VURUGU
zilizoibuka Julai 18 mwaka huu na kudumu kwa siku mbili katika kijiji cha Lupa
wilayani Chunya mkoani Mbeya zimesababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya zaidi
ya shilingi milioni 30.
Uharibifu
huo ulitokana na kuchomwa kwa gari yenye namba T 882 ANM Toyota Landcruiser
yenye thamani ya shilingi milioni 20 na nyumba yenye thamani ya shilingi
milioni 10 iliyoteketea pamoja na vitu vyote vilivyokuwa ndani vyote vikiwa ni
mali ya Masagija Jilala(40) mkazi kijijini hapo.
Kwa
mujibu wa kamanda wa polisi mkoani hapa Diwani Athumani wakazi wa kijiji hicho
ndiyo walichoma mali hizo ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi kutokana na baba wa
Masagija aliyefahamika kwa jina la Jilala Kamonga(88) ambaye ni kiongozi wa
askari wa jadi(Sungusungu) kuamuru askari hao kuwakamata watu wataatu
waliotuhumiwa kuiba ng’ombe watatu.
Kamanda
Athumani alisema mnamo julai 18 majira ya saa 3:30 asubuhi katika kijiji hicho watu
watatu walituhumiwa kuiba ngo’mbe watatu mali ya Edward Helbert(32),Masagija
Kamaga(40) na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Mohamed.
Aliwataja
watuhumiwa wa wizi huo kuwa ni Kadoda Kayombo(40) na Msafiri Mgaya(38) wote
wakazi wa kijiji cha Lupa na Makula Mfanyange(28) mkazi wa kijiji cha Ng’ung’ungu.
Alisema
baada ya kutuhumiwa kundi la askari wa sungusungu waliwakamata watuhumiwa na
kuwapeleka msituni walikoanza kuwatesa kwa kuwapiga.
Kamanda
Athumani alisema baada ya wananchi kuona watuhumiwa waliokamatwa hawarejeshwi
kijijini na hakuna taarifa za kuwapeleka polisi walijichukulia sheria Julai 19
saa 1:30 usiku kwa kuvamia nyumba ya mtoto wa Mtemi wa sungusungu na kuchoma
nyumba na gari yake.
Hata
hivyo alisema watuhumiwa wa wizi waliokuwa wamekamatwa walipatikana baadaye
msituni wakiwa wametelekezwa na kufikishwa hospitali ya wilaya ambako walipata
matibabu na kuruhusiwa.
Kufuatia
hali hiyo kamanda huyo alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka sungusungu waliohusika pamoja na
wananchi waliochoma moto gari na nyumba.
No comments:
Post a Comment