ALIYEKUWA mgombea wa ubunge Mbeya
mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Sambwee Shitambala amempongeza mshindi
wa nafasi hiyo kupitia Chadema Joseph Mbilinyi(Sugu) na kubainisha kuwa hana
mpango wa kwenda mahakamani kupinga matokeo.
Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25
mwaka huu Shitambala alishika nafasi ya pili akipata kura 46,894 huku Mbilinyi
akimshinda kwa kupata jumla ya kura 97,675.
Katika tamko lake alilolitoa kwa
vyombo vya habari leo(Nov 4),Shitambala amesema hana mpango wa kwenda
mahakamani kupinga matokeo hayo kwakuwa kufanya kutachelewesha mpango wake wa kuwatumikia
wananchi nje ya nafasi ya ubunge.
Amesema pamoja na kukosa nafasi
hiyo,hatosita kutekeleza ahadi zote alizoziahidi kwa wakazi wa kata zote za
jijini hapa lengo likiwa ni kuondoa adha zinazoikabili jamii.
Amezitaja baadhi ya ahadi
atakazozitekeleza japo hakuchaguliwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika
kata za Iyunga, Igawilo, Ilemi na Nsoho, Shule katika kata ya Iziwa, na nyinginezo,
usafiri wa daladala pembezoni mwa mji, maji na umeme na pia kutafuta waalimu
wazuri kwa ajili ya shule za jijini hapa.
Amesema pia hatosita kumkumbusha
rais mteule Dk.John Pombe Magufuli juu ya ahadi alizotoa kwa wakazi wa jiji la
Mbeya ikiwemo ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 10 kwa kiwango cha
lami.
No comments:
Post a Comment