Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, March 3, 2016

MUST NA MATARAJIO MAKUBWA YA MAFANIKIO


Na Joachim Nyambo.

AMA kweli safari ni hatua!Ndiyo maneno yanayoweza kutumiwa na wadau wa elimu ndani na nje ya nchi wanapokizungumzia Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya(MUST).Chuo hiki kilianzishwa rasmi 2012 baada ya mabadiliko ya iliyokuwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya(MIST).Kilikabidhiwa Idhini ya chuo kikuu mwaka 2013.

Tangu kupewa idhini hiyo tayari Chuo tayari chuo hiki kimeendesha mahafali tatu zenye kudhihirisha jitihada zake katika kuendeleza na kutoa fursa za kitaaluma kwa maendeleo ya jamii mbalimbali nchini.Hadi mwishoni mwa mwaka jana tayari wahitimu 2,297 wametunukiwa stashahada na shahada mbalimbali chuoni hapa tangu kipandishwe hadi na kuwa chuo kikuu.

Katika mahafali ya tatu ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana,makamu mkuu wa chuo,Prof Joseph Msambichaka alisema mafanikio yaliyopo na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya uongozi wa Must na serikali katika ngazi mbalimbali.

“Mafanikio yoyote ya kitaasisi huja kutokana na ushirikiano mzuri unaokuwepo baina ya wadau mbalimbali.Hata mafanikio haya tunayoyazungumzia ya kutunuku shahada kwa idadi hii kubwa ya wanafunzi ni matokeo ya ushirikiano mzuri.Na huu ni mhimili muhimu utakaozidi kukipa mafanikio makubwa na mazuri chuo chetu siku za usoni”

Prof Msambichaka anasema kwa kuzingatia mahitaji ya uboreshaji wa elimu ya sekondari nchini kupitia mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari(MMES) ambao umesaidia sana kuongeza idadi ya shule za sekondari nchini na pia mkakati wa kujenga maabara za sayansi katika kila sekondari,chuo hicho kinaandaa mitaala ya kufundishia shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi ili kulisaidia taifa kupata walimu wa kutosha katika masomo hayo

Anasema chuo pia kinaendelea na mipango ya kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya Ualimu na Sayansi(College of Science and Education) kitakachokuwa mahususi kwaajili ya kutoa mafunzo ya ualimu katika masomo ya Sayansi ambapo mafunzo hayo yataanza kutolewa katika mwaka wa masomo 2016/2017.

“Must pia imeandaa mitaala mipya kwaajili ya kutolea mafunzo uhandisi katika ngazi za Stashahada ya juu ya mafuta na gesi na uhandisi Ujenzi,Shahada ya uzamili ya uhandisi nishati mbadala na uhandisi maji na ujenzi na Shahada ya uzamivu ya uhandisi maji na ya uhandisi Ujenzi.Mafunzo haya pia yataanza mwaka wa masomo ujao” alisema Prof Msambichaka.


Anasema udahili wa wanafunzi kwa mwaka 2014/2015 ulikuwa na wanafunzi 3,342.Jitihada za kuanzishwa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu na Sayansi,kuanzishwa Kampasi mpya mkoani Rukwa na kuendelea kuanzisha kozi mpya katika chuo cha teknolojia na uhandisi kunategemewa kuongeza udahili wa wanafunzi mpaka kufikia wastani wa wanafunzi 4,000 katika mwaka wa masomo 2016/2017.

“Chuo kimeendelea kutoa mafunzo ya awali yaani Pre entry course ili kuwawezesha wanafunzi wa kike wasiokuwa na ufaulu wa kutosha kujiunga na mafunzo ya stashahada za uhandisi na teknolojia katika fani mbalimbli.”

“Katika mwaka wa masomo 2015/2016 wanafunzi wa kike 42 waliweza kufaulu na hivyo kuwa na sifa za kujiunga na mafunzo ya stashshada katika fani za uhandisi na teknoloji”

Kuanzishwa kwa mafunzo ya Lugha ya kichina ni mafanikio mengine ya chuo hiki kinachozidi kupaa kimaendeleo.Hii ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano baina ya chuo hicho na vyuo vingine duniani.

Kwa mujibu wa Prof Msambichaka mafunzo ya lugha ya Kichina yalianza kutolewa Novemba mwaka huu na yanafanyika kwa ushirikiano baina ya Must,Chuo kikuu cha Dar es salaam na Taasisi ya Confucius ya nchini China.Kuanza kutolewa kwa mafunzo ya lugha ya kichina ni fursa kwa wafanyabiashara na wanafunzi kujifunza lugha hiyo ili kupanua wigo wa mawasiliano na biashara kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa China inaendelea kwa kasi kubwa sana kiuchumi.

Akizungumzia uboreshaji wa utoaji taaluma chuoni hapo,Makamu mkuu huyo wa chuo anasema uendelezaji wa kitaaluma kwa watumishi unaendelea kufanyika lengo likiwa ni kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa rasiliamli watu.

Chuo kimeendelea kusomesha watumishi katika ngazi mbalimbali ambapo kwa sasa kina jumla ya watumishi 68 walioko masomoni ambao kati yao 43 ni walimu na miongoni mwa walimu hao 15 ni wa shahada ya uzamivu na 28 shahada ya Uzamili.Waendeshaji mitambo ni 25 ambao shahada ya uzamili wapo sita,Shahada ya kwanza 13 na stashahada wapo sita.

“Chuo pia kwa kushirikiana na kampuni ya RAINAT Technical Solution imeweza kuanzisha maktaba ya mtandaoni kwaajili ya kuwawezesha wanafunzi wa ngazi mbalimbali nchini kuweza kusoma vitabu mtandaoni”

“Tovuti ya maktaba hiyo ya www.tovl.ac.tz ambayo kwa sasa iko katika majaribio itazinduliwa mapema wakati wowote” anabainisha Prof Msambichaka.

Pamoja na mafanikio ambayo chuo kimepata katika kipindi cha mwaka 2014/2015,chuo kina mipango mbalimbali ili kukabili changamoto zilizopo na zitakazojitokeza baadae.Kuongeza udahili wa wanafunzi hususani kwa wanafunzi wa kike ni miongoni mwa mipango husika.

Chuo kina mpango wa kusomesha watumishi wengi zaidi hasa katika ngazi ya shahada ya uzamivu.Kuwezesha ufanyikaji wa tafiti zenye kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii,Kuongeza vitabu na nafasi katika maktaba na kuongeza mitambo na vifaa vya kufundishia katika karakana na maabara.

Kuna mpango wa kuongeza majengo ya madarasa,maabara na karakana,mabweni ya wanafunzi,numba za kuishi watumishi,kukarabati na kuboresha mifumo ya maji machafu,maji masafi na umeme na pia kukarabati na kuboresha barabara za ndani ya chuo na kuendelea kuwasiliana na halmashauri ya jiji la Mbeya kujenga barabara inayounganisha chuo na barabara kuu ya Mbeya-Tunduma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Prof Penina Mlama anasema pamoja na mafanikio yaliyopo bado kuna changamoto kubwa katika udahili wa wanafunzi wa kike.Anasema jitihada zaidi zinahitajika katika kuhamasisha jamii juu ya suala hilo.Huenda mfumo dume bado ni tatizo linalokwamisha jamii ya wanawake kujiunga na chuo hicho.

Hata hivyo Prof Mlama anasema kupitia utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano chini ya utawala wa rais Dk John Magufuli chuo kitaweza kufanya mambo makubwa zaidi.Iwapo katika kipindi cha miaka michache tangu kipewe hadhi ya chuo kikuu kimeweza kutoa zaidi ya wahitimu 2000 basi kwa miaka ijayo mafanikio makubwa yatarajiwe.

Anaahidi chuo hicho kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wenye kuzingatia falsafa muhimu ya Hapa Kazi Tu akisema ni yenye malengo ya kulijenga taifa na watu wake kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment