Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, November 20, 2015

NILIYOYAONA KIJIJINI IGANGWE,CHUNYA.

Na Joachim Nyambo. 
WASWAHILI husema tembea uyaone!Huyasema haya wakimaanisha unapotembea nje ya mazingira yako ya siku zote utayaona mapya zaidi ya yale uyaonayo siku zote.Utayaona na kuyajua hata usiyowahi kufikiri kuwa yapo katika dunia hii.

Hivi karibuni nimeungana na wahenga kutaka name niyajue yaliyopo katika kijiji cha Igangwe kilichopo katika kata ya Mtanila wilayani Chunya mkoani Mbeya.Hiki ni kijiji kilichotokana na oparesheni maalumu zilizofanyika miaka ya 1970 ya kuvunja vijiji vidogo vidogo na kuunda vijiji vikubwa.Kutoka jijini Mbeya mpaka kilipo kijiji hiki unatembea takribani kilomita 150 kwa mwendo wa gari.

Nikiwa kijijini hapa mahali ambapo ndipo yalipo makao makuu ya kata ya Mtanila nilipata wasaa wa kutembelea vitu mbalimbali viki vikijikita kwenye masuala ya asili ya eneo na pia wakazi.Wakazi wa kijiji hiki wengi wao ni wa kabila la Wanyekyusa na si Wabungu kama ilivyo kwa maeneo mengi ya wilaya ya Chunya.Lakini wengi wa wakazi hao walihamia kijijini hapa kivutio kikubwa kikiwa ni shuguli ya kilimo cha Tumbaku.

Nje kidogo ya kijiji ukiachilia mbali maeneo yanayotumika kwa shughuli za kilimo,wapo wakazi ambao wao hujishughulisha na ufugaji.Hawa ni watu wa makabila ya Kisukuma,Wazanaki,Barabaigi  na wamang’ati.

Jambo la kwanza lililonishangaza kijijini hapa ni kuona uoto wa asili uliostawi.Miti mbalimbali ya asili utaiona kijini hapa na sin je ya kijiji kama ilivyo kwa vijiji vingine.Kinachofanyika hapa ni kila mwanakijiji anayejenga nyumba yake kutokana mti wowote wa asili ulio nje ya jingo lake analojenga.Atakata ule tu ulio ndani kwakuwa haiwezekani ndani ya nyumba kukawa na mti.

Hii inakifanya kijiji hiki kionekana kuwa na nyumba zilizo chini ya miti mkubwa ya asili na yenye kuleta kivuli kizuuri katika karibia nje ya kila nyumba wenyeji wakisema kila mji.Haupati shida ya kufuata kivuli mbali na nyumba uliyofikia au ulipo kwa wakati husika.

Uwepo wa uoto huu wa asili kijijini unapojumuiswa na uoto wa kupandwa wa miti ya kisasa kama ya miembe unakifanya kijiji hiki kuonekana katika hali ya kupendeza nay a ukijani kwa kipindi cha mwaka mzima.Wakati mwingine majira ya usiku ukiwa safarini waweza ukakipita kijiji hiki pasipokujua kama unapita mahali wanapoishi watu wengi.Hapa niliupenda utaratibu wa utunzaji miti ya asili.

Misitu ya kijiji hiki haiishii tu kijijini.

Nje ya kijiji kuna misitu minene zaidi.Vilima vilivyopambwa na miti ya asili ya aina mbalimbali inalindwa na kutunzwa na kila mkazi wa kijiji hiki.

Takribani kilometa tatu kutoka kijijini upande wa Magharibi kuna bonde kubwa la mto Lupa.Bonde hili lina historia ya kutisha kidogo.Wakazi wa kijiji hiki wanasema miaka ya 1970 wakati wa kuanzisha kijiji cha Igangwe walihamishwa kutoka maeneo mbalimbali walikokuwa wakiishi.Kwenye bonde hili ndiko walikokuwa wakifuata maji kwaajili ya matumizi kwenye kambi walizofikia.

Lakini wanawake waliofuata maji kwenye bonde hili ililazimu wasindikizwe kwakuwa ni eneo lililokuwa pia na wanyama wengi wakiwemo wakali kama simba.Mara kadhaa walikutana na simba waliokuwa wakijipumzisha kwenye mawe yaliyopo ng`ambo ya mbuga hiyo.Yawezekana walikuwa wakifanya mawindo kwa wanyama pia na kufuata maji katika eneo hilo.

Mkazi wa kijiji hiki Hamis Mwandura anasema historia inaonyesha kuwa ukiachilia mbali wanyama kama swala na tandala ambao hadi leo wanapatikana kwenye misitu inayozunguka bonde hilo,katika kipindi hicho,wanyama wengine kama tembo,nyati,Twiga walipatikana kwa wingi.Ilikuwa suala la kawaida pia kukutana na fisi,chui na nyoka wa aina mbalimbali na wa ukubwa tofauti.

“Ni eneo lililokuwa linatisha hata wakati sie tunakua.Haikuwa rahisi kuja pasipo kujidhatiti kiulinzi na usalama katika eneo hili”.anasema Hamisi ambaye kwa sasa mashamba yake hadi kuyafikia ni lazima avuke bonde hilo.Lakini kwa miaka hiyo wazazi wake ndiyo walikuwa wakikumbwa na mikasa ya wanyama hao.
Katika bonde hilo,chini kidogo ya eneo lenye mawe yaliyokuwa mapumziko ya simba nikakutana na bwawa moja kubwa.Bwawa hili ni maarufu kama Bwawa na Masimba.Kwa sasa maji ya bwawa hili linatumika kumwagilia vitalu vya miche ya tumbaku kabla ya kwenda kuipandikiza mashambani.Bwawa hili ni tegemeo kubwa kwa wakulima kwa nyakati za kiangazi kwa kuwa hutunza maji mengi hata pale mto Lupa unapokuwa umekausha maji yake yote.

Kwa nini bwawa hili liliitwa Bwawa la Masimba?Ni swali ambalo mtu yeyote angeweza kuuliza.Wenyeji wanasema bwawa hili kwa miaka ya zamani haikuruhusiwa kulisogelea hovyo.Ni mahala palipotumika kwa matambiko.Hata wenyeji wa eneo hilo na maeneo ya mbali waliokuwa chini ya himaya ya utawala wa Chifu Kasaka walifanya tambiko hapo walipoona kuna mambo hayakwenda sawa.

“Hata Kasaka mwenyewe alikuwa akifanyia tambiko hapa.Alikuwa kila akija hapa lazima mvua kubwa inyeshe na mto Lupa ukafurika maji” anasema mwenyeji wangu akimaanisha Chifu Kasaka na si huyu Njelu Kasaka wa sasa ambaye ni mwanasiasa.

Inasemekana katika kipindi hicho ndani ya bwawa hilo kulikuwa na samaki mkubwa kuliko wote ndani ya mto Lupa.Alikuwa aina ya Kambare mweusi.Huenda huyu ndiye aliyekuwa akiabudiwa wakati wa matambiko japo hakuna aliye na uhakika juu ya hilo.

Kambare huyu alikuwa na uwezo wa kusafiri hadi nchi kavu pale alipoamua.Safari za nchi kavu alizifanya nyakati za usiku kukiwa kumetulia.Smaki huyu alifanya safari hizi pale alipoamua kutembelea mabwawa mengine yaliyokuwa jirani wakati ambapo mto Lupa haukuwa na maji.

Inasemekana siku moja akiwa nje ya bwawa lake hilo,alivamiwa na Simba mkubwa aliyekuwa mawindoni.Inaaminika na wakazi wa eneo hili mapambano baina ya wawili hao yaani Simba na Samaki huyo mkubwa haikuwa ndogo.Walipambana kwa muda mrefu.Simba akitumia nyenzo zake yaani kucha na meno yake lakini Samaki akitumia mfupa wake mkubwa uliokuwa kwenye ubavu wake.

Fainali hiyo inaonekana iliishia kwenye ufukwe wa bwawa ambapo siku iliyofuata zipo ishara nyingi za ajabu zilijitokeza na kuwalazimu wakazi kwenda kwenye bwawa hilo kuona nini kilitokea hata kuwepo na ishara za ajabu kama hizo.Walipofika pembezoni mwa bwawa walishangazwa na kile walichokikuta.Walikuwa simba mkubwa aliyekufa na pia samaki akiwa amekufa.

Hapo ndipo bwawa hilo lilipobaddilishwa jina na kuitwa Bwawa la Masimba.Ilikuwa simanzi kubwa kwa wakazi katika miaka hiyo.Lakini pia huo ndiyo ukawa mwisho wa tumaini lao la kupata majibu ya matatizo kwa kufanya maombi kwenye tambiko kupitia bwawa hilo.Hadi sasa kila mmoja anajiendea kwenye bwawa atakavyo na kufanya atakayo japo bado ni eneo la hatari hususani inapofika wakati wa mvua nyingi kwani viboko na mamba huonekana kupenda kuishi humo na mabwawa mengine yaliyopo jirani.

Historia ya bwawa hili ilinifanya nizidi kufiatilia kila nilichokiona kwenye bonde la mto Lupa,eneo la kijiji cha Igangwe.Kaskazini mwa bwawa hili,takribani mita 150 nikaona miti mikavu iliyopangwa juu ya miamba iliyochimbiwa chini.Binafsi nilihisi ni eneo flani linalotumika aidha kwa kutega samaki au wanyama.Kwakuwa ni eneo lililo jirani na mashamba ya Tumbaku nikajua labda hutumika pia kuanikia Tumbaku!
Juu Mwenyeji wangu Hamis Mwandura akirejesha miti kwenye eneo lake katika daraja la asili.Chini nikiendelea kuhoji juu ya matumizi ya daraja hili.
Ilimbidi mwenyeji wangu acheke kidogo. “Lile ni daraja!Kama nilivyokueleza wakati wa mvua nyingi hauwezi kuvuka kirahisi huu mto.Maji huwa mengi mpaka unalifikia daraja hili lazima uvulie nguo zako kuleeeee!Karibia mita miambili”

“Kwa hiyo unapokuja huku darajani inamaana umefikia katika maji ya kina kirefu sana.Sasa hapa kwakuwa ndiyo kunapokuwa na mkondo wa maji ya kasi inatuwezesha kutumia daraja hili ambalo kimsingi nalo huwa linakuwa limezama lakini mnaiona miti kwa ndani ya maji.Utafanya hivyo wakati wa kuvuka kwenda shamba na wakati wa kurudi”

“Wakulima wanaovuka mto huu ni sisi tunaokwenda katika mashamba yaliyopo maeneo ya Kiji,Shaurimoyo na Manyungu.Lakini pia kuna watu wanaokwenda mpaka kijiji cha Ngwala wanaweza kupita huku lakini kwa kipindi kama hiki ambacho mvua hazijanyesha kwa wingi na kuujaza mto Lupa.”

“Kwa sasa abiria wanaokwenda kijiji cha Ngwala kupitia njia hii hutumia usafiri wa pikipiki ambao hulipia shilingi 15,000 kwa kila mmoja kulipia usafiri huo.Kwa nyakati za mvua nyingi ni vigumu kutumia usafiri huu kwakuwa kuvuka huu mto inakuwa vigumu” anasema Hamis.

Mwenyeji huyu anasema hatari iliyobakia katika mbuga hiyo ni uvukaji wa mto wakati wa mvua nyingi.Anasema wapo watu waliowahi kufa maji mtoni hapa.Ilikuwa katika vpindi tofauti lakini ni wakati mto huo unapokuwa umefurika kiasi cha mbuga yote kujaa maji.

Mbuga hii imebarikiwa ndugu yangu.Niko katika eneo hili hili nikaona matanuru mengi na makubwa ya tofali zilizochomwa.Mwenyeji akanambia kwa sasa wanaitumia mbuga hii kama kiwanda cha kuzalishia tofali.Anayetaka tofali mbichi atafyatua hapa na zitakuwa imara lakni akitaka zilizo imara zaidi atafyatua na kuzichoma kabla ya kujengea.Lakini shughuli zote hizi hufanyika wakati wa kiangazi.

“Kwa muda mrefu tulikuwa tukihangaika wapi tupate tofali imara.Hatukujua kama tuna utajiri kiasi hiki.Ni hivi karibuni tu alihamia jamaa mmoja akitokea huko wilayani Mbozi.Ndiye aliyetufumbua macho na ndiyo sababu unaona sasa kijiji kinapendeza kwa kujengwa nyumba bora.Hii ni kutokana na tofali za hapa mbugani” anabainisha.

Baada ya kumaliza maswali yangu nikiwa katikati ya mbuga,kwa mbaali upande wa pili nikaona kama kuna matanuri mengine,lakini yaliyoezekwa.Sikuweza kufikiri mara moja kuwa zilikuwa nyumba kwakuwa zilikwenda juu zaidi ya nyumba za kuishi.Hapo mwenyeji wangu akanambi twende tufike utajionea mwenyewe.

Nilipofika ndipo nilipobaini hayakuwa matanuri ya tofali kama yale ya mbugani,wala si nyumba za kuishi.Ni matanuri kwaajili ya kukaushia tumbaku!Wenyeji wanaita mabani.Yapo ya kisasa nay a kizamani.Ya kisasa hutumia pia majiko ya kisasa na hutumia kuni chache kuliko mabani ya kizamani.Hivyo ya kisasa ni rafiki wa mazingira zaidi ya yale ya kizamani kwakuwa miti inayokatwa kwaajili ya kuni hupungua idadi.

Pamoja na kuelekezwa namna tumbaku inavyokaushwa kwenye mabani hayo baada ya kuvunwa shambani pia nikafundishwa namna ambavyo tumbaku huhifadhiwa kabla ya kuuzwa.Lakini ndani ya mabani nikalazimika kuuliza ni kwa nini sehemu ya njia za moto zimevunjwa,tena inaonekana si kwa bahati mbaya ni makusudi.

“Hii ni kazi ya wawindaji.Wanalazimika kubomoa njia hizi kwenye mabani kwakuwa wanapowinda wakitumia mbwa sungura hukimbilia kwenye haya majiko.Kwa wakati huu ambapo hayatumiko wanyama wadogo kama sungura huyatumia kama sehemu ya makazi na maficho anapohisi adui.Sasa wawindaji wakibaini amekimbilia humu wanazima alikoingilia na ndipo wanakuja kumshambulia humu ndani kwa kubashiri kwenye hizi njia za moto”alisema mwenyeji wangu.

Niliyaona mabani mengi kwakweli.Lakini niliamua kuutembelea msitu wa asili wa kijiji pia.Huko nikakutana na matunda ya asili kama yakiwamo nyefi kama wenyeji wanavyoyaita.Yalikuwepo pia matunda pori mengine mengi,yanayoliwa na yasiyoliwa.Kwakuwa ni msimu wa mvua za mwanzo pia nikafanikiwa kuuona uyoga pori mkubwa ambayo kwa huku ni toweo kizuri sana.
Wenyeji walitupikia nasi tukafurahia kitoweo hiki kwa kula na ugali.Tukafurahia kwa pamoja mazao yam situ wa asili.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Igangwe Gulila Mwakosya anasema utunzaji endelevu wa misitu ya asili ni chachu ya mafaniko ya wakazi wa kijiji hicho,kata ya Mtanila na watanzania wote kwa ujumla.Misitu hii inayo faida kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.Ni katika msitu hu huo ambapo dawa za asili pia hupatikana.Baadhi ya magonjwa yakiwemo ya matumbo hutibiwa kwa mgonjwa kutumia dawa kutoka misitu hii.

“Ndiyo sabau hata sisi wakulima wa tumbaku tunahimizana kuyalinda mazingira yetu.Tunapokata miti kwaajili ya mashamba na pia kukaushia tumbaku tunahakikisha tunahimizana pia kupanda miti.Na kwa mashamba tunayoacha kuyalima tunayatunza ili kurejesha uoto wa awali” anasema Mwakosya ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha msingi cha wakulima wa Tumbaku katika kijiji cha Igangwe(Igangwe Amcos).

Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Mtanila Venant Lymo anasema lengo la serikali za vijiji vyote vya kata hiyo ni kuona misitu ya asili inatunza kwa manufaa endelevu.

Yapo mengine mengi niliyojifunza kijijini Igangwa,Nafasi haitoshelezi kuyaelezea.Lakini kwa hakika siku nilizokaa kijijini hapa nilifurahia sana.Nikualike nawe utembelee kijiji hiki ukajionee!

UNAWEZA PIA KUIPATA MAKALA HII KUPITIA GAZETI LA HABARILEO LA NOVEMBA 20,2015.

No comments:

Post a Comment