Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, April 6, 2012

Kapunga wanatamani Nyerere afufuke awarudishie ardhi waliyompa na sasa inawapa mateso


MWAKA 1985 wakazi wa kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali waliombwa na serikali kutoa eneo tepetepe lenye ukubwa wa hekta 5500.Ombi hilo lililenga serikali kupata eneo hilo kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Inasemekana Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyeomba eneo hilo baada ya kupita katita vijiji vilivyopo pembezoni mwa barabara kuu na kukuta wakazi wakiuza mahindi mabichi na mbogamboga.Kwakuwa ilikuwa msimu wa kiangazi ilimshangaza.

Baada ya kuuliza wenyeji na kuambiwa kulikuwa na bonde lililo na maji mengi aliomba apelekwe kulitembelea na ndipo akawaomba wakazi wa Kapunga watoe eneo hilo kwa serikali.

Mwenyekiti wa sasa wa kijiji hicho Ramadhan Nyoni anasema wanaKapunga walikubaliana na ombi hilo hasa baada ya kuelezwa manufaa ambayo wangenufaika kwa serikali kuliboresha eneo hilo kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji.Zao lililopendekezwa kulimwa kwenye bonde hilo ni mpunga.

Jitihada za kujenga miundombinu ndani ya shamba hilo lenye hekta 5500 zilianza kwa serikali kuomba mkopo benki ya dunia WB.Lakini benki ya dunia ilitoa sharti kwa serikali kuhakikisha pia inaboresha eneo la hekta800 kwa wakulima wadogo waliotoa ardhi yao.

“Hapo ndipo ukafikiwa uamuzi wa hekta 5500 za serikali ziwe mashariki na hekta 800 za wakulima wadogo ziwe magharibi na katikati eneo la kijiji cha Kapunga lenye hekta 1070.”anasema Nyoni na kuendelea

“Savei iliyofanyika ilihusisha maeneo yote matatu kwa maana ya eneo lililo na jumla ya hekta 7370.Na katika mambo tuliyokuwa tumeahidiwa ni pamoja na serikali kukijenga kijiji chetu na kuwa cha mfano”

“Serikali katika kujenga mradi kwenye eneo lake kupitia shirika la Nafco haikumaliza wote.Hekta 500 ndizo ziliandaliwa kwaajili ya kilimo.500 zilitumika kwa ujenzi wa makazi ya Nafco,kiwanda na karakana na 2000 zikaachwa”

Baadaye Nafco ilishindwa kuliendesha shamba hilo na hatimaye serikali ikaamua kuliuza kwa mwekezaji.Matangazo ya kuuza shamba hilo yalionesha hekta 5500.

Baadaye serikali ilimpata mwekezaji na kumkabidhi shamba hilo.Kinyume na matangazo ya kumtafuta mwekezaji mkataba uliongiwa kati ya serikali na kampuni ya Expot Trading Limited unaonesha jummla ya hekta 7370.

Mkataba huo ulisainiwa agosti 17 mwaka 2006.Katika mkataba huo,inaonekana serikali iliwakilishwa na  mhandisi mkazi wa wizara ya Kilimo,Chakula na Ushirika Rosemary Tesha na kampuni ya Expot Trading Limited ikawakilishwa na Sunil Kumar kutia sahihi.

“Maswali tunayojiuliza wana Kapunga ni kwamba kama serikali ilituomba hekta 5500 za ardhi,tukaipa hekta hizo na matangazo ya kutafuta mwekezaji yakamaanisha hekta hizo huo mkataba ulioingiwa kati ya serikali na mwekezaji unaoonesha hekta 7370 unatoka wapi?”

“Ina maana serikali iliamua kuuza mpaka ardhi ya wananchi walioikaribisha na kuipa eneo.Hili limekuwa mgogoro wa muda mrefu kati yetu na mwekezaji kwakuwa madai yake anasimamia mkataba hivyuo uwepo wetu sisi na shamba letu la wakulima wadogo hautambui”

Mwenyekiti huyo wa sasa wa kijiji cha Kapunga anasema hivi sasa wakazi wa kijiji hicho wanajuta kwa kukubali ombi la mwalimu Nyerere la kumpa ardhi.Anasema badala ya matarajio waliyokuwa nayo wakati huo sasa wanavuna mateso na adhabu ambazo kama wasingetoa ardhi yao wangeendelea kuishi maisha ya furaha siku zote za maisha yao.

“Wakati tunaombwa shamba tuliahidiwa mambo mengi sana yaliyotuvutia.Tuliambiwa kijiji chetu kitakuwa cha mfano maana tungejengewa shule ya kisasa,kuletewa umeme na pia watoto wetu wangepata ajira kutoka katika shamba tulilotoa”

“Wakati wa Nafco tulianza kuona mwelekeo wa kutekelezwa kwa ahadi tulizopewa.Maana tuliletewa maji kijijini kwetu na tukawa tunayatumia kwa matumizi yote.Badaa ya kuingia mwekezaji alikata huduma hiyo na kutoa sababu nyingi”

“Ndoto ya kuwa na kijiji cha mfano iliondoka mara tu baada ya mwekezaji kuuziwa shamba.Hapo usemi wa baadhi ya viongozi akiwemo Juma Ngasongwa na mwenzake Joseph Mungai waliosema mkae mkao wa kula walipokuwa wanamkabidhi shamba mwekezaji tukaona ulimaanisha make mkao wa kufa.Maana badala ya kutujengea shule ya kisasa alithubutu hata kuleta kijiko kikavunja tofali za tanuli mbili tulizokuwa tumechoma tukilenga kujenga shule yetu wenyewe.”  

Baada ya kuvunja tanuli hizo mwekezaji huyo alizigeukia baadhi ya nyumba za wakazi na kuzichoma kisha akajenga uwanja wa ndege kwenye eneo hilo.Anasema alianza kwa kuweka mabango kwenye makazi ya kaya 18 kabla ya kuzichoma moto na wakazi hao wakalazimika kuishi chini ya miti.Badaye aling’oa madaraja na kukataza wakijiji kukatisha ndani ya eneo laki wanapokwenda mashambani mwao.

Anasema badala ya ushirikiano kati ya watumishi wa Nafco na wakazi kijijini hapo ikaonekana sasa viendo vya unyanyasaji,udhalilishaji na kukomoana.Vitendo hivyo ni pamoja na mifugo kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi 20000 kila mmoja walipokutwa ndani ya eneo la mwekezaji.Na wafugaji awlipoomba stakabadhi ya malipo hayo wakapewa ya Nafco na si kampuni ya sasa.

Nyoni anafafanua kuwa matukio ya mwekezaji huyo yapo mengi yanayowanyiam raha wakazi hao lakini tatizo ni kutofahamika kwa mpaka halisi.Lipo pia tukio la Julai 10,2011 ambapo mfanyakazi wa kampuni hiyo alimgonga kwa gari mfugaji Mwiguru Nguru na kumchana msamba kabla ya kumpiga ng’ombe mmoja risasi.

Mzee Willium Joram Kasekwa (72) ni miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho walioshiriki mchakato wa kuikabidhi serikali eneo la shamba la Kapunga.Anaikumbuka sana siku alipokuja mwalimu Nyerere kuja kutia baraka katika shamba hilo.

“Akimaanisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi alizindua shamba la wakulima wadogo kwa kupanda miche kadhaa ya mpunga katika shamba langu.Ulikuwa mwaka 1966 alipokuja na aliongozana na mkewe mama Maria pamoja na mwanamke mwingine aliitwa Bibi Titi”

Wazee wengine Zebrone Gaone Mbila na Elbaut Mwinuka pia wanakumbuka busara za Nyerere alizozionesha na kuwahakikisha maisha bora kwa kutoa kwao shamba kwa serikali.

Lakini wanasema wema wao umewasababishia sasa familia zao kuishi kama mkimbizini.Baada matukio ya mwekezaji katika shamba hilo hayaishi na kila kukicha anasisitiza kuwa kijiji cha Kapunga pamoja na mashamba ya wakulima wadogo ni eneo lake hivyo wakazi wanapaswa kuondoka.

Jitihada mbalimbali zimefanywa na wakazi wa kijiji hicho lakini zimekuwa zikigonga mwamba.Moja ya jitihada hizo ni pamoja na barua ya Februari 5 mwaka 2007 waliyomwandikia rais Jakaya Kikwete kuomba awasaidia kutatua mgogoro wa mpaka kati ya kijiji na mwekezaji lakini haikujibiwa.

Wanasema maendeleo katika kijiji hicho sasa yamekwama tangu mwaka 2006 kwakuwa wapo mguu nje mguu ndani.Wanailalamikia sera ya ubinafsishaji wakisema imeleta mateso makubwa kwao na kutamani Mwalimu Nyerere kurudi duniani ili awarejeshee ardhi yao.

Uongozi wa wilaya ya Mbarali kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya unakiri kuwa mgogoro wa kimpaka kati ya kijiji cha Kapunga na mwekezaji ni pasua kichwa unakwamisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment