Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, March 29, 2016

Biashara ya Vileo na hatari ya ngono kwa mabinti Mbeya.

Na Joachim Nyambo.

BIASHARA ya vileo inazidi kushamiri siku hadi siku mkoani Mbeya kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini.Kushamiri kwa biashara hii kunakoendana na kupanuka kwake kunasababisha wafanyabiashara kubuni mbinu mpya kila kukicha.Lengo la ubunifu huu ni kuvutia wateja.

Mkoani hapa mji ulio na bishara kubwa ya vileo ni jiji la Mbeya.Maeneo kama ya Mwanjelwa,Kabwe,Soweto,Ilomba na Sae yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu yanaonekana kuwa na baa nyingi ikilinganishwa na maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.

Ingawa mkoa wa Mbeya unanafasi kubwa ya kuongoza kwa kuwa na makanisa mengi nchini,uwingi wa nyumba hizo za ibada bado haujafikiaa maeneo yanayouza vilevi.Yawezekana unapovuka kanisa moja kabla ya kulikuta jingine utakutana na baa,au Grocery zaidi ya tano mpaka sita.

Uwepo wa maeneo mengi ya kuuza mvinyo unatokana na jiji hili kuwaa moja ya maeneo nchini yenye kupata wageni wengi achilia mbali kipato kizuri cha wakazi wake.Wapo wageni ambao huingia jijini hapa kutoka mikoa mbalimbali nchini kila siku.Wapo pia wageni ambao huingia wakitokea nchi mbalimbali za jirani zikiwemo Zambia,Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Wengi wa wageni hawa ni wafanyabiashara ambao ama huingiza bidhaa kutoka makwao au kuja kuchukua zile zinazozalishwa mkoani hapa yakiwemo mazao ya chakula na biashara.Mazao hayo ni pamoja na Ndizi,Mahindi,Kokoa,Mpunga na Kahawa.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanabainisha kuwa Uwepo wa maeneo mengi ya starehe ni dalili za kukua kwa uchumi wa eneo husika.Hivyo kwa Mbeya kushamiri kwa biashara ya vilevi pia ni kiashiria cha kuwepo kwa uchumi imara na wenye kukua kila kunapokucha.

Lakini biashara ni matangazo!Hapo ndipo wamiliki wa baa,grosery na maeneo mengine ya starehe jijini hapa wamekuwa wakukuna vichwa kila mmoja akitafuta ubunifu utakaowezesha wateja wengi kukimbilia kwake.

Kuweka wahudumu wengi na walio warembo ni moja kati ya ubunifu ulioibuka katika siku za hivi karibuni jijini hapa.Wafanyabiashara za mvinyo wanasema njiaa hii inarahisisha zaidi kuwapata wateja kwakuwa hushawishika na uwepo wa warembo.

“Usione watu wanajaa namna hii ukajiuliza maswali mengi.Ni kweli wengine wanaweza kusema umetumia kizizi na wengine wakasema umeboresha mazingira yako vizuri.Lakini ukweli ni kwamba siku mabinti hawa wakipungua na mauzo yanapungua pia” alisema mmoja wa wafanyabiashara ya mvinyo katika maeneo ya Mwanjelwa aliyeomba kutotaja jina lake wala jila la eneo lake la biashara.

Mmiliki mwingine alisema kutokana na ushindani uliopo wanalazimika kuwafuata mabinti mbali kwakuwa wanaotoka jirani ni wasumbufu ahasa wanapopewa majukumu na mabosi wao.Hivyo inawalazima ama kutuma gari au nauli ili kuwafuata wahudumu.Hasara hutokea pale wanapofika na kulizoea jiji kwani huanza kurubuniwa na wenyeji na kuhamia sehemu nyingine.

Uchunguzi umebaini kuwa kivutio cha wahudumu hawa kwa wateja sit u kuwahudumia vinywaji.Ipo biashara ya ngono pia inayoendelea baina ya pande hizi mbili.Hiki ndicho hasa huwavuta wateja wengi kwenye baa hizi zilizo na warembo wengi.

Unyonge utokanao na kutofahamu haki zao kisheria unatajwa kuwa chanzo cha wahudumu hawa wa kike katika baa nyingi mkoani hapa kugeuzwa watumwa wa biashara ya Ngono.

Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Community Media Organization(Tacomo),linasema limefanya uchunguzi na kubaini hali mbaya kwa wahudumu wa kike katika biashara ya ngono.

Mkurugenzi wa Tacomo, Gordon Kalulunga, anasema kumekuwepo na tatizo kubwa la wasichana wanaofanya kazi kwenye baa kukatiliwa kingono huku msingi mkubwa wa ukatili huo ukijengwa na waajiri wao.Hali hiyo imezidi kuwa mbaya na hatari kwa wafanyakazi hao lakini wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa kwa hofu ya kufukuzwa kazi na usalama wa maisha yao.

"Waajiri wakiwemo wamiliki wa baa na mameneja wamekuwa wakiwalazimisha wahudumu kufanya nao ngono kabla ya kuwapa ajira hizo.Lakini hata mara baada ya kuwaajiri huwalazimisha kufanya ngono na wateja wa baa hizo kwa makubaliano ya wateja hao kulipia kati ya shilingi elfu tano hadi elfu kumi kwa siku fedha iliyopewa jina maarufu la malipo ya kaunta.Malipo haya hayamhusishi binti anayekwenda kutumikishwa katika ngono bali itategemeana huruma ya mtu aliyekwenda naye akiamua kumlipa sawa na asipotaka pia haya” alisema Kalulunga.

“Kibaya zaidi ni kwamba tumebaini uwepo wa biashara ya binadamu ambapo kuna wahudumu wamekuwa mawakala wa kuwanunua wenzao mikoani kwa kuwalaghai kuwa waje Mbeya kufanya kazi za Hoteli na kulipwa fedha nyingi, ahadi ambayo haitimii kwani wakifika hapa wanaishia kutumikishwa kingono kwenye baa wanazoajiriwa" aliongeza Kalulunga.

Mkurugenzi huyo aliitaja mikoa ambayo wasichana wengi wanatolewa huko na kuletwa bmkoani Mbeya kutumikishwa kingono kuwa ni pamoja Singida, Iringa, Njombe na Ruvuma.

“Mkoa wa Singida unaongoza katika jambo hili.Tulichobaini ni kuwa wengi wanadanganywa kwa kuahidiwa mambo makubwa wakiwa makwao.Ndiyo sababu utakutana na mabinti wadogo wanaotoka kwenye mkoa huo wakifanya kazi za uhudumu katika baa za hapa mjini.Wapo pia wanaokuwa wametoroka mashuleni na kuja hapa”

“Ukweli wanapofika hawakutani nay ale walioahidiwa wakiwa nyumbani.Hujikuta wametumbukia kwenye hatari ya ulevi na ukahaba kwa kulazimishwa na waajiri wao”

“Wanajikuta kuhiari utumwa wa kuuzwa kwakuwa wanapofika hupewa chumba kimoja kwaajili ya kulala na kuhifadhi vitu vyao kama nguo.Haijalishi wako wengi kiasi gani.Wengine hupewa godoro na kitanda kimoja ili walale hapo.Wao huviita vyumba hivi Gheto.Siku pekee ambayo binti anaona analala vizuri ni pale anapobebwa na mwanaume kwenda kufanya naye ngono.Kwakuwa watalala wawili tofauti na Gheto anajiona mwenye bahati.Huenda pia akala chakula kizuri zaidi ya wanachokula wenzie Gheto” anasema Kalulunga.

Mkurugenzi huyo anasema ili kukabiliana na hali hiyo,Tacomo wameandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa wahudumu kwa kushirikiana na wadau wengine watakaoona kuna umuhimu wa jambo hili kufanyika, ili kuweza kutoa elimu kwanza ya kujitambua wahudumu hao ili kuwaondolea woga wa kutoa taarifa.

Aliwaomba wadau mbalimbali kuona umuhimu wa kushiriki katika mpango huo huku akivitaja vyombo vya habari kuwa mhimili muhimu utakaowezesha kuikomboa jamii ya wahudumu wa baa.

Kadhalika aliwataka wahudumu wa kike kwenye baa mkoani hapa,kujitokeza kwenye vyombo vya habari na sheria, kutoa malalamiko ya ukatili wa kijinsia hasa rushwa za ngono wanazofanyiwa.

Uchunguzi pia uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini uwepo wa uwezekano mkubwa wa wahudumu hawa kuambukizwa maaradhi kwa njia ya ngono.Wateja wengi huwanunuliwa pombe wahudumu wanaolenga kuondoka nao siku husika.Mara nyingi wawili wote hulewa na wanapofikia uamuzi wa kwenda kufanya ngono uhakika wa ngono salama unakuwa mdogo.

“Kama tunajikuta tumebeba mimba kutokana na wanaume hao hao tunaolewa nao iweje kwa magonjwa.Ni kweli upo uwezekano mkubwa wa kupata pia maambukizi kwakuwa wakati mwingine tunakosa namna ya kujitetea hasa pale mwanaume anapokuwa amekulipia kaunta na umekunywa bia zake” alisema mhudumu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jasmini japo alisema hilo ni jinalake la mjini tu.

“Inafikia wakati Yule anayepata wanaume wengi anaonekana mwenye bahati zaidi ya ninyi wengine.Atakula vizuri,atavaa vizuri,atasuka vizuri na atapendeza zaidi hata tunapokuwa tumeingia kazini.Anakuwa amejitengenezea mtaji mzuri wa kupata mwanaume mwingine aliye na fedha nyingi.Hivyo unapoanza shughuli hii kwa kumpata mwanaume mwenye nazo unakuwa umejipatia mtaji mzuri sana.”alisema dada huyo.

Histori pia inaonesha kuwa mabinti wengi huanza kutumia vilevi wanapowasili jijini hapa na kuanza kazi ya uhudumu.Wakiwa kwao hawatumii na hata ukiwauliza wanakwambia hawakuwahi kutumia kilevi chochote tangu kuzaliwa kwao.

Hatua hii inazua hofu ya kusafirishwa kwa magonjwa ya zinaa kutoka jijini hapa na kuyapeleka katika jamii wanazotoka mara wanapokwenda kwenye mapumziko.Wazazi wengi wa mabinti hawa sambamba na jamii zinazowazunguka wanaamini kuwa ni wafanyakazi katika mahoteli makubwa.Hii ni kwakuwa wengi wa wazazi hawa hawajafika jijini hapa kuona nini watoto wao wanafanya.

Uchunguzi unaonesha waahudumu hawa kulipwa mishahara midogo kutokana na uwingi wao.Anaebaki kutegemea mshahara ni wazi atabakia kuishi maisha magumu na kuwa ombaomba kwa wenzie.Wapo pia wahudumu ambao huwaomba mameneja kuwaruhusu wafanye kazi pasipo kuwalipa.Malipo yao hujilipa wenyewe kutokana na ubunifu wao.Mara nyingi hawa ni wakongwe kwenye biashara hii na wanaona kulipwa ujira kunasababisha waajiri kuwabana.

Halii hii ni changamoto kwa jamii,sit u wanakotoka mabinti hawa.Bali pia maeneo wanayofanyia shughuli zao.Ni wakati kwa mamlaka husika pia kulivalia njuga suala hili na kulitafutia ufumbuzi ili kuokoa kizazi hiki na kijacho.Nasema nihatari kwakuwa biashara hii inaendelea kukua kila siku.

Thursday, March 24, 2016

MWANAKIJIJI AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA

Mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Isandula kata ya Kilimampimbi wilayani Mbozi mkoani Songwe ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiofamika.

Diwani wa kata ya Kilimampimbi Henry Mwilenga akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu amemtaja marehemu kuwa ni Luka Kabuka anayekadirwa kuwa na umri wa kati ya miaka 70-80 mkazi wa Isandula wilayani humo

 Mwilenga amesema tukio hilo limetokea march 21 saa mbili usiku mwaka huu ambapo marehemu alikuwa akitokea matembezini na kabla hajafika nyumbani kwake mita sabini alivamiwa na watu wasiofahamika na kufanyiwa unyama huo.

Amesema tukio hilo limegunduliwa na mtoto wa marehemu ambaye naye siku ya tukio alichelewa kufika nyumbani na wakati anafika karibu na eneo la tukio ndipo aligunduwa kuwa aliyeuawa ni baba yake na ndipo akapiga mayowe na kuomba msaada.

Mwilenga amesema baada ya tukio hilo kutokea waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya wilaya ya mbozi kwaajili ya uchunguzi na kusadikiwa kuwa marehemu alinyofolewa baadhi ya viungo na wakuruhusiwa kwa ajili ya mazishi.

Katika hatua nyigine diwani huyo amesema marehemu ameuauwa kinyama kwani alipoingalia maiti ilikutwa na majereha makubwa matano usoni hali inayoashiria kuwa alipigwa na vitu vyenye ncha kali.

Aidha amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwagundua watu waliohusika na unyama huo kwani tukio hilo ni la pili kutokea katika kata hiyo ndani ya miaka miwili. 

Tuesday, March 22, 2016

ZOLA D APONDA WATUNISHA MISULI WENZAKE



Image result for Zola  DMSANII wa Muziki wa hip hop laini nchini David Michael Mlope maarufu kama Zola D ameibuka na kuwaponda vijana wanaofanya mazoezi ya kutunisha misuli akisema wanahatarisha afya zao kutokana na dawa wanazotumia.

Zola D ambaye pia ni mmoja wa mabondia nchini alibainisha hayo alipozungumkza na waandishi wa habari alipokuwa mkoani Mbeya ambapo alisema tabia ya Mapenzi ya jinsia moja ni miongoni mwa matokeo ya Dawa wanazotumia watunisha misuli ili kutanua misuli yao kwa haraka.


“Vijana wengi hivi sasa  wanatumia kwa wingi dawa za kutunisha misuli maarufu kama ‘doping’ ili waweze kutanua misuli yao kwa haraka pale wanapohitaji.Kwa sababu zinazotajwa kuwa ni kutafuta ajira kama vile ulinzi kwenye kumbi za starehe, ulinzi wa watu maarufu(bodyguard) na wengine mashindano ya kunyanyua vitu vizito au wakiutafuta utanashati wanatumia dawa hizi bila kujua madhara yake baadaye” alifafanua Zola D.


Alisema dawa hizo maarufu kwa jina la Anabolic Steroids husaidia kutunisha misuli ndani ya muda mfupi lakini madhara yake ni makubwa ambapo mtumiaji huweza kupata magonjwa ya kansa, kupanuka kwa moyo na kupasua mishipa ya damu inayopelekea kupoteza maisha.

Alisema mbali na madhara hayo pia vijana wengi hupoteza uwezo wa kufanya mapenzi jambo linalowapelekea kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutokana na kupoteza nguvu za viungo vya uzazi inayosababishwa na matumizi ya madawa hayo.

Alibainisha kuwa kutokana na madhara hayo kwa vijana kupitia kampuni ya Tanzania Streetsworkout ameanzisha aina ya mazoezi ambayo hayahusiani na kwenda gymu wala kunyenyua vitu vizito mazoezi ambayo yanamlenga kila mtu bila kujali umri wala jinsia


Alisema mazoezi ni tiba ya magonjwa mengi hivyo ni muhimu kila mtu akaona umuhimu wa kufanya mazoezi ambayo sio lazima kunyenyua vitu vizito ilikuwa na misuli mikubwa bali ni kujenga utimamu wa mwili ili kujiepusha na magonjwa.
Image result for Zola  D
Aliongeza kuwa aina hiyo ya mazoezi wanayofundisha wao ni yale ambayo hufanywa nyumbani, chumbani, ofisini na hata barabarani ambapo kila mtu anaweza kufanya mazoezi kwa dakika tatu na kuendelea kadri atakavyojipangia lakini matokeo yake ni makubwa kutokana na mabadiliko anayoyapata.

Alisema kwa sasa kupitia kampuni hiyo,wanazunguka nchi nzima lengo likiwa ni kuhamasisha vijana,wazee na watoto kuacha kutumia dawa za kutunisha misuli na badala yake wajikite kwenye mazoezi ya kawaida ili kujenga afya zao na hatimaye kujikita katika uzalishaji mali.Image result for Zola  D

Monday, March 21, 2016

WATATU WAUAWA KWA KUNYONGWA NA KUCHOMWA MOTO WAKIWA GUEST

WATU watatu wameuawa kwa kunyongwa na kisha miili yao kuchomwa moto katika Nyumba ya kulala wageni iitwayo Mexico Guest House iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya walikokuwa wamepanga vyumba vitatu tofauti.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Mbeya Ahmed Msangi waliouawa wametambuliwa kwa majina waliyoandika katika kitabu cha Mapokezi aliowataja kuwa ni wafanyabiashara Mariam Hassan aliyepanga chumba namba 15 na Abbas Yasini aliyepanga chumba namba 14 na mkulima Tatizo Adam aliyepanga chumba namba 103.

Kamanda Msangi amesema mnamo Machi 19 saa 10 jioni walifika wageni wane katika Guest hiyo kati yao watatu wakiwa wanaume na mwanamke mmoja ambapo walikodi vyumba vitatu na Marium aliingia katika chumba namba 15 akiwa na mwanaume mmoja ambaye hakuandika taarifa zake kwenye kitabu cha orodha ya wageni.

Amesema majira ya saa moja jioni watu hao ambao wote walisema wanatokea Songea mkoani Ruvuma walionekana wakitoka na baadaye waliporejea wakaingia na kukaa chumbani kwa Marium na kufanya maongezi huku wakinywa vinywaji.

Mnamo Machi 20 saa 1:30 asubuhi mtu mmoja aishiye jirani na nyumba hiyo aliona moshi ukitokea kwenye chumba namba 15 alichopanga Mariam na ndipo akawajulisha wahudumu wa gesti hiyo ambao baada ya kwenda kukagua walikuta miili ya watu watatu ikiwa imenyongwa na kasha kuchomwa moto.

Amesema hata hivyo inadaiwa kuwa mapema siku hiyo mwanaume aliyelala chumba namba 15 pamoja na marehemu Mariam ambaye hakuandika taarifa zake kwenye kitabu aliondoka gesti hapo akiwa amebeba ndoo ndogo na begi dogo ambapo aliaga kuwa yeye anasafiri lakini wenzake amewaacha wanaendelea kupumzika.

Kamanda Msangi alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi huku mmiliki wa gesti hiyo Sprian Mtengela anashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano huku akisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Kyela kwaajili ya utambuzi.


Friday, March 18, 2016

Sasyaka sekondari mkombozi anayechelewa kutua Mbeya vijijini

Na Joachim Nyambo.

NI miaka mitatu sasa imepita tangu wakazi wa kata ya Masoko wilayani Mbeya walipochukua uamuzi wa kujenga shule ya sekondari.Lengo la wakazi hawa ilikuwa kutekeleza adhma ya serikali ya kila kata kuwa walau na shule moja ya sekondari.

Sekondari ya kata ya Masoko ijulikanayo kama Shule ya sekondari ya Sasyaka ilianza kujengwa mwaka 2013 lakini mpaka leo haijaanza kutumika.Kutoanza kufanya kazi kwa shule hii kunasababisha wanafunzi wanaofaulu katika shule za msingi zilizopo kwenye kata ya Masoko kwenda kuanza masomo ya sekondari kwenye shule za sekondari za kata za Shisyete na Ilembo.

Hii huwalazimu wanafunzi hao kwenda kuishi mbali na wazazi wao katika vyumba vya kupanga au kulazimika kutembea umbari mrefu wa zaidi ya kilometa 20 kwa siku kwenda na kurudi shuleni.

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Oran Njeza anasema kilio kikubwa cha wakazi wa kata ya Masoko ni kukosekana kwa shule ya sekondari.

Anasema kutokana na kukosekana kwa sekondari,wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wamekuwa wakilazimika kupangiwa shule zilizopo kwenye kata nyingine ikiwemo Ilembo hatua ambayo huwalazimu kutembeza zaidi ya kilometa 10 kuzifikia shule hiyo hivyo kwa siku wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 20 kwaajili ya kwenda na kurudi.

“Watoto wanawakati mgumu sana katika kata hii.Wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 20 kwa siku.Hii inawalazimu kutumia muda mwingi kutembea na muda mchache mno darasanai.” Anasema Njeza.

Anasema hali ni mbaya zaidi katika kipindi cha mvua nyingi kwakuwa wanafunzi hufika shuleni wakiwa wamenyeshewa na mvua na na vivyo hivyo wakati wa kurudi makwao na hivyo kushindwa kushiriki vipindi darasani ipasavyo.

Wakazi wa kata hii wanasema wamechoshwa na watotoa wao kwenda kusoma mbali na kata yao.Wamechoshwa na athari ambazo zimekuwa zikiwakumba watoto hao na familia zao kwa ujumla.Familia zilizo na watoto wa kike ndizo huathiriwa zaidi.

Fidelia Mwasenga ni mmoja wa wakazi wa kijiji cha Masoko kilichopo kwenye kata hiyo,Anasema Kukosekana kwa sekondari kwenye kata yao kunasababisha uduni wa elimu.Ndoto zao ilikuwa kuanza kunufaika mapema na sekondari wanayoijenga.Sasa siku zinazidi kupita pasipo matunda tarajiwa kuonekana.

“Sasa shule hii mimi inanikera kwakuwa najiuliza ni kwa nini inachelewa kufunguliwa?Na hii tunaumia kutokana na Mazingira ambayo watoto wanasoma.Ni mabaya sana,watoto wanapata mimba humo njiani,Wengine hawaendi shule inavyostahili kwakuwa wanarubuniwa njiani.”

“Tumelia kwa muda mrefu.Imefikia wakati mpaka wazazi wanakata tama ya kupeleka watoto wao shule kwakuwa kila wanapojaribu kuwapeleka hawafikii malengo ya familia kwakuwa wanaishia njiani.Tunaomba serikali itusikilize ifungue shule yetu” anaomba Fidelia.

Mkazi mwingine Donati Mwalinda anasema walioathirika si watoto peke yao,wazazi pia wameathirika sana kwakuwa hawaoni matunda ya michango wanayochangia katika elimu.

“Kwa mfano kipindi hiki cha mvua,mtoto analowa njia nzima mpaka anafika shuleni.Akifika darasani amelowa hata mahesabu hawezi kufanya kwakuwa akili haifanyi kazi.Atalazimika kulowa tena wakati wa kurudi nyumbani mpaka anafika.Taayari kwa familia ni tatizo kwani kwa kunyeshewa na mvua tayari anaweza kupata magonjwa na kuilazimu familia kugharamia matibabu.”

“Tulijenga madarasa manne kwa wakati mmoja mwaka huo huo 2013.Kazi nyingi tumefanya mapaka majengo ya shule hii kufikia hapa unapoyaona.Kusomba tofali,kuchimba na kusomba mchanga kwa kichwa kutoka mtoni zote tumefanya.Tukaambiwa tujenge kwanza jengo la utawala.Lakini matokeo yake tumejenga mpaka jengo la utawala hawataki kufungua shule yetu” anasema mkazi mwingine Obeid Mwashibanda.


Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wialayani hapa Abihudi Fungamtama,anasema kilichocheleweshwa kufunguliwa kwa shule hiyo ni kutokamilika kwa vigezo vinavyotakiwa.

“Mwenye mamlaka ya kusajiri shule ni Kamishna wa Elimu na Upo waraka maalumu uliotolewa unaoeleza kuwa ili shule ifunguliwe lazima ikidhi vigezo ambavyo tumekuwa tukiwaelekeza wakazi wa kata hii kuvitimiza”anasema Fungamtama.

“Moja unatakiwa kuwa na vyumba vya madarasa angalau vya kutosha wanafunzi wa miaka miwili kwa maana ya kidato cha kwanza na cha pili kwa mikondo miwilimiwili hivyo kunatakiwa kuwepo na madarasa angalau manne.Lakini pia Miundombinu kwa maana ya Nyumba za walimu,maji na eneo ambalo kwa kijijini ni hekta tatu.”

“Kwa shule hii kwa upande wa eneo inalo la kutosha.Tatizo kubwa ni kwamba hakuna nyumba za walimu na pia maji hayaklo jirani na shule.Pia hakuna samani kwa maana ya meza na viti.Jengo la utawala halijakamilika na pia hakuna vyoo”

Afisa huyu anasema kutokamilika kwa vigezo hivyo kwa kipindi cha nyuma kulitokana na kutojitoa kwa wananchi katika michango  mbalimbali ya ujenzi kama ilivyohitajika.Uongozi wa kata hiyo ulihamasisha wananchi kutochangia ujenzi huo ukisema serikali ina jukumu la kutekeleza jambo hilo tofauti na uongozi uliopo hivi sasa ambao umeonesha nia ya kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye mikakati ya kujiletea maendeleo.

“Kwa kasi ninayoiona hivi sasa nina amini mwakani shule hii inaweza ikafunguliwa.Na sisi kama halmashauri kama ilivyokuwa huko nyuma tutaendelea kushiriki kwa karibu kushauri ili ikamilike kwa wakati ili angalau mwaka kesho shule iweze kupata usajiri” anasema afisa huyo.

Lakini tama ya mbunge wa jimbo hili ni kuona shule hii inafunguliwa haraka na watoto kuanza masomo shuleni hapo.Nia ni kuwaondolea adha wanafunzi huku pia akisema atahakikisha ujenzi wa Hosteli shuleni hapo unafanyika kwa haraka ili wanafunzi wa kike waishi jirani na shule yao kuepuka vishawishi vya wanaume wa mitaani.

“Nilianza kuja shuleni hapa hata kabla sijawa mbunge.Nikiwa Kamanda wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) nilifika mara kadhaa hapa hivyo natambua haja ya wakazi wa kata hii juu ya sekondari.Nitahakikisha ninafanya kila linalowezekana kukamilisha jambo hili kwa wakati”anasisitiza Njeza.

Nia ya mbunge huyu imejidhihirisha hivi karibuni pale alipoandaa harambee ya kuchangia sekondari hii ya Masoko ili kukamilisha ujenzi wake.Katika harambe hiyo iliyofanyika kwenye eneo la shule husika Njeza alifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 30.

Miongoni mwa fedha zilizokusanywa katikaa harambee hiyo ni pamoja na shilingi milioni 16 zilizotolewa na mbunge Njeza huku halmashauri ya wilaya ikiahidi kuchangia shilingi milioni 6.2.

Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Masoko Tumaini Mzumbwe kiasi cha shilingi milioni 71 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa sekondari hiyo.

Akizungumzia harambee hiyo,mbunge Njeza aliyeambatana na wafanyabiashara rafiki zake kutoka mji mdogo wa Mbalizi wilayani hapa ambao pia kila mmoja wao alichangia kwa kadiri alivyoweza,alisema huo ni mwanzo na iwapo kuna jambo lolote atahitajika kuchangia hatosita.

“Lakini haya yote yatawezekana iwapo tutashirikiana kila mmoja kwa namna anavyoweza.Tumekwishawambia wananchi kuwa tusitarajie maendeleo kwa kutegemea nguvu ya jirani.Ni lazima tushiriki kujiletea maendeleo na ndiyo sababu hata bajeti ijato ya serikali kuu inalenga kujitegemea zaidi badala ya kubaki ombaomba”anasema Njeza.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbeya Mwalingo Kisemba anasema ni kata mbili pekee zimebakia kwenye halmashauri yake hazika shule za sekondari.Ipo kata ya Masoko ambayo ujenzi wa sekondari ya Sasyaka unaendelea na kata ya Inyala ambako ujenzi wa sekondari ya Iyelanyala unaendelea pia.

“Kwa kutimiza ujenzi wa sekondari katika kata nyingine zote tunaamini tumepunguza deni kwa kiasi kikubwa hivyo kutokana na ushiriki wa wananchi kwa sasa tutakamilisha na hizi mbili kwa kipindi kifupi kijacho.Uwepo wetu tu hapa leo unaonesha nia yetu katika kutekeleza jambo hili mapema” alisema Kisemba aliyehudhuria pia harambee hiyo.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa namba 0756 40 95 97 Email nyambojoachim@gmail.com