Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, April 18, 2012

CHUO CHAJIVUNIA WAHITIMU KUPATA AJIRA

ASILIMIA 50 ya wanafunzi 175 waliohitimu mafunzo ya Stadi za Ujasiriamali katika Utengenezaji Nguo mwaka jana kwenye chuo cha Ujuzi na Teknolojia kilichopo wilayani Kyela wamepata ajira kwenye viwanda mbalimbali vya nguo nchini.

Mkuu wa chuo hicho dokta Leonard Mwaikambo aliyasema hayo katika mahafali ya kwanza ya wahitimu wa chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo na kubainisha kuwa wapo pia wahitimu walioajiriwa na chuo katika nafasi za ualimu.

Dokta Mwaikambo alivitaja baadhi ya viwanda vilivyotoa ajira hizo kuwa ni pamoja na A to Z cha jijini Arusha kilichoajiri wahitimu 36,Mzava Fabric  and Production  cha mkoani Morogoro kilichotoa ajira saba na 21st Century cha Morogoro pia kinatarajia kuajiri zaidi ya wahitimu 10 kuanzia sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha kampasi cha uhandisi na Teknolojia na mkuu wa uhandisi mitambo na viwanda chuo kikuu cha Dar es salaam Carthbert Kimambo alisema mradi unaoendeshwa na chuo hicho unalenga kuwawezesha vijana walio nguvu kazi ya taifa.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Gabriel Kipija alisema majengo na eneo linalotumiwa na chuo hicho haliendani na hadhi yake hivyo halmashauri inatarajia kutoa eneo jingine na kusaidia ujenzi wa majengo mapya.

“Ni juzi tu tulifanya kikao na kujadiliana wapi tukipeleke chuo hiki ambacho sisi tunaamini kipo kwaajili ya kutusaidia wanaKyela.Tumetenga maeneo kadhaa ambayo tutampeleka mkuu wa chuo hiki ili aende kuchagua panapofaa na baada ya hapo tutaanza taratibu za ujenzi”

Hata hivyo mwenyekiti huyo alilalamikia kushuka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kutoka 175 wa mwaka jana hadi 50 mwakaa huu hali aliyosema inadhihirisha wakazi wa wilaya hiyo kutokuwa na mwamko wa kukimbilia elimu kama ilivyo kwa wakazi wa maeneo mengine.

No comments:

Post a Comment