HABARI NDUGU WANAHABARI!
Kwanza napenda kutoa shukurani kwa
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sote kumaliza kampeni na uchaguzi kwa usalama na
amani bila kuibuka kwa vurugu za aina yoyote. Na hiii ilikuwa kauli mbiu yangu
amani na usalama ndo msingi wa maendeleo ya nchi na jimbo letu.
Pili natoa shukurani kwa chama cha
MapinduzI kwa kuniteua kupeperusha bendera ya chama changu katika uchaguzi mkuu
kugombea ubunge jimbo la Mbeya mjini ambao ulihitimishwa Oktoba 25.
Pia nawashukuru wanahabari kwa
msaada wao katika kuujuza umma wa Mbeya mambo yaliyokuwa yakijiri kwenye
kampeni zetu tulizokuwa tukizifanya kwenye kata zote 36, nilifanikiwa kufanya
jumla ya mikutano 56 na zaidi ndani na nje na niliweza kukutana na wananchi
wengi maeneo mbalimbali niliyofanya kampeni na kusikiliza kero zao.
Nachukua fursa hii pia kuwashukuru
wagombea wenzangu wote wa ndani ya chama wapatao 15 kwa kushirikiana nami
katika Kampeni hizo. Shukrani za pekee zimwendee Charles Mwakipesile aliyekuwa
Meneja wangu.
Pamoja na mimi kuteuliwa na chama
bado wagombea wenzangu katika chama walijitahidi kuniunga mkono na kunisapoti
kwa hali na mali wapo walioacha shughuli zao na kuzunguka nami kwenye kampeni
zote jitihada zao zimeonekana, nawashukuru sana.
Navishukuru kipekee vyombo vya
ulinzi na usalama kwa kazi kubwa, ngumu na nzuri waliyoifanya na kulifanya jiji
letu la Mbeya kuwa salama hadi leo. Nawashukuru sana.
Nilijitahidi kufanya kampeni za
kistaarabu, kwa kutumia uwezo wangu wote pamoja na matukio mbalimbali ya kejeli
yaliyokuwa yakitolewa na wapinzani wetu, nilichukulia kama ndio siasa kwani
kila mmoja alikuwa anatafuta kiti cha Ubunge wa Jiji la Mbeya kwa namna yake
lengo letu lilikuwa moja kusukuma maendeleo ya Jiji letu.
Mwenzangu wa chadema ameibuka na
kura nyingi zaidi ya wengine tuliogombea naye na kutangazwa kuwa mbunge mteule
wa jiji la Mbeya. Haya ni maamuzi ya wana Mbeya wengi zaidi ya wale waliotaka
niwe mbunge wao. Nampongeza Sugu kwa ushindi huo na pia ninamtakia kila laheri
katika muda wake wa uongozI. Pamoja na dosari zilizojitokeza kwenye uchaguzi
huu lakini nimekubaliana na matokeo, tuweke mambo ya itikadi pembeni tusimame
pamoja tuijenge Mbeya yetu.
Kwa bahati mbaya sana nimeshindwa
katika uchaguzi huu nikiwa nimekusanya takribani kura 50,000 inawezekana
wakati bado haujafika wa mimi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya, nimefarijika kwa
wale walionipa kura na hata wale ambao hawakunichagua, Nawashukuru
wananchi wote.
Najua walionichagua walinielewa,
walinikubali,walihitaji niwawakilishe. Nasema nitawawakilisha na sitowatupa.
Yale niliyoyasema yatatimia juu yao kwa namna moja ama nyingine kadri Mungu
atakavyojalia. Sitawaacha wala kuwaangusha. Nawaomba wasijione wameshindwa na
wasikate tamaa. Nipo nao pamoja. Ahadi nilizotoa wakati wa kampeni
nitazitekeleza kwa kadri ambavyo Mungu atanijaalia.
Nipo na wanajamii hapa hapa Mbeya,
shughuli zangu na biashara zangu zipo hapa Mbeya nitaendelea kuwa na wana Mbeya
kwa hali na mali tukiendelea kulijenga Jiji letu la Mbeya.
Naahidi nitaendelea kushirikiana na
wananchi wa jimbo la Mbeya kwa hali na mali nikifuatilia na kutekeleza ahadi
zilizoahidiwa na Rais mteule Dkt.John Pombe Magufuli, pamoja na kwamba
sikuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Mbeya.Kwa niaba ya walionipigia kura nitafanya
kazi.
Ndugu wanahabari nilijiwekea
vipaumbele wakati wa kampeni zangu pamoja na ahadi kwa wananchi wa jimbo la
Mbeya katika baadhi ya maeneo niliahidi mambo mbalimbali kama vile ujenzi wa
zahanati kata ya Iyunga, Igawilo, Ilemi na Nsoho. Shule kata ya Iziwa, na
zinginezo, usafiri wa daladala pembezoni, maji na umeme. Pia kutafuta waalimu
wazuri kwa ajili ya shule zetu. Bila kusahau pembejeo kwa wakati.
Nitashirikiana na wananchi katika kutekeleza ahadi zangu.
Pia zipo ahadi nilizoahidiwa na Rais
wangu mteule ambaye ni muadilifu na mchapakazi nitamkumbusha ikiwemo km 10 za
barabara Jiji la Mbeya na mengineyo ambayo nimeahidi kuyatekeleza mwenyewe kwa
wapiga kura wakati wa kampeni.
Ndugu zangu wanahabari, naamini
mlikuwa mkitafakari kukaa kwangu kimya baada ya kumalizika kwa uchaguzi huu
wengi walitegemea ningeweza kupinga matokeo, kufanya hivyo kungesababisha
kuchelewesha mahitaji ya wakazi wa jiji la Mbeya ambao wanahitaji huduma yangu
na ahadi nilizotoa kwa wengi waliojitokeza kuniunga mkono, nawaahidi
sitawaangusha.
Mwisho lakini si kwa umuhimu napenda
kuwasisitiza wakazi wa Jiji la Mbeya kuendelea kushikamana kwa ajili ya
kuliendeleza jiji letu, tuepuke vishawishi na kujiingiza katika mambo ya
uvunjifu wa amani na utulivu.
Amani ya Mbeya ikitoweka hakuna
biashara inayoweza kufanywa wala hakuna shughuli zozote za maendeleo ambazo
zinaweza kufanywa,vijana wajikite kwenye ujasiriamali watafute riziki yao
halali kwa kuwa Mbeya yenye amani na salama kwa Maendeleo yetu linawezekana.
Ahsanteni
Capt. Sambwee Shitambala (MNEC-CCM,
Mbeya)
No comments:
Post a Comment