Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, February 15, 2012

MILA POTOFU CHANZO CHA KUFA WAJAWAZITO MPANDA

IMEELEZWA kuwa mila potofu na ukosefu wa elimu kwa jamii juu ya uzazi salama na wa mpango ni miongoni mwa sababu zinazochangia  ongezeko la vifo vya wajawazito wilayani Mpanda mkoani Rukwa.

Muuguzi mkuu wa wilaya ya Mpanda, Dk.  Pius Buzumalle alisema hayo jana wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa habari yaliyofanyika ofisini kwake, mjini hapa waliotaka kujua kiini cha baadhi vifo vya wajawazito wanaofikishwa katika hospita ya wilaya ya Mpanda.

Alisema kuwa bado jamii imekuwa ikiamini mila potofu zilizopitwa na wakati ambapo wajawazito wengi wamekuwa wakijifungulia kwa wakunga wa jadi ambao hawatambuliki na hawana utaalamu wa kutosha, hivyo  wamekuwa wakisababisha kutokea kwa vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

" utafiti unaonyesha kuwa Wapo wakinamama wenye tabia ya  kwenda kwa waganga wa kienyeji na kuwapatia dawa za miti shamba ambazo zimekuwa zikiwazuru wakati wa kujifungua, hivyo kuwaletea madhara makubwa ikiwamo kupoteza maisha yao na watoto" alisema Dk. Buzumalle.

Aliongeza kuwa pia kutokana ukosefu wa elimu ya uzazi salama kwa wakina mama wengi wajawazito imesababisha baadhi yao kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya na zahanati pindi wanapopata ujauzito hali ambayo imewasababishia kupata matatizo hayo.

Muuguzi mkuu huyo, ametoa maelezo hayo kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusiana na vifo vya akina mama wajawazito  wawili waliofariki katika hospitali ya wilaya ya mpanda hivi karibuni wakati wa kujifungua.

Ambapo amedai kuwa vifo vya akina mama hao vilitokana na sababu tofauti ikiwamo ya mmoja kuchelewa kufikishwa hospitalini na mwingine ambaye alifanyiwa uchunguzi baada ya kifo chake iligundulika kuwa kilitokana na kunywa dawa za miti shamba.

Dk. Buzumalle alieleza kuwa lengo la madaktari na wauguzi ni kuhakikisha kila mama mjamzito anayefikishwa katika hospitali ya wilaya ya mpanda na kwenye vituo vyote vya afya anajifungua salama na si tofauti na hivyo.

No comments:

Post a Comment