Na Joachim
Nyambo.
MAGONJWA ya
Matende na Mabusha(Ngirimaji),Minyoo ya Tumbo,Kichocho,Trakoma na Usubi ni
miongoni mwa magonjwa yanayoiathiri jamii na kuidhoofisha.Inakadiriwa kuwa watu
bilioni moja duniani kote tayari wameathiriwa.Zaidi ya watu bilioni mbili wako
hatarini kupata magonjwa hayo.
Nchini Tanzania
tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa maambukizi ya magonjwa haya hupatikana karibu
maeneo mengi.Licha ya uwepo wake ndani ya jamii yalikuwa hayapewi kipaumbele
kwenye mikakati ya kupambana na maradhi.Jamii masikini zinatajwa kuathirika
zaidi na magonjwa haya.
Afisa Mradi wa
Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbelea kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Dk.Edward Kirumbi
anasema magonjwa mengine yaliyopo kwenye kundi hili ni pamoja na Kichaa cha
mbwa,Homa ya Papasi,Malale na Tauni.
Dk.Kirumbi
anasema magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yapo kwenye jamii zetu.Kwa muda
mrefu yalikuwa hayapewi umuhimu stahili
na wadau wa huduma za afya kama ilivyo kwa magonjwa mengine kama ilivyo
kwa Malaria,Ukimwi na mengineyo.Hayakupewa umuhimu kutokana na athari zake
katika jamii.
“Kila mtu yuko
katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa haya endapo hatazingatia ushauri
wa kitaalamu” anasema Dk Kirumbi.
Nini uambukizi
wa magonjwa haya.
Dk Kirumbi
anasema Usubi husababishwa na minyoo iitwayo Onchocerca Volvulus.Minyoo hii
huenezwa nzi wadogo weusi wanaokaa kandokando ya mito iendayo kasi.Ugonjwa huu
husababisha ngozi kuwasha au ngozi kuwa na mabaka mabaka mithili ya mamba au
mjusi.
Matende na
Mabusha(Ngirimaji) husababishwa na minyoo aina ya Wucheria Bancrofti
inayosababishwa na Mbu.Anasema minyoo hii huishi kwenye mfumo wa maji ya
damu.Ni ugonjwa unaosababisha kuvimba kwa miguu,mikono na sehemu za siri.
Kichocho
Husababishwa na minyoo aina ya Shistosoma.Konokono anaeneza ugonjwa huu kwa
kutoa vimelea kwenye maji yaliyotuwama na binadamu huambukizwa kwa kugusa maji
hayo..Kichocho husababisha damu kutoka kwenye mkojo na choo.Pasipo tiba ya
haraka baadaye kichocho kinaweza kusababisha Saratani ya tumbo,kibofu cha mkojo
na ini.
Minyoo ya tumbo
ni minyoo iliyopo katika aina tatu.Minyoo mviringo,Minyoo mjeledi na Minyoo
Safura.Minyoo hii huishi ndani ya tumbo.Isipotibiwa mapema husababisha mwili
kuwa dhaifu,upungufu wa damu,utumbo kujifunga na hata kifaa.Pia inaweza
kumfanya mtoto kushindwa kuhudhuria shule au kuelewa vizuri masomo.
Trakoma
Husababishwa na bacteria aina ya Chlamydia Trachomatis wanaosambazwa na nzi na
pia kwa njia ya kugusana baina ya mtu na mtu aiwapo mmoja wao ana maambukizi.Trakoma
isipotibiwa mapema husababisha upofu.
Malae
husababishwa na vimelea aina ya Protozoa anayeitwa Trypanasoma.Huenezwa na
Mbung’o.Ugonjwa huu husababisha udhoofu wa viungo vya mwili,kuuma mwili,kichwa
kuuma,kuvimba tezi za shingo,kuchanganyikiwa,kulala mara kwa mara, hasa mchana
na kukosa usingizi usiku.
Tauni ni ugonjwa
unaosababishwa na bacteria aitwaye Yersinia Pestis.Bakteria hawa husambazwa na
viroboto vya panya.Dalili za ugonjwa huu ni homa kali,maumivu ya mitoki(tezi)
na mwili kuchoka.
Kichaa cha
Mbwa,Ugonjwa huu husababishwa na virusi.Binadamu anaambukizwa baada ya
kung’atwa na Mbwa au wanyama wengine wa jamii hiyo kama Mbweha na paka walio na
ugonjwa huo.Pia binadamu anaweza pia kuambukizwa kwa kugusa mate ya mnyama
mwenye ugonjwa huu.Dalili za Kichaa cha Mbwa ni homa,kichwa kuuma,mwili
kuchoka,kushtuka,kuchanganyikiwa,kupoteza fahamu,kuogopa maji,upepo na wakati
mwingine kushindwa kutembea.
Homa ya Papasi
Husababishwa na bacteria aina ya Borrelia.Bakteria hawa huenezwa na
Papasi.Dalili za ugonjwa huu ni homa kali,kichwa kuuma,mwili kuchoka na pia
kutapika.
“Njia za
kujikinga na magonjwa haya ni pamoja na Kutumia dawa za kutibu na kudhibiti
magonjwa haya ambazo hutolewa kila mwaka katika jamii iliyoathirika.Kuzingatia
usafi wa uso na mwili kwa ujumla ni jambo muhimu” anasema Dk Kirumbi
“Jamii inapaswa
kuzingatia usafi wa mazingira kwa ujumla na pia kutokuoga,kutokuogelea wala
kutotembea kwenye maji yasiyo safi na yaliyotuama kama vile mabwawa na
mifereji.Tunapaswa kujikinga na kuumwa na nzi,Mbung’o,mbu na wadudu wengine
wasambazao magonjwa haya.Matunda na Mbogamboga zioshwe vizuri na maji safi na
salama kabla ya kuliwa.Lakini pale tunapokuwa tumepata maambukizi tayari ni
muhimu kutibiwa haraka.”
Anasema utoaji
wa chanjo kwa wanyama kama mbwa ni muhimu sana.Hii ni kwa manufaa ya jamii yote
kwakuwa mbwa aliyechanjwa si rahisi kuwa na virusi vya ugonjwa wa kichaa
vinavyoweza kumpata mtu yeyote iwapo mnyama huyo atamng’ata.
Nini mikakati ya
Udhibiti na kutokomeza magonjwa haya.
Afisa mradi huyo
anasema magonjwa ya Usubi,Matende na Mabusha(Ngirimaji),Trakoma Vikope,Kichocho
na Minyoo ya tumbo hudhibitiwa moja kwa moja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti
Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbelea kwa njia ya kugawa dawa za kuzuia na
kukinga maambukizi ya magonjwa haya.Dwa hutolewa kila mwaka mara moja kwa jamii
katika mikoa na wilaya zilizoathirika.
“Magonjwa
mengine yakiwemo,Malale,Kichaa cha Mbwa,Tauni,Homa ya Dengu,Homa ya Papasi,Kifua
kikuu na Ukoma hushughulikiwa na mpango huu kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali” anasema.
Praziquantel ni
dawa inayotibu na kukinga Kichocho cha Tumbo na Kichocho cha Kibofu cha mkojo,Zithromax
ya vidonge na maji inatibu na kukinga Trakoma.Albendazole na Mectizan zinatibu
na kukinga Matende,Usubi na Minyoo ya tumbo.
Manufaa ya dawa
hizi zikitumika kwa usahihi ni pamoja na Kupunguzamaambukizi kutoka kwa mtu
mmoja kwenda kwa mwingine,kuua vimelea vya magonjwa haya,kukinga upungufu wa
damu,kukinga,kupunguza maumivu na athari zinazosababishwa na magonjwa haya,kuboresha
nguvu kazi katika jamii,kuwezesha watoto kukua vizuri kimwili na kiakili na pia
kuongeza mahudhurio ya watoto shuleni na uweza wa kuelewa masomo.
Kila mwananchi
anayestahili anatakiwa kumeza dawa za kutibu na kuzuia magonjwa haya mara moja
kila mwaka.Itawezesha vimelea vilivyo ndani ya mwili kufa na maambukizi
hayataendelea.Kutokana na ukweli huu kila mwananchi anapaswa kujitokeza kupata
dawa za kutibu magonjwa haya katika siku maalumu zinazopangwa na kutangazwa
katika jamii.
Hivi karibuni katika
warsha ya Uraghibishi na Uhamasishaji juu ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele iliyofanyika mkoani Mbeya,Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
alisema haya ni magonjwa ambayo
yanaathiri jamii ya watu hususan jamii yenye
kipato cha chini, wananchi wake wanaishi katika maeneo duni, maeneo ambayo hata upatikanaji wa huduma za afya ni mgumu.Kiwango cha maambukizi ya magonjwa haya
katika jamii ni kati ya asilimia 1 hadi asilimia 87.6 kitaifa.
“Pamoja na
athari nyingine,Magonjwa haya pia husababisha usumbufu mkubwa kwa waathirika
wake na yanaongeza matumizi ya
rasilimali chache tulizonazo katika kuyakabili kwa gharama kubwa mno. Pamoja na
athari zote hizo, waathirika wa magonjwa haya
wakabiliwa na unyapaa katika jamii.”
“Ombi langu
kwenu Wakurugenzi wa Halmashauri, ni kwamba muhakikishe Mpango huu unaingizwa
katika Mpango Kabambe wa Halmashauri na kutengewa fedha za kutosha, ili tusiwe
tegemezi kwa wahisani tu.”
“Lakini,
vilevile Wakurugenzi na maafisa wote mnaohusika na mchakato wa kuzitoa fedha
hizi wilayani mpunguze ukiritimba ili fedha itoke kwa wakati na kuwezesha
shuguli kufanyika kwa wakati uliopangwa.”
“Rai yangu kwa
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wa ngazi
zote ni kwamba msimamie kikamilifu zoezi
la umezeshaji dawa kwa kinga –tiba ya magonjwa haya, ili Mkoa wetu mwaka huu na
miaka ijayo uweze kupata “coverage” nzuri ya umezaji dawa.”
“Pia ni muhimu
kwa wananchi wote kumeza dawa hizi za Kinga-tiba kama wanavyoelekezwa na wataalam
wakati wa Kampeni husika. Dawa hizi zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani
pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini kuwa ni salama na hazina Madhara
yeyote.”alisisitiza Kandoro.
Muandaaji wa Makala haya anapatikana kwa namba 0756 40 95 97, Email nyambojoachim@gmail.com
No comments:
Post a Comment