Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, July 24, 2012

RC ASHUSHA RUNGU KWA MAFISADI CHUNYA


MKUU wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ametoa muda wa siku mbili kwa mkuu wa wilaya ya Chunya kutoa taarifa juu ya upotevu wa nyaraka zenye taarifa ya miradi ya kilimo zilizopotea.

Kwa mujibu wa Kandoro nyaraka hizo zinazoelezwa kupotea ni za miradi ya kilimo yenye thamani ya jumla ya shilingi 408,659,706.

Katika kikao maalumu cha baraza kilicholenga kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa fedha za serikali(CAG) mkuu wa mkoa amehoji ni kwa nini nyaraka hizo zipotee na hakuna hatua zilizochukuliwa.

Amesema upo uwezekano mkubwa wa kuwa fedha hizo hazikutumika ipasavyo na ndiyo maana zimefichwa ili ukweli usibainike.

“Kwa nini zipotee?Inaonekana kuna shughuli hazikufanyika lakioni fedha zilitumika.Nataka ndani ya wiki hii nipate maelezo juu ya upotevu huo na ilikuwaje.Mkuu wa wilaya hakikisha mpaka alhamisi ya wiki hii uwe umeniletea maelezo ofisini kwangu na hawa madiwani wapewe taarifa kamili” alisisitiza.

Amezidi kuitaja idara ya kilimo kuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wake kutokana na taarifa mbalimbali zinazobainisha kuwepo kwa kasoro.

Mkuu huyo wa mkoa amesema pia kuna miradi ya kilimo ya kiasi cha shilingi 496 milioni haijakamilika licha ya serikali kutoa fedha zote na kuhoji ni kwa nini lakini swali hilo halikupata majibu kutokana na afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya hiyo kutohudhuria kikao hicho.

Aliendelea kusema kuwa pia ipo miradi yenye thamani ya shilingi milioni 73 haijakamilika na kuhoji kuna nini katika idara ya kilimo mpaka kuwe na uozo wa namna hiyo.

Aliwataka madiwani kutokubali kuburuzwa na wakuu wa idara na kukubali kupitisha taarifa za miradi kwenye vikao vyao pasipo kujiridhisha iwapo zinaendana na uhalisia wa miradi husika.

Kandoro pia amezishushia rungu idara za Maji, na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF)akisema pia zinatuhumiwa kwa kuwa na uozo wa matumizi mabovu ya fedha kama ilivyo kwenye kilimo na kuhitaji maelezo ya kina ni kwa nini.

Amesema katika idara ya maji kuna kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 4.6  zimetumika pasipo maelezo ya matumizi yake huku pia kiasi cha zaidi ya milioni tano zikionekana kuwa malipo ya kughushi.

Kwa upande wa TASAF amesema kuna kiasi cha zaidi ya shilingi 5020,000 zimetumika kununua mafuta lakini hakuna nyaraka zinazoelekea mafuta yalinunuliwaje na kutumika vipi.

No comments:

Post a Comment