Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, September 20, 2016

KUFUNGWA KWA MAFUNZO YA UONGOZI KWA ASKARI MAGEREZA KATIKA CHUO CHA MAGEREZA KIWIRA RUNGWE

  











Ofisi ya Madini Chunya na mchango wake katika sekta ya Madini.

Na Joachim Nyambo.

OFISI ya Madini Chunya kwa sasa inahudumia eneo lote la wilaya za Chunya mkoa wa Mbeya na Songwe mkoani Songwe.Huduma ni pamoja na Utafiti,uchimbaji na biashara ya madini.

Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa wilaya ya Chunya Ndege Bilagi,Ofisi ina jumla ya watumishi 12 wanaogawanyika katika kada za mhandisi wa migodi mmoja,mjiolojia mmoja,Fundi sanifu mmoja,mhasibu mmoja,madereva watatu,walinzi watatu,mwangalizi wa ofisi mmoja na katibu mhitasi mmoja.Watumishi wane kati ya hao ni wa mkataba.

Ofisi hii inafanya kazi za Idara ya Madini iliyo chini ya wizara ya nishati na Madini,inatoa taarifa yake ofisi ya madini Kanda iliyopo jijini Mbeya.Pia inatoa taarifa katika taasisi nyingine za serikali ikiwa ni pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za ofisi.

Ofisi inashirikiana na Halmashauri katika kutekeleza majukumu yake kwani shughuli nyingi za uchimbaji zinaingiliana na matumizi mengine ya rasilimali kama maji,misitu na ardhi.

“Baadhi ya shughuli zinazosimamiwa na ofisi ni pamoja na Kusimamia na kuratibu mfumo wa leseni wa Online Mining Cadastre Transaction Portal(OMCTP) kwa watumiaji wa leseni ikiwemo kuwasajiri,kuwafundisha wachimbaji au wateja namna ya kuomba na kuingiza maombi ya leseni kwa kutumia akaunti zao za barua pepe”anasema  Bilagi.

Shughuli nyingine ni Kusimamia uchimbaji wa awali(mdogo) wa madini ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za ugani(Extension Service) kwa wachimbaji wadogo.Kukagua usalama wa maeneo ya wachimbaji wadogo na wakubwa na Kutoa elimua ya uhifadhi wa mazingira kwa wachimbaji wadogo,wa kati na wakubwa.

Nyingine ni kutoa elimu kuhusiana na matumizi ya baruti na kusimamia au kuhakikisha kuwa sheria na matumizi ya baruti vinatekelezwa kwa ufasaha.Kukusanya Maduhuli ya aina mbalimbali ya serikali yatokanayo na shughuli mbalimbali za madini.

“Ofisi pia ainawajibika kukagua shughuli za utafiti wa madini zinazofanywa na wenye leseni kubwa za utafiti wa madini(prospecting licenses),kupokea taarifa za robo mwaka kutoka kwa watafiti madini wenye leseni kubwa na kuzioanisha ili kubaini kama taarifa hizo zinaendana na kazi iliyofanyika katika leseni husika”

“Kuna kusimamia shughuli za uchimbaji mkubwa ili kubaini kama Sheria na kanuni zinafuatwa.Kufanya ukaguzi wa shughuli zote za uchimbaji kwa lengo la kubaini ukiukwaji wa sheria,Kutoa vibali vya kusafirisha madini na sampuli zenye madini nje na ndani ya nchi na pia Kutoa vibali vya kuagiza Baruti,kukagua maghala ya kutunzia baruti”

“Kwa kifupi tunasimamia Sheria ya Madini ya mwaka 2010,sheria ya Baruti ya mwaka 1963 pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004” anasema Bilagi.

Uchimbaji mdogo wa madini

Bilagi anasema,Uchimbaji mdogo wa madini unafanywa na watanzania pekee ambao lazima wawe na leseni za awali za uchimbaji zijulikanazo kama Primary Mining Licenses(PMLs).Katika wilaya ya Chunya uchimbaji huu unafanyika katika maeneo yaliyogawanywa kwenye kanda.

Kanda ya Makongolosi kuna maeneo ya Mkola,Mapele,Gepu,Ujerumani,Chipoka na Kilombero wakati Kanda ya Matundani vipo vituo vya Kasisi,Kasakalawe,Itumbi Jeshini,Jobu Iti,Makatang’ombe,Idundu na Bwawani.

Kanda ya Chunya kuna maeneo ya Sinjili,Mlima Yasini,Mapogolo,Kiwanja,Mbugani,Itumba,Godima,Simba Reef,Simbachai,Safari Mine,Saitunduma,Simbadume,Majengo,Isenyela,Chalangwa,Nyatula,Mlimanjiwa,Kasanga Madini,Kasanga Market,Soweto na Mamusapu.

Maeneo mengine kwenye ukanda huu ni Mapapai,Ifumbo,Chikula,Kisu Mine,Magamba,Makoma,Mawelo,Mnyolima,Mwankonyonto,Shoga,Legezamwendo,Ilepuka,Chokaa,Mapunga,Majengo,Ihamba,Tukuyu,Sangambi,Izumbi na Kikavu.

Anasema wilaya za Chunya na Songwe zina wachimbaji wadogo wenye leseni za PMLs zipatazo 729.

Utafutaji wa Madini

Anasema Shughuli za Utafutaji wa madini zinafanyika kwenye leseni zinazojulikana kama Prospecting Licences(PL) katika  maeneo yote ya wilaya ya Chunya ili kubaini uwezekano wa kupata mashapo makubwa ya madini.

Ukanda huu wa madini unajulikana kwa jina la kijiolojia kama Lupa Gold Fields ambao una madini ya dhahabu na madini mengine ya Metali yaani Shaba,fedha,galena,chuma na mengineyo.Nje ya ukanda wa Lupa Goldfields kuna madini mengine kama rare earth elements(Metals),Magadi(Soda ash),madini ya vito na mengineyo.Wilaya hizi mbili zina jumla ya leseni za utafutaji madini 179.

“Kuna kituo cha Kufundishia wachimbaji wadogo cha Matundasi ASM kilichoanzishwa na serikali mwakaa 2005 ili kutoa elimu kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo.Kituo hiki kipo eneo la Matundasi ambapo mwaka 2008 kilibinafsishwa kwa mwekezaji kwa makubaliano na serikali ili akiendeleze. Kwa sasa mradi huo unaendelea na shughuli za uchorongaji miamba ili kubaini mashapo yatakayoweza kuanzisha mgodi darasa”anasema.

Uchimbaji Mkubwa

Uchimbaji mkubwa unafanyika katika maeneo mbalimbali na kuna leseni zipatazo tano katika eneo linalisimamiwa na Ofisi hii ya Madini ya Chunya.Kwa eneo la wilaya ya Chunya pekee kuna uchimbaji mkubwa unafanyika eneo la kata ya Matundasi ambapo kampuni ya Sunshine Mining Co Limited yenye leseni ya ucjenjuaji(processing licence) namba 00067/2013 na imeomba Mining Licence kwa maeneo yake mawili.

“Kwa sasa kampuni hii  imesimamisha shughuli zake ili kutengeneza miundombinu ya bwawa la maji machafu(Tailing Storage Facility-TSF).Vilevile tuna wachimbaji wengi wadogo ambao sasa mitaji yao na uchimbaji wao umekuwa kutoka kwa wachimbaji wadogo hadi kufika kuwa wachimbaji wa kati.Mfano ni Aidani Msigwa,Isack Msowoya na Elias Mwembe.”

Uzalishaji Madini na Ulipaji wa Maduhuli ya Serikali

Kwa mujibu wa sheria ya madini,Wachimbaji wakubwa na wadogo wanapaswa kulipa kodi za serikali ambazo ni Ada ya mwaka ya leseni,mrabaha wa asilimia nne kutokana na uzalishaji waa madini,ada za kubeba baruti,ujenzi wa maghala ya kuhifadhia baruti.Hivyo serikali kupata mapato kutokana na tozo hizo ambapo utaratibu ni kuwa fedha zinapaswa kulipwa benki moja kwa moja.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 hadi 2015/2016 Jumla ya Shilingi 1,888,642,319.66 zilikusanywa na Ofisi ya Madini wilayani Chunya ikiwa ni Mrabaha wa asilimia 4 wa madini aina ya dhahabu yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo wilayani hapa katika kipindi hicho.

Bilagi anasema katika kipindi hicho Jumla ya Gramu 821,113.16 za dhahabu zenye thamani ya jumla ya Shilingi 47,216,058,041.50 zilizalishwa katika migodi mbalimbali wilayani hapa hivyo kuwezesha serikali kujipatia shilingi 1,888,642,319.66 ikiwa ni mrabaha wa asilimia 4.

Akifafanua zaidi,anasema katika mwaka wa fedha 2010/2011 gramu 11,934.38 zenye thamani ya shilingi 668,325,550 zilizalishwa hivyo serikali ikajipatia mrabaha wa shilingi 26,733,020.

Mwaka wa fedha 2011/2012 gramu 14,693.80 zilizalishwa zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi 822,852,600 hivyo serikali ikajipatia shilingi 32,914,104.

Mwaka 2012/2013 zilizalishwa gramu 11,957.93 zenye thamani ya shilingi 669,643,800 hivyo serikali ikapata shilingi 26,785,752 na mwaka wa fedha 2013/2014 zikazalishwa gramu 68,508.93 zenye thamani ya shilingi 3,836,499,900 na serikali ikajipatia shilingi 153,459,996.

Anasema mwaka wa fedha 2014/2015 zilizalishwa gramu 405,587.81 zilizokuwa na thamani ya jumla ya shilingi 22,712,917,481 na serikali ikajipatia shilingi 908,516,699.24 na mwaka 2015/2016 gramu 308,430.31 zilizalishwa zikiwa na thamani ya shilingi 18,505,818,710.50 na hivyo serikali ikajipatia shilingi 740,232,748.42.

Utengaji wa Maeneo kwaajili ya wachimbaji wadogo

Akizungumzia Utengaji wa Maeneo ya Uchimbaji mdogo,Bilagi anasema Wizara ya Nishati na Madini ilitoa eneo la Itumbi B lenye ukubwa wa Kilometa za mraba 12.78 ambapo baada ya kufanyiwa michoro zaidi ya viwanja 300 vilipatikana.

Anasema pia kwa sasa Wizara imetenga maeneo ya Mbugani na Chalangwa na mpango wa kuyagawa maeneo hayo utafanyika mara baada ya Wakala wa Jiolojia Tanzania(GST) atakapofanya kazi ya Utafutaji wa awali ili kubaini uwepo wa mashapo ya madini.

Changamoto zinazoikabili Ofisi
 Kwa mujibu wa Bilagi Ofisi ya Madini Chunya inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kimsingi zinakwamisha utendajikazi.Changamoto hizi ni pamoja na Ukosefu wa rasilimali fedha za kuendesha ofisi.Hii imesababisha kusimama kwa shughuli nyingi za nje ya ofisi(field activities) kama ukaguzi kwa wachimbaji,watafutaji madini,kutoa semina katika vijiji na pia kudhibiti wachimbaji haramu.

Umiliki na matumizi holela ya  Baruti ni changamoto nyingine inayohatarisha maisha ya wachimbaji wadogo wa madini,familia zao na majirani wilayani Chunya.Bilagi anasema baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakitunza baruti majumbani mwao,madukani na baadhi husafiri nazo kwenye gari zao.

“Uhifadhi huu holela ni hatari kwa maisha ya wachimbaji hao,familia na majirani zao kwakuwa inaweza kusababisha mlipuko na kuwadhuru watu wanaokuwa jirani”.

Anasema changamoto nyingine iliyopo ni baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali za vijiji kuingilia shughuli za ofisi ya madini hasa pale wanapotoa vibali kwa wachimbaji kinyume cha sheria.Baadhi yao wamekuwa wakaidi hata wanapoelimishwa na badala yake wamekuwa wakichochea migomo kwa wananchi ili wasikubali kutii sheria ya madini ya mwaka 2010.

“Tuna changamoto pia ya baadhi ya wanakijiji kujimilikisha maeneo ya kuchimb kwa kisingizio kuwa madini yapo katika mashamba yao.Vile vile hali hii imesababisha baadhi ya wachimbaji wanaomiliki leseni kisheria kushindwa kuchimba maeneo yao kwa kuhofia kufanyiwa vurugu na wenyeji”

 “Bado pia uchimbaji wa kuhama hama unaendelea.Hii inasababishwa na wachimbaji wengi kutokuwa na mitaji ya kutosha ya kufanya utafiti wa kugundua kama maeneo wanayoombea leseni yana mashapo ya madini ya kutosha ili wachimbe” alisema Bilagi.

Kuwepo kwa Utitiri wa kodi na tozo nyingi kwa wachimbaji wadogo nalo linatajwa kama changamoto kubwa.Baadhi ya taasisi zinatoza kodi kubwa zinazoleta manung’uniko kutoka kwa wadau wa shughuli za madini.Mfano watu wanaosaga mawe wanatakiwa kulipa TRA shilingi 700,000 kwa mwaka,wakilipe kijiji kuanzia kiasi cha shilingi 15,000 hadi 20,000 kwa mwezi na wanatakiwa walipe ushuru halmashauri ya wilaya.

Wachenjuaji wanalalamikia kodi ya zimamoto ambapo hadi baadhi yao waliwahi kuwekwa mahabusu wakiamriwa kulipa shilingi 5,000,000 kwa mwaka kama ada ya zimamoto huku wachimbaji wakiwa hawapati huduma yoyote kutoka jeshi hilo.Kero kubwa ni namna taasisi husika inavyoidai kwa njia ya shuruti kabla ya kuwaelimisha.

Bilagi anasema katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto,serikali kupitia ofisi ya madini wilaya imeendelea kutoa Elimu kuhusu sheria ya Madini ya mwaka 2010 ili wananchi waweze kutambua kuwa unapomiliki ardhi hauna ruhusa ya kumiliki madini yaliyopo bila kufuata sheria.

Anasema pia Elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi na wachimbaji juu ya namna bora ya kumiliki na kutumia baruti kwa mujibu wa Sheria ya Baruti ya mwaka 1963

Afisa huyo anasema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuinua hali ya wachimbaji wadogo ili wasiwe wa kuhama hama hivyo imeiwezesha wakala wa Jiolojia Tanzani(GST) ili wafanye utafutaji wa awali wa mashapo yenye madini katyika maeneo mbalimbali nchini na Chunya ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele.

“Serikali ina mpango wa kujenga kituo kingine cha kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika kata ya Mbugani ili wawe na weledi wa uchimbaji wenye tija.Tunaendelea kutoa huduma ya kuandikisha wananchi katika mfumo wa leseni wa OMCTP ili kila mchimbaji aweze kuomba leseni bila ya kuwa na ulazima wa kufika ofisi ya madini”

Anasema kuhusu utitiri wa kodi Ofisi ya madini Chunya ilikwisha wasilisha kwa Kamishna wa Madini.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla alipotembelea shughuli za madini na kukutana na wadau wa Sekta hiyo aliahidi kuendelea kupigania haki za wachimbaji wa madini ili kupunguza adha zinazoikabili sekta hiyo wilayani hapa.

Monday, September 19, 2016

ELISABENE,SHULE ILIYOANZISHWA KUTOKANA NA MISUKOSUKO YA KIFAMILIA KIELIMU

Na Joachim Nyambo.

“Yapo mambo mengi yaliyonisukuma kuanzisha shule” Ni sentensi aliyoanza nayo Anivene Lusubilo nilipozungumza naye.Huyu ni mmoja wa wakurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya mchepuo wa kingereza ya Elisabene iliyopo mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.Mkurugenzi mwenza ni mumewe Frank Shitindi.

Ipo historia ndefu kwa familia ya wanandoa hawa hata kufikia hatua ya kuwa na taasisi ya kutoa elimu ambayo sasa imekuwa manufaa kwa jamii pia inayowazunguka na kwingineko nchini nchini.Ni familia yenye watoto wane wote wakiwa ni mabinti.

“Msukumo wa kwanza nilianza kuupata kutokana na mimi mwenyewe kupata elimu kwa kuungaunga sana.Hii ilitokana na wazazi wetu kutotambua sana umuhimu wa elimu”

“Suala la pili ninaye binti yangu ambaye mara baada ya kumaliza darasa la saba na kupata matokeo mabaya nilihangaika sana kupata shule ya sekondari ya kumpeleka.Nilimpeleka shule tano binafsi lakini kila alipofanya usaili alionekana kushindwa.Nilichokibaini ni kuwa alishindwa kutokana na kuwa na uwezo mdogo wa lugha ya kingereza.Iliniumiza sana,nikawaza halii kama hiyo ikoje kwa jamii inayonizunguka!” alisema Anivene ambaye ni mtaalamu wa Kilimo katika halmashauri ya mji wa Tunduma.

“Watoto wote waliofaulu kwenye usaili uliofanyika kwenye shule nilizompeleka mwanangu nilibainia walitokea katiak shule binafsi.Nikaona walimu katika shule hizi wanajituma kutokana na kutetea ajira zao hivyo mwanafunzi atapewa elimu inayostahili.Katika shule za serikali wapo walimu wanaobweteka na kuona hana cha kupoteza mtoto anapokuwa na maendeleo mabaya kitaaluma”

Anasema hapo alianza kufikiria kupeleka watoto wake wote kwenye shule za michepuo ya Kingereza ili wasikumbwe na adha iliyomkuta dada yao.Alimshawishi mumewe na walianza kuwekeza kidogo kidogo fedha kutoka katika sehemu ya mishahara yao ya kila mwezi.

 “Niligundua gharama haikuwa kubwa sana kumsomesha mtoto katika shule hizi.Nilimshawishi mume wangu kila mmoja wetu atenge shilingi elfu ishirini katika mshahara wake wa kila mwezi.Tukajikuta tunaweza.Yule aliyekuwa darasa la nne na mwezie wa darasa la kwanza tukawapeleka wote English Medium katika shule moja iliyopo hapa mkoani kwetu lakini wilayani Mbozi.”

Anasema kuwapeleka watoto katika shule hiyo ya mchepuo wa kingereza kukampa fundisho jingine ambalo lilizidi kumpanua mawazo na kuzidisha nia ya kutafuta ufumbuzi.Mazingira aliyokutana nayo yakaonekana kutomridhisha kama mzazi.

“Kwakweli pamoja na watoto kuendelea kusoma pale sikuweza kuwa na amani kwakuwa kila tulipokwenda kuwasalimia watoto hatukuridhishwa sana na mazingira tuliyokutana nayo.Masuala ya lishe,malazi na pia mazingiara ya shule kwa ujumla.Tukaona kuna kila dalili za watoto kuambukizana magonjwa kwa urahisi.Hapo tukaamua kuwahamishia katika shule moja iliyopo jijini Mbeya.”

Wakati haya yakifanyika suala la uchungu wa mzazi kuishi mbali na watoto wake nalo likajitokeza.Anivene akajikuta anakuwa mpweke kwa watoto wake kuishi mbali nae.Akahisi watoto pia hawana imani kutokana na kuishi kwao mbali na wapendwa wazazi wao.Akahisi kuna mambo muhimu wanayakosa.

“Hakuna siku niliyoumia kama nilipokuwa namwacha mtoto wangu wa mwisho anakwenda kuanza darasa la awali.Kilikuwa kitoto kidogo mno chenye miaka sita.Kilipoanza kulia nikajikuta na mimi nabubujikwa na machozi.Nilikosa raha hata baada ya kuwa nimemwacha shuleni.Nilijua uangalizi ni mzuri lakini nikawaza namba amekuwa akifurahi kila tuamkapo asubuhi.Nikaona furaha yake sasa itakuwa imepotea na huenda hata masomo ikawa shida kwake.nilibeba uchungu wa wanawake wote wa eneo hili”.

Wakati huo wote alikuwa akijaribu kutafakari ni kwanini watu wenye uwezo kwenye maeneo ya jirani hawajataka kuanzisha shule kama hizo wanazozifuata mbali ili watoto waweze kusoma jirani na makwao?Mji wa Tunduma una wakazi walio na vipato vizuri kutokana na wengi wao kuwa wafanyabiashara wakubwa.Lakini hawakutaka kuwekeza katika suala la elimu.Wote wakawa wanapeleka watoto mbali nao.

“Iliniuma sana lakini ikanibini kuja na wazo jipya.Ili uweze kuanzisha shule yakupasa uwe na vigezo gani.Hapo ndipo nilipoanza mchakato wa kufuatilia vigezo vinavyohitajika mpaka pale niliporuhusiwa na serikali”

Anasema hapo ndipo alipoanza kujenga majengo kwenye eneo lake lililopo katikati ya mji wa Tunduma ambako kwa sasa yapo madarasa ya shule ya awali pekee.Mwaka 2012 baada ya kukamilisha majengo hayo nikaanza kuwaza napataje walimu wa kuanza nao.Mtaji umeishia katika kujenga majengo na kuboresha mazingira.

“Nilihitaji muda wa kujipanga zaidi mpaka kufikia kuanza kuajiri na kupokea wanafunzi.Madhari niliyokuwa nimeweka yanayovutia watoto kwa kuwepo na bembea siku moja yakaniponza.Siku hiyo watoto wawili wa rafiki yangu waliokuwa wakisoma katika shule moja hapa mjini waligoma kwenda shuleni kwao.Walimlazimisha mama yake awalete kwenye majengo yetu na wakasema hawatokwenda shuleni kwao iwapo mama yao hatokubali ombi lao.”

“Mama yao alinipigia simu kuniomba awapeleke kwenye majengo yetu nikamwambia haiwezekani sisi hatujaanza kufanya kazi hivyo hatuwezi kuruhusu.Badaye alipoona wanamsumbua sana akanipigia tena simua akanambia kwakuwa pale kuna walinzi anawapeleka hivyo hivyo ili wakashinde huko wao wafurahi”

“Wakati akinambia hayo alikuwa tayari njiani kuelekea huko.Sikuwa na namna zaidi ya kumkubalia.Nilimpigia mlinzi akawafungulia geti na kuwaruhusu kuingia na mama yao akawaacha hapo.Mpaka nakwenda niliwakuta wanaendelea kucheza wala hata hawakujali kuwa walikuwa peke yao”anasema.

Anasema hapo akawa na mtihani mpya.Ili mlazimu atumie pesa yake ya mfukoni kuwanunulia chipsi kwenye kibanda kilichopo jirani kwaajili ya chakula cha mchana.Baadaye mama yao aliwapitia watoto hao na kurudi nao nyumbani.Kesho yake hali ilikuwa hivyo hivyo,watoto waligoma kwenda shuleni kwao ikabidi waletwe shuleni hapo.

“Nikawa na kibarua kigumu.Watoto wa watu wanasinda kwenye majengo yangu,hakuna mtu wa kuwasimamia,nikaona nina wakati mgumu.Ilibidi nikutane na mzazi wao ili tulijadili jambo hili kwa pamoja.Ajabu hakuwa na hofu kama yangu!Akanambia wewe unasubiri nini kutafuta walimu?akasema tafuta mwalimu aanze kuwafundisha watoto mimi nitakutafutia wanafunzi wengine kama unashindwa kuwatafuta”

“Nikaona mbona huyu simwelewi!Lakini nikaona huenda huu ndiyo mwanzo wenyewe.Akanitafutia mwalimu mmoja anaitwa Sarafina.Sikuwa na kwa kumweka ikabidi niishi nae nyumbani kwangu.Rafiki yangu akashawishi wafanyabiashara wakaniletea watoto wengine wawili.Hapo nikawa na wanafunzi wane.Kwakuwa usajiri  wa shule tulikuwa tumepata tayari hatukuwa na mashaka.”

Anasema baadaye waliopata mwalimu mwingine raia wa Kenya.Lakini hakuweza kudumu shuleni hapo kwakuwa baadaye ilibainika hakuwa ametimiza masharti ya kufanya kazi nchini hivyo aliondoka.Walilazimika kuendelea kudunduliza walimu.

“Unajua tatizo kubwa tulilonalo hapa nchini ni kupata walimu walio na uwezo.Si kwamba walimu hawapo!wapo wengi tu lakini uwezo ni tatizo.Na hii ndiyo inasababisha shule zetu kuwa na ushindani mkubwa wa kuwapata walimu wenye kuiwezesha taasisi yako kufanya vizuri”

Anasema kupenda kwake kujifunza kulimfanya azidi kupanua wigo wa uelewa kila mara aliposafiri.Alipenda kutembelea shule mbalimbali zinazotoa elimu sawa na ya shuleni kwake.Na kila jambo jipya alilojifunza aliangalia namna ya kuliongeza kwenye taasisi yake.

“Kutokana na ugumu wa kupata walimu kuna wakati ilinilazimu kwenda Dar es salaam na kukaa huko kwa majuma mawili nikiwatafuta wanaoweza kuja kunisaidia.Hapo ndipo nilipokutana na mwalimu David Buyogela ambaye sasa ndiye Mkuu wa shule.Nakumbuka ilikuwa mwaka 2013.Wakati huo pia mpaka nafanya mazungumzo na mwalimu huyu nilikuwa naumwa na kabla sijarudi ilibidi nifanyiwe upasuaji”

Kwakuwa mtazao wa familia hii ulikuwa ni kuwa na shule ya awali na Msingi zilizokamilika,waliamua kutumia eneo walilokuwa nalo nje ya mji kidogo litumike kwaajili ya kujenga shule ya msingi.Hapo ujenzi ulianza na baada ya kuziona taasisi za kifedha zikakubali kutukopesha fedha.

Anivene anasema kujua namna ya kutawala imekuwa chachu ya mafaniko kwenye taasisi yao kwani hadi sasa walimu na wanafunzi wamezidi kuongezeka.Wapo wanaohamia wakitokea katika shule nyingine na pia wale wanaoanza awali kila mwanzo wa mwaka wa masomo.

Mkuu wa shule mwalimu Buyogela anasema hivi sasa shule ina jumla ya wanafunzi 255 kwa maana ya kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu.Darasa la awali wapo 114  wasichana wakiwa 58 na wavulana 56,darasa la kwanza wako 71 wavulani 37 na wasichana 34.Darasa la pili waapo 54,wasichana 31 na wavulana 23 na darasa la tatu wako 16 wasichana 11 na wavulana watano.

“Wapo watoto wanaohamia kutoka shule nyingine.Hawa tunawasaili na kuona uwezo wao iwapo unaridhisha anaendelea na darasa alilokuwa huko alikotoka na iwapo tutaona kiwango chake hakiridhishi tunaongeza na mzazi au mlezi kumrejesha darasa moja.Lengo ni kumjengea uwezo kitaaluma aweze kwenda sambamba na wenzie darasani” anasema Buyogela.

“Kama watumishi tumekuwa na jambo la kujivunia kutokana na mahusiano mazuri baina yetu na mwajiri.Baadhi ya waajiri hawapedi kupokea maoni ya wafanyakazi wao.Kwa hapa hali ni tofauti,tunasikilizwa na tunajiona sehemu ya taasisi.”

Baadhi ya wanafunzi shuleni hapa Tecla Almasi,Moses Ndaga na Jesca Korogwe wote wa darasa la tatu,wanasema mazingira ya utoaji elimu yanayokwenda sambamba na kupata chakula yanawawezesha kupata fursa nzuri ya kuwaelewa walimu wao.

 Tecla na Moses wanasema walihamia shuleni hapa wakitokea shule tofauti lakini tofauti na walikotoka hapa wameongeza uwezo kitaaluma.Wanasema huenda mazingira ya walimu kuwajali na uwepo wa miundombinu rafiki ya kufundishiwa imekuwa chachu ya mafanikio yao tofauti na awali.

Uwepo wa uwekezaji shule ya Elisabene umekuwa chachu ya maendeleo kwa watu mbalimbali.Zipo ajira zilizozalishwa kama za walimu,madereva,wapishi,walinzi,watu wa usafi na utunzaji bustani,ujenzi wa majengo,ufyatuaji tofali na nyingine nyingi.

“Wananchi waishio jirani na shule pia tunawapa maji kutoka katika kisima kirefu tulichochimba hapa shuleni.Tunashiriki pia katika shughuli za kijamii kwa kuchangia michango mbalimbali.Tunaamini jamii inayotuzunguka ni sehemu yetu” anasema mkuu wa shule.

Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado kuna changamoto zinazoikabili shule hii.Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na mtoto kuletwa akiwa amechelewa kuanza shule,mzazi kutaka mtoto aingie darasa la juu japo hana uwezo akiona kumrudisha darasa atapata hasara.Pia kutokuwepo kwa hostel kunasababisha wanafunzi kukosa muda wa kutosha kupumzika akiwa katika mazingira ya shule.

“Kama watumishi tunataraji utawala unafanyia kazi suala la Usafiri wa watumishi,kujenga nyumba za wafanyakazi,Kujenga hosteli,kupata fursa ya kujiendeleza kielimu,kushiriki semina za mara kwa mara ili kujijengea uzoefu na pia kutuunganisha na taasisi za kifedha ili kupata mikopo na pia mifuko ya kijamii”anasema Buyogela.

Mkurugenzi wa shule anasema changamoto za kiutawala ni pamoja na wazazi kutolipa ada kwa wakati licha ya kuwa wazazi wengi wanao uwezo mzuri kiuchumi,upatikanaji wa walimu,kutofikiwa kwa miundombinu ya maji na maji katika eneo la shule ya msingi hivyo kulazimu kutumika kwa jenereta na kisima cha kuchimbwa.Taasisi za kifedha kutoza riba kubwa kwenye mikopo.

“Tuna changamoto kubwa ya mtazamo hasi wa serikali juu ya fedha binafsi,inaamini kuwa zinapata faida kubwa na hapo ndipo tunapolundikiwa mzigo wa kodi lukuki zikiwemo za majengo,TRA,fedha za ukaguzi,kulipia majengo.Hapa tunaona kama hakuna mahusiano mazuri baina ya serikali na shule binafsi”

“Lakini kuna suala la wazazi kutowajibika na watoto wao.Wapo ambao hawajawahi kufika hapa shuleni tangu watoto wao waanze kusoma hapa.Hawaulizii maendeleo ya watoto wao na wala hawawaandai watoto wanapokuja shule.Mtoto anakuja ukimuona tu utajua huyu anaumwa lakini unapompigia mzazi anakuwa hajui lolote na amemruhusu aje shule siku hiyo.Mtoto mwingine utakuta amekuja na nguo chafu ni kama hakutokea kwa mzazi.Hii yote ni kutokana na wazazi kutowajali watoto” anasema Anivene.

Mkurugenzi huyu anasema matarajio ya taasisi hii ni kujenga hosteli ili watoto waweze kukaa shuleni japo ni kwa wale watakaopenda.Japo hii ni changamoto kwake kwani awali alipenda mtoto aje kusoma na jioni aungane na familia yake.

Kuanzisha shule ya sekondari kutategemea mwenendo mzuri wa mafanikio ya shule ya msingi.Japo ni muhimu kwakuwa itasaidia watoto wanaomalisha shuleni hapo kuendelea na masomo ya sekondari wakiwa katika mazingira waliyoyazoea tofauti na kwenda shule nyingine.

Mtazamo wa Serikali ya mkoa wa Songwe ni kuona uwekezaji katika Nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu unaimarishwa.Hii itasaidia jamii ya wakazi mkoani hapa kujikwamua na kuondokana na maadui Ujinga,Maradhi na Umasikini pale watakapokuwa na elimu ya kutosha.

“Tunataka kuwaondoa wakazi wa mkoa wa Songwe kwenye Unyonge.Wana fursa nyingi za uzalishaji mali lakini bado ni wanyonge na ili kuwaondoa kwenye hali hii lazima tuwape elimu”alisema mkuu wa mkoa wa SongweLuteni mstaafu Chiku Galawa alipozungumza na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI).

Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa,George Mbijima,alipokimbiza mwenge shuleni hapa alipongeza waasisi wa shule ya Elisabene akisema jamii inapaswa kujikita katika uwekezaji wa kujikomboa kutoka kwenye adui Ujinga.