Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, February 25, 2012

WANAWAKE CCM WATAKIWA KUGOMBEA UONGOZI

WANAWAKE wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Mbeya wamepewa changamoto ya kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama katika uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Katibu wa jumuiya ya wanawake wana ccm mkoani Mbeya Tabu Lugwesa alitoa hamasa hiyo wakati akizungumza na wanajumuiya hiyo katika wilaya za Kyela na Rungwe alipoambatana na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mbeya dk.Mary Mwanjelwa aliyekwenda kukabidhi msaada wa mashine za kutotoleshea vifaranga vya kuku.

Lugwesa alisema kwa miaka mingi wanawake ndani ya chama hicho wamekuwa hawajitokezi kuwania nafasi mbalimbali hali inayotokana na kutojiamioni kuwa wanao uwezo wa kuongoza na kukipa mwelekeo mzuri chama chao kama ilivyo kwa wanaume.

Aliwataka wanawake hao kubadilika kwa kuhakikisha wanachukua fomu na kugombea nafasi katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho ili wao pia waweze kutoa mchango wao kwa kukiongoza chama chao.

Alisisitiza kwa wale watakaogombea kutopakana matope kwakuwa inafaa ifike muda wa wao kusema inatosha wanawake kutajwa na jamii kuwa watu wasiopendana na kutakiana maendeleo.

“Tutasemwa wanawake hatupendani mpaka lini?Tubadilike tuwaonyeshe wanaotusema kuwa tunao uwezo wa  kushirikiana hasa katika hili la uchaguzi ili tuongeze wanawake wengi viongozi ndani ya chama chetu” alisema.

Hata hivyo aliwasihi kuhakikisha wanachagua viongozi walio na uwezo wa kukiongoza chama hususani wale wanaoweza kusimama mbele za watu na kujibu mapigo ya wapinzani akisema lengo la chama ni kupata viongozi wachapa kazi ili kijipange upya.

Alikemea tabia ya baadhi ya wanachama ambao wanapita kwa wenzao na kuanza kupotosha juu ya kanuni za uchaguzi zitakazofuatwa katika uchaguzi wa chama hicho mojawapo ikiwa ni wale wanaosema madiwani hawataruhusiwa kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment