Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, October 27, 2013

AFA MAHAKAMANI AKISIKILIZA KESI YA MWANAYE

MAHAKAMA ya wilaya ya Rungwe juzi ilijikuta inasitisha kwa dakika kadhaa kusikiliza kesi baada ya mkazi wa kaya ya Masukuru wilayani hapa aliyefahamika kwa jina la Tiger Mwaigomole (70) kufariki dunia ghafla akiwa ndani ya chnumba cha mahakama wakati mashitaka yakiendelea. Mwaigomole alianguka ghafla mahakamani hapo na kufariki dunia alipokuwa akiendelea kufuatilia kesi ya kupigana na kujeruhi inayomkabili mtoto wake anayefahamika kwa jina la Gwakisa Tiger(40) iliyokuwa ikiendelea mahakamani hapo. Tukio hilo ambalo ni nadra sana kutokea,lilitokea majira ya saa 9 alasiri ndani ya Mahakama hiyo ambapo marehemu alifika mahakamani hapo akiwa na mwanaye aliyejulikana kwa jina la Lusajo Tiger wakiwa na lengo la kumwekea dhamana Gwakisa Tiger ambaye alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa kwa kosa la kupigana na kujeruhi katika ugomvi uliotokea kijijini kwao. Kwa mujibu wa Lusajo wakati kesi ikiendelea mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Omary Kingwele, ndugu yao alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili ndipo marehemu alipoanza kutetemeka kwa madai kuwa anajisikia baridi kali sana. Alisema kutokana na marehemu kulalamikia baridi aliamua kumnunulia chai ya moto ili anywe na kupunguza baridi ambapo baada ya kufanya hivyo marehemu alikata roho muda mfupi baada ya kumaliza kunywa chai aliyokuwa amepelekewa huku akiwa amekaa ndani ya chumba cha mahakama hiyo. Kutokana na tukio hilo askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo waliuchukua mwili wa marehemu na kuukimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana kwa ajili ya vipimo lakini hata hivyo mwili ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi ingawa ripoti ya kifo chake haikutolewa mapema. Wakati huo huo hukumu ya kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe na pia mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya hiyo, John Mwankenja inayowakabili Hakimu Mwakalinga na wenzie watatu huenda ikatolewa kesho(Oktoba 29). Uhakika wa kufika kwa ukomo wa shitaka hilo unatokana na mahakama kuu kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi kwa upande wa washitakiwa wote. Mwishoni mwa wiki jana Jaji Karua alisema baada ya kumaliza kusikiliza pande zote mbili atatumia muda wa siku mbili kwa ajili ya kuandika hukumu ambayo anatarajiwa kuitoa jumanne hii kesi ambayo inasimamiwa na Mwanasheria wa Serikali Archiles Mulisa wakati washitakiwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.

No comments:

Post a Comment