Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, November 16, 2015

Priscar,Filamu inayozidi kulitambulisha jiji la Mbeya katika sanaa.


 Na Joachim Nyambo.
AMA hakika tasnia ya filamu mkoani Mbeya inaonesha kuzidi kushika kasi na kulifanya jiji hilo kuwa miongoni mwa miji mikubwa nchini yenye wasanii wanaofanya kazi zinazohitaji pongezi.Nalizungumza hili baada ya kuona jitihada zinazofanywa na wacheza filamu wa mkoani hapa.Kazi wanazofanya kwa sasa ni tofauti kabisa na walizofanya miaka kadhaa iliyopita huko nyuma.

Napata jeuri ya kuyasema haya kwakuwa na ushahidi wa filamu ambayo hivi sasa imelitenga soko la filamu nchini kote.Hii ni filamu ijulikanayo kwa jila la Priscar.Filamu hii imeandaliwa na kuchezwa na wasanii wa Mbeya kupitia kampuni ya Orange filim Entertainment yenye maskani yake jijini Mbeya.

Washiriki wakuu katika filamu ya Priscar ni pamoja na Mwanadada Jackline Charles aliyebeba jina la filamu.Msanii huyu ambaye mwaka jana alitamba vizuri katika filamu ya Vanilla iliyochezwa pia na wasanini wakazi wa jijini Mbeya ameonesha kuiva zaidi kwenye filamu ya Priscar.

Washiriki wengine ni Andrew Mlelema(Hansi),Ally Abdul-(Daniel) na Aisha Omary(Doreen).Hawa kwa pamoja wamefanya kazi kubwa ya kuifanya filmu ya Priscar kusheheni kila aina ya burudani kwa wapenzi wa filamu na pia mafunzo kulingana na maisha ya mwanadamu.

Priscar ni filamu ya kwanza kutengenezwa na kampuni ya Orange filim Entertainment.Stori yake iliandaliwa na Andrew Mlelema ambaye pia ni miongoni mwa walioshiriki kucheza na skripti ikaandaliwa na Takesh Edward.

Pamoja na burudani iliyopo ndani ya filamu hii,yapo mafundisho mbalimbali unayoweza kuyapata baada ya kuitazama.Fundisho la kwanza ni pale inapoonekana haraka na tama vinavyoweza kumharibia mwanadamu mfumo halali wa maisha na kujikuta akiingia katika maisha mengine yasiyo endelevu kwake japo kwa muda mfupi yanaweza kuonekana ni mazuri.

Mfano mzuri wa fundisho hili ni pale ambapo Priscar baada ya kumuomba kwa siku kadhaa mchumba wake Daniel pesa kwaajili ya kulipia matibabu ya shangazi yake aliyelazwa hospitalini.Kwakuwa ilikuwa katikati ya mwezi Daniel hakuweza kupata fedha kwa wakati na ikamlazimu kuendelea kumuomba mchumba wake kuvuta subira kwakuwa anajaribu kila sehemu kukopa inashindikana.

Hapo Priscar alifikia hatua ya kuamini mchumba wake hataki kumsaidia na akaamua kutafuta njia nyingine kupata fedha kwaajili ya kulipia matibabu ya shangazi.Hapo ndipo alipojikuta anaangukia katika mikono ya kijana Hansi mmiliki wa kampuni ya kutoa mikopo ya fedha.Prisca baada ya kusaidiwa fedha na milionea Hansi akajikuta anajitumbukiza katika penzi na tajiri huyo na kumwacha Daniel akihaha asijue la kufanya.

Lakini maisha ya kuponda raha na starehe kati ya Priscar na mchumba mpya Hansi yakafikia tamati baada ya mrembo huyu kubaini kuwa kijana huyo ana mchumba wa siku nyingi na haina ubishi kuwa anampenda zaidi yake na wako mbioni kuoana.Hapo ndipo Priscar akajikuta njia panda kwani hata alipomkumbuka mchumba wa awali,akakuta tayari Daniel alikwishapata mchumba mwingine na ni mjamzito.

Fundisho la pili ni namna binadamu wasivyopaswa kuishi kwa kudharau watu wasiowajua.Hili linajitokeza katika kipande ambacho kinamuonesha Mrembo Priscar akiwa kituo cha mabasi kusubili daladala,mara anapita kijana Hansi na kumbembeleza kumpa rifti.Kwa kujiona mrembo na mwenye hadhi kuliko anayembembeleza Priscar alionesha dharau hapa pale alipokubali kupanda kwenye gari mpaka aliposhushwa.

Kwa bahati mbaya safari ya Priscar ilikuwa ni kwenda kufuatilia maombi ya mkopo aliyokuwa amepeleka katika kampuni moja.Kwakuwa fomu zake za maombi ya mkopo hazikukamilika alishauriwa na watoa huduma kwenye ofisi hizo aende kuonana na mkurugenzi wa kampuni ili aone uwezekano wa kumsaidia.

Hamadi!bosi ndiye Yule kijana aliyeoneshewa dharau njia nzima alipojitolea kumpa rifti mrembo Priscar.Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Priscar kujutia dharau zake kwa mtu asiyemjua.

Lipo fundisho la tatu.Hili ni wanadamu kutodharau watu wanaofanya shughuli flani na kuwaona makahaba au watu wanaojiuza na wasioweza kuishi maisha yenye mfumo unaostahili hususani wahudumu kwenye baa.Hili linajitokeza pale kijana Daniel anapoonesha kukerwa na ushauri wa rafiki yake Jackob anayemshauri kwakuwa Priscar amemsaliti basi asipate shida achukue japo mhudumu mmoja pale baa walipokaa ili akamliwaze.

Hapo ndipo Daniel anaonesha kuwa anachokiamini yeye ni kila mhudumu wa baa ni kahaba.Anasema hawezi kuwa na mwanamke anayefanyakazi baa.Lakini baada ya kufukuzwa kazi kutokana na kupoteza majalada aliyoagizwa na bosi wake,Daniel anajikuta anaangukia mikononi mwa mhudumu aliyemwokoa siku alipolewa zaidi pombe na kuamua kumlaza katika chumba cha wahudumu wa baa.

Kwa kuyumba kimaisha Daniel akalazimika kuishi na mhudumu huyo na hatimaye kumpa ujauzito.Mhudumu huyu anaonesha hali ya kumjali Daniel na kumfariji kila wakati hasa pale anaporudi akiwa mchovu kutokana na shughuli ya kuzurula mjini kusaka ajira mpya.Anaendelea kumjali mpaka siku aliporejeshwa kazi baada ya majalada yaliyopotea kupatikana.Hapo Daniel akaamini kuwa amepata mchumba mwema zaidi ya Priscar japo mchumba wa sasa walikutana baa.

Waandaaji wanasema zipo changamoto nyingi zilizoukabili mchakato mzima wa uandaaji wa filamu ya Priscar iliyorekodiwa na kampuni ya S Media ya mkoani Morogoro.Moja ya changamoto kubwa ilikuwa ni kupotea kwa kazi ya kwanza baada ya kutoka location.

“Kazi ilipotea kwenye Extenal disc.Ilitupa wakati mgumu kwani ilitubidi kujipanga kuanza kazi upya.Ilikuwa Februari mwaka jana ambapo kazi ilipotea katika mazingira ya kutatanisha.Lakini tulijipa moyo tukarudi Locationi kufanya upya” anasema mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Orange filim Entertainment Andrew Mlemela.

“Tumetumia takribani miaka miwili mpaka kuja kuikamilisha filamu na kuiingiza sokoni.Kwakuwa ni filamu yetu ya kwanza hatukuona haja ya kutumia wasanii walio na majina makubwa.Tulitaka tufanye wenyewe ili tujipime na pia wadau watupime.Ndiyo sababu tulishirikisha pia wadu kwa kila hatu tuliyofikia”.

Anasema wadau wengi wa filamu waliyoitazama wanaonesha kuridhishwa nayo.Huo ni mwanzo mzuri kwa kampuni kujipanga kwa kazi nyingine nyingi zaidi na zenye ubora unaohitajika.Japo wanatishwa na utitiri wa filamu sokoni.

Anasema sanaa ya filamu kwa mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini inakwamishwa na baadhi ya waandaaji wasiozingatia umakini katika utekelezaji wa majukumu yao.

No comments:

Post a Comment