni mwa ajenda zake ilikuwa kumchagua naibu
meya na kupitisha kamati mbalimbali.
“Haya majengo yapo kwaajili ya kuangalia ni wapi
miradi inatekelezwa.Msikae huku mpaka wakulima waunguze mazao yao kwa matumizi
mabaya ya mbolea.Nendeni huko mtoe mafunzo kwa vitendo wakulima wabadilike na
waanze kunufaika na mikakati ya matumizi ya pembejeo bora”.
Sigalla amesisitiza ushirikiano baina ya watendaji
na madiwani akisema chuki inapaswa kuwa
mwiko iwapo pande hizo zina nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa halmashauri
ya wilaya hiyo.
Amesisitiza watendaji kuzingatia maoni ya madiwani
badala ya kuyapuuza kwakuwa wapo kuwawakilisha wananchi wa kata wanazoziongoza na
miradi wanayoomba ndiyo inayohitajika kwa wananchi wao.
Hata hivyo alisema wapo baadhi ya madiwani walio na
tabia ya kusema ya kwao na si wananchi na kusema diwani mzuri ni ni
anayehakikisha mikutano inafanyika katika vijiji vyote vya kata yake kabla ya
kuleta hoja za wananchi wake kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Ameonya madiwani na wanasiasa kutohamasisha vitendo
vinavyozusha migogoro akisema Mbeya ni muhimu kuliko vyama vya siasa hivyo ni
vema wakajikita katika kuilinda amani ya wilaya yao badala ya kutekeleza
matakwa ya siasa zilizo na mwelekeo wa kuhatarisha amani.
Mkuu huyo wa wilaya hakusita kuonya kuwa kwa yeyote
atakayebainika kuhusika na uchochezi wa migogoro atakuwa wa kwanza kuchukuliwa
hatua za kisheria pasipo kuangalia ni diwani ama ana wadhifa upi katika chama
chake cha siasa.
Amesisitiza kutumia njia ya majadiliano zaidi pale inapobainika
kuna tofauti badala ya kuanzisha makundi ya malumbano yasiyo na sababu za
msingi.
No comments:
Post a Comment