Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, March 22, 2023

Daraja la Bilioni moja lapeleka ligi daraja la nne Mwansanga na Tembela

 Na Mwandishi wetu,Mbeya.

 

UJENZI wa daraja la Mwansanga uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 umeanza kuleta neena kwa wakazi wa Kata za Mwansanga na Tembela baada ya Chama cha soka Mbeya mjini(Mufa) kuamua kituo cha hatua ya awali ya Ligi daraja la nne kufanyikia kwenye kata hizo.

 

Madiwani wa Kata ya Tembela,Frank Mwasyoke na wa Kata ya Mwansanga, Jelly Wokola walisema kujengwa daraja na barabara kumeanza kufungua milango kwenye maeneo yao na sasa wana imani wananchi wao wataanza kuneemeka na fursa kama ilivyokuwa kwa wakazi wa maeneo mengine.

 

“Naamini chama cha mpira kimependekeza uwanja huu ni baada ya juhudi za serikali kujenga daraja kubwa na la kisasa maana awali maeneo haya yalikuwa hayafikiki lakini sasa hivi kufika hapa Tembela na Mwansanga limekuwa jambo jepesi sana.”

 

“Tunamshukuru rais Samia kwa kutujengea daraja na pia mbunge wetu Dk Tulia kwa kuwa karibu nasi kunanikisha hili la ujenzi wa daraja. Na kwa chama cha mpira kuleta haya mashindano ni kuunga mkono juhudi za serikali.” Alisema Mwasyoke.

 

Diwani huyo alizitaja faida zitakazopatikana kwa kata hizo kupelekewa mashindano ya ligi daraja la nne kuwa ni pamoja na vijana kupata fursa ya kuonyesha vipaji vyao na pia yatafungua njia za kiuchumi kwa wakazi kufanya biashara kwakuwa yanavuta watu wengi.

 

Kwa upande wake Wokola aliwasihi wadau wa mchezo wa soka mkoani hapa wakiwemo viongozi wa timu za Tanzania Prisons,Mbeya City na Ihefu FC kufika kwenye michezo ya mashindano hayo ili kuvumbua vipaji vipya vya vijana wanaoweza kuwasjiri.

 

“Tumefurahi kwamba uwanja huu lazima utatoa vijana wenye vipaji. Tunao vijana wengi  kwenye maeneo yetu..wanakuwa wachezaji wazuri lakini hawaonekani..sasa kupitia mashindano haya na sisi tunaweza kupata vijana wanaokwenda kuchezea Mbeya City.”

 

Mwenyekiti wa Mufa,John Gondwe alisema ni kwa miaka mingi Kata hizo mbili zilikuwa hazipati fursa ya kushiriki mashindano ya ligi ya wilaya kutokana na changamoto ya usafiri hususani kutokuwepo kwa daraja.

 

“Baada ya serikali kwa kushirikiana na mbunge kuweka daraja tukaona huku sasa kumefunguka.. na tukaona na wenyewe tuwaletee hii fursa ya michezo.Walikosa burudani ya michezo kwa muda mrefu.Tunaona mwitikio ni mkubwa kama unavyoona kuna watu wanafanya pia biashara hapa uwanjani.” Alisema Gondwe.

 

“Ni wakati kwa wadau wengine wa michezo waje kutuunga mkono ili tuwezeshe maeneo haya yachangamke kama ilivyo kwa maeneo mengine ya jiji letu.” Aliongeza.

 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo timu zinazoshiriki ligi hiyo ni pamoja na Mbogo Mwansanga,Ilemi FC,Ilembo FC,Leopard FC zilizopo Kundi A, huku Kundi B zikiwa ni Mpaju FC,Sido FC,Ilemi FC na Icon FC.