Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, November 13, 2015

WATATU WAFA MBEYA KATIKA MATUKIO TOFAUTI

WATU watatu wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke mmoja aliyekutwa akiwa ameuawa na watu wasio fahamika.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Ahmed Msangi jana alisema mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Lucy Yesaya(22) aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na usoni.

Alisema mwili wa Lucy ulikutwa ukiwa na majeraha mnamo Novemba 11 saa 12:30 asubuhi katika kijiji cha Izumbwe Sokoni,kata ya Songwe wilayani Mbeya.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo sambamba na kuwasaka wauaji ambapo chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika.

Katika tukio la pili Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba Promis Dank mkazi wa Bwawani wilayani Chunya alipefariki dunia alipokuwa njiani kupelekwa hospitali baada ya kutumbukia kisimani.

Kamanda Msangi alisema mtoto huyo alitumbukia kwenye kisima chenye maji mnamo novemba 11 saa 12:00 asubuhi katika kitongoji cha Railway mtaa na kata ya Bwawani.

“Inadaiwa kuwa mtoto huyo baada ya kutumbukia kwenye kisima ambacho kilikuwa wazi aliokolewa akiwa hai lakini alifariki dunia akiwa njiani kuelekea hospitali teule ya Mwambani iliyopo Mkwajuni kwaajili ya matibabu” alisema Kamanda Msangi.

Akizungumzia tukio la tatu,kamanda huyo alisema mpanda baiskeli wa kiume ambaye hakufahamika jina lake anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 28 alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajiri  T 838 AAC aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikiendeshwa na Deo Mbilinyi.

Alisema ajali hiyo ilitokea novemba 11 saa 10:40 jioni maeneo ya Uyole jijini Mbeya na chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari ambapo dereva alikimbia mara baada ya tukio na anatafutwa na polisi.

No comments:

Post a Comment