Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, April 11, 2012

MADIWANI JIJI LA MBEYA NUSURA WATOANE ROHO KUGOMBANIA ZIARA


MADIWANI wa halmashauri ya jiji la Mbeya juzi(April 10) walijikuta wanaacha kujadili mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 na kuanza malumbano ya ziara za kamati. 

Mvutano na malumbano hayo yaliilenga zaidi kamati ya fedha iliyotajwa kufaanya ziara nyingi za kujifunza tofauti na kamati nyingine hali iliyoonekana kutowaridhisha wajumbe wa kamati hizo wakiona wenzao wananufaika zaidi.

Licha ya ziara zilizoelezwa kufanywa na kamati hiyo katika mwaka wa fedha unaomalizima katika halmashauri mbalimbali ikiwemo ya manispaa ya Morogoro bajeti ya mwaka ujao pia iliitaja kamati hiyo kuwa itasafiri kwenda Kampala kujifunza.

Diwani wa kata ya Mwansanga George Mwakabaya alisema kama lengo ni kwenda kujifunza basi ipo haja ya madiwani wote kuongozana na si kamati moja kufanya ziara kila siku huku wajumbe wa kamati nyingine wakibaki kuwatazama.

Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya madiwani wengine na kuanzisha mjadala uliodumu kwa muda mrefu ambapo miongoni mwa madiwani hao wamo Fanuel Kyanula na Lucas Mwampiki.

Mwampiki ambaye ni diwani wa kata ya Mwakibete alipendekeza pia kamati yoyote inapotoka ziara ya kujifunza inaporudi kifanyike kikao na wajumbe wa kamati hiyo waelezee ni nini walichojifunza na si kukaa kimya kama vile ziara iliwalenga wao pekee.

“Lengo ni kujifunza hivyo ni vema wanaokwenda nje wakirudi wakae nasi ili watueleze ni yapi mapya waliojifunza huko.Lakini inaonekana kama vile kamati inapokwenda ziara ni kwa lengo la kujifunza yenyewe na si madiwani wote.Sidhani kama hapa tutakuwa tunajenga” alisema.

Akijibu hoja hizo meya wa jiji la Mbeya Athanas Kapunga alisema suala la madiwani wote kuambatana katika ziara moja ni jambo lisilowezekana na ataonekana kama mtu aliyekosa utashi wa kazi atakaporuhusu hali hiyo.

Kapunga alisisitiza kuwa kamati zote zitafanya ziara za kujifunza katika mwaka wa fedha ujao hivyo hakuna budi madiwani kuanza kutoa lawama kwa kuona kamati ya fedha pekee ndiyo iliyotajwa katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao kuwa itafanya ziara.

Aliahidi pia elimu wanayoipata wajumbe wa kamati yoyote inapofanya ziara italazimika kutoa elimu ya mambo wapya waliyoyapata ili kuwawezesha madiwani wote kuwa viongozi bora na walio na uwezo wa kuiletea maendeleo halmashauri yao.

No comments:

Post a Comment