ASILIMIA
kubwa ya kilimo kinachoendeshwa mkoani Rukwa nchini Tanzania ni kile cha kizamani na
kisichokuwa na tija kubwa katika kumwinua mkulima na mfugaji kiuchumi.Wakulima
wengi mkoani hapa bado wanalima kilimo cha kutegemea mazao ya muda mrefu
hususani mahindi,maharage,ulezi,mtama na karanga.
Kilimo cha
mazao haya kimekuwa na changamoto nyingine kwakuwa hutumia mizezi mingi tangu
kupandwa kwa zao husika hadi kukomaa na kufikia mavuno.Kwa zao kama mahindi
mkulima hulazimika kutumia kati ya miezi mine mpaka mitano kuvuna.Kipindi hiki
ni kirefu mna na huathiri mapato ya mkulima.
Ufugaji pia
unaofanyika mkoani hapa si ule wa kisasa.Wafugaji wengi wanafuga
ng’ombe,mbuzi,kuku,bata na nguruwe kwa kutumia mazoea.Hawafugi kibiashara hatua
ambayo ingewainua haraka kiuchumi iwapo wangebadilishwa.
Kilimo hiki
kisicho na tija ndicho kilipelekea wadau wachache kukaa na kuibuka na wazo la
kuanzisha Asasi ya Maendeleo ya Kilimo na Wafugaji(Amawawa).Mwaka 2009 ndipo
kilipoundwa chombo hiki.
Lengo la
kuanzishwa kwa Amawawa ni kuwawezesha wakulima na wafugaji wadogo kuwa na nguvu
ya pamoja.Waweze kuwa na sauti ya pamoja ya kutetea na kutatua changamoto
zinazowakabili ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikwamisha jitihada zao za
kupiga hatua kimaendeleo kupitia shughuli zao za kiuchumi.
Kutokana na
unyeti wa jambo husika,kupitia asasi hii waanzilishi wake wakaona jambo la
kwanza na muhimu kufanikisha lengo la kuanzisha kwake ni kuwa na kituo cha
kutoa elimu ya kilimo na ufugaji wa kisasa kwa vitendo na si kuishia kuzungumza
kama wanavyofanya wadau wengi wa kilimo.Wengi wamekuwa wakiishia kupiga porojo
majukwaani na utekelezaji wao kuishia kwenye makabrasha na vipeperushi.
Katibu wa
Amawawa Petro Milambo anasema walengwa wakuu wa kituo hiki ni vijana.Hao ndio
wanaopaswa kunufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa kituo hicho kilichopo nje
kidogo ya manispaa ya Sumbawanga.Kwa kupata mafunzo ya kilimo na ufugaji wa
kisasa wataweza kuona umuhimu wa kujiajiri kupitia shughuli hizo.
Milambo
anasema vijana wengi wamekuwa wakivikimbia vijiji vyao na kwenda mijini
wakiamini huko kuna unafuu mkubwa wa upatikanaji wa ajira.Lakini matokeo yake
huko mijini wemekuwa wakijikuta wanaingia kwenye makundi ya vijana yenye
kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu.
“Vijana
wengi wamekuwa na imani potofu kuwa mijini pekee ndiko wanakoweza kupata mafanikio
ya haraka.Lakini hii yote ni kutokana na kilimo kuonekana hakiwaletei tija
vijijini kwao.Huko mijini matokeo yake imekuwa ni kujiunga na vikundi
vinavofanya mambo maovu kama wizi na matumizi ya dawa za kulevya”
“Lakini
wanakimbia kilimo kwakuwa hawaoni kama kinaweza kuwaajiri.Tunapowapa elimu tunawahamasisha
kulima na kufuga kwa njia za kisasa ni dhahiri wataweza kujiajiri wakiwa
vijijini kwao.Kamwe hawatatamani kwenda mijini kwakuwa tayari wamekwishaona
mifano ya wenzao waliokwenda huko na hawakupata mafanikio.Badala yake walirudi
wakiwa wameharibikiwa baadhi yao wakiwa wagongwa baada ya kuambukizwa virusi
vya ukimwi” alisema Milambo.
AMilambo
anasema kwa vijana kunufaika na ajira za kilimo na ufugaji wa kisasa wakiwa
vijijini kwao kunawezesha hata wenzao waliokimbia kurudi na kuungana nao ili
kwa pamoja waweze kuunganisha nguvu kwenye shughuli hizo.Kwa sasa vijana
wengi wanakimbilia mjini na kuiacha sekta ya kilimo bila nguvu kazi kwani wazee
wao ndio wanaobaki wakijihusisha na shughuli hiyo.
“Kwa hapa
kituoni vijana ambao wanakuwa wakija kupata mafunzo hapa kwa vitendo wanaweza
kujifunza mambo mbalimbali.Wakiwa hapa wanajifunza kilimo cha matunda na mboga
mboga kama unavyojua mkoa wa Rukwa hamasa ya kilimo cha matunda bado ni ndogo
ikilinganishwa na mikoa jirani kama Mbeya.Lakini kilimo cha matunda kina
manufaa makubwa mno.Tukidhamiria kwa dhati kujikita katika kilimo hiki vijana
wanaweza kujikuta wanapata mafanikio kwa muda mfupi sana na umaskini
unaowasumbua kwa sasa ukabaki katika historia.Matunda kama mapera na matunda
jiwe yanastawi sana mkoani hapa lakini hayalimwi kwa malengo”
“Lakini pia
kilimo cha mboga mboga kinachofanyika mkoani hapa ni cha kizamani.Wakulima
hawalimi kwa matarajio makubwa na kuona kama kinaweza kuwasaidia kunyanyuka
kimaendeleo na jamii ikabaki inashangaa.Tunatambua kuna tatizo la miundombinu
hasa ya kilimo cha umwagiliaji lakini tunaamini serikali nayo ina wajibu wa
kujipanga kuwasaidia vijana hasa inapoona wadau wengine tunatekeleza kwa upande
wetu” anasema
Katibu huyo
wa Amawawa anasema katika msimu wa 2014-2015 Kitruo hicho kilianza kutekeleza
adhama ya kilimo cha matunda.Anasema anasema shamba darasa lenye ukubwa wa
ekari moja lililimwa na kufanikiwa kuvuna kiasi cha tani 2.5 za matunda aina ya
tikiti maji.
“Tikitimaji
ni kilimo kinachotumia miezi mitatu tu.Hivyo tulikuwa na misimu kadhaa ya
kilimo hiki licha ya kuwa katika msimu huo tulikumbwa na changamoto ya uhaba wa
maji kwakuwa kutokana na mvua kuwa kidogo msimu wa kiangazi ulikuwa mkubwa na
hivyo kukawa na ukame”
Milambo
anasema kupitia shamba darasa la kilimo cha tikiti chuoni hapo wapo wakulima
hususani vijana waliopata fursa ya kujifunza kilimo hicho waliporudi makwao waliweza kutumia teknolojia
hiyo na wanaendelea kunufaika nayo.
“Unaweza
usiamini lakini wanaojifanyia kazi elimu waliyoipata hapa wananufaika kwa kiasi
kikubwa licha ya uwepo wa changamoto ya upungufu wa maji.Mpaka leo wapo ambao
uchumi wao umeonesha kukua kwani wameweza kununua mifugo kama Ngombe,Mbuzi na
wapo pia waliojenga nyumba za kisasa na kuezeka bati badala ya nyasi kama
ilivyokuwa awali.”
“Takribani
vijana 35 kutoka manispaa ya Sumbawanga na pia Sumbawanga vijijini walifika
kituoni hapa kupata elimu ya kilimo cha matikiti maji kwa kipindi hicho.Kilimno
hiki kimeonekana kuwa na manufaa kwao kwakuwa soko lake si la kusuasua kama
ilivyo kwa mazao kama mahindi.Matikiti yanapokomaa kazi yako ni kutafuta mteja
tena wa jumla na akija shambani unavuna na kukabidhiana naye papo hapo”
Amawawa pia
inalenga kufundisha vijana ufugaji wa kisasa wa Sungura,nguruwe,kuku,mbuzi na
ndezi.Uongozi wa kituo unaamini hiyo yote ni miradi yenye kuweza kumwingizia
kipato kijana mmoja mmoja au wakiwa katika kikundi.Kijana ama kikundi kikilima
mchicha wakati huo huo kikawa na ng’ombe wa maziwa au mbuzi na pia mifugo
mingine midogomidogo hatoweza kukosa fedha.
Ufugaji wa
nyuki na samaki ni mafunzo mengine yanayotolewa kituoni hapo kwa vijana.Ufugaji
huu unawezesha kwa kiasi kikubwa utunzaji wa mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa
yameharibiwa na kilimo cha mfumo wa kizamani.Miti na misitu mingi imefyekwa ili
kupata mashamba ya kulima.Lakini pia upo uchomaji moto wa mapori kwaajili ya
baadhi ya watu kutafuta wanyama wadogo wa porini kwaajili ya kitoweo.
Kwa kufuga
samaki na nyuki kwa njia za kisasa vitoweo vitapatikana kwa urahisi na vijana
watajiingizia vipato kwa kuuza samaki,asali na pi nta kutokana na mazao hayo
kuwa na soko zuri.Hii pia itasaidia kutunzwa kwa mazingira kwa kutochomwa moto
misitu na kufyekwa hovyo miti.
“Yapo mambo
mengi mazuri ambayo vijana wakiwa hapa watajifunza.Na tunataka wakitoka hapa
waone kuwa awali walikuwa wakicheza mijiji na waweze kujipanga kuanza maisha
upya wakitaraji neema kwa wakati mfupi.Lini hatutoishia kutoa elimu kwa vijana
watakaofika kituoni hapa pekee.Tunataka pia wakulima wawe wanapanga ziara za
kimafunzo na kuja hapa kujifunza wakaondoka”
Mwenyekiti
wa Amawawa Oscar Msangi anasema pamoja na mipango hiyo mizuri ya
kituo,changamoto zinaonekana kuwa nyingi zaidi ya uwezo wa kuzikabili.Ukosefu
wa rasirimali fedha umekuwa kikazo kikubwa.
“Shughuli
zetu zote zinahitaji fedha.Tulitegemea zaidi nguvu ya wafadhili mbalimbali ili
kumudu gharama za uendeshaji wa kituo hiki.Tunahitaji vijana wanaokuja
kujifunza wakae hapa kituoni na si watoke mbali.Tumejitahidi kujenga majengo
kwaajili ya mabweni kwa kuchanga fedha zetu za mifukoni.”
“Tunao
uhitaji wa samani kama vitanda,meza na viti.Tunahitaji pia magodoro kwaajili ya
kulalia vijana wawapo kituoni hapa wakijifunza.Tatizo fedha hatuna.Tunajaribu
kushirikisha wadau wengine bado hatujakata tama tunaamini siku moja
tutafanikisha lengo la kuinua uchumi wa mkulima ” anasisitiza Msangi.
Mwenyekiti
huyo anasema changamoto nyingine ni hali ya ukame.Hii imeleta ugumu katika
suala zima la ufugaji wa samaki katika mabwawa.Anasema kutokana na ukame sehemu
kubwa ya mabwawa kituoni hapo yamekauka na kusababisha samaki wengi kufa.Hasara
inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi 5000,000 za kitanzania imepatikana
kutokana na kukauka kwa mabwawa hayo.
Kwa mujibu
wa mamlaka ya hali ya hewa nchini,msimu wa kilimo mwa mwaka 2015/2016
unatarajiwa kuwa na mvua nyingi.Kwa Amawawa hii ni neema inayotarajiwa.Kituo
hiki kinaamini kuwa kwa uwepo wa mvua nyingi msimu huu mabwawa yatajaa maji na
ufugaji wa samaki utarejea katika hali ya kawaida.Wanaamini pia vyanzo vingi
vya maji hususani mbuga zitakuwa na maji ya kutosha kwaajili ya kilimo cha
mboga mboga na matunda.Hii itawezesha kituo kuwa na mashamba darasa endelevu na
pia wakulima wanapojifunza kwenda kufanya vizuri kwenye mashamba yao.
“Jana tu
hapa Sumbawanga imenyesha mvua kubwa sana.Kwetu sisi tunapata matumaini kwakuwa
tunahitaji maji mengi kufanya shughuli kituoni kwetu na pia kwenye mashamba ya
wakulima tunaowafundisha.Pasipo maji ya kutosha hatuwezi kufanikiwa kitu.Ndiyo
sababu tunahimiza pia suala la utunzaji wa mazingira.” Anasema Msangi.
Tunahitaji
pia fedha kwaajili ya kufanikisha mradi wa maji ya mserereko.Yapo umbali wa takribani
mita 600 kutoka kituoni hapa.Kituo kinataraji kutega na kuyavuta kwaajili ya
matumizi ya kilimo.
Msangi
anasema changamoto ya rasilimali fedha pia inatokana na kupungua kwa asilimia
kubwa kwa waanzilishi wa asasi hii.Kati ya waasisi 30 ni 15 pekee waliosalia
hivyo kusababisha nguvu ya utafutaji ufadhili kupungua Anasema wengi wa waasisi
wamekimbia majukumu ya kuchangishwa kila kunapokucha.
No comments:
Post a Comment