KATIKA kile kinachoonekana Chama cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Mbeya mjini kuzidi kupoteza mwelekeo na pia kudhihirisha kutoheshimu Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA),chama
hicho kimewatimua makada wake watatu kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa waasi
ndani ya chama.
Miongoni mwa waliovuliwa madaraka na
kisha kutimuliwa ni pamoja na mjumbe wa Kamati tendaji ya wilaya Meshack
Kapange ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema kata ya Uyole.
Wengine ni katibu wa baraza la
wanawake la wilaya(Bawacha) Agatha John na Mtunza hazina wa Chama hicho katika
kata ya Igawilo Stanley Tweve.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
kutoka chanzo cha ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa juzi
katika kikao kilichofanywa na Kamati tendaji ya wilaya na kuamuru kuwasimamisha
uanachama wafuasi wake hao watatu.
“Taarifa hizi ni za kweli kabisa na
ni maamuzi yaliyofikiwa kwenye kikao cha jana.Vipo vikao vingi vilivyofanyika
kabla ya hiki kilichotoa maamuzi ya kuwavua uanachama” alisema mmoja wa makada
wa Chadema aliyeomba kutoandikwa jina lake gazetini.
Alipohojiwa juu ya taarifa za
kuvuliwa uanachama Kapange alikiri kupokea barua kutoka wilayani ya kusitishiwa
uanachama kabisa.
Kapange alisema alipokea barua hiyo
juzi akisimamishwa uanachama kwa tuhuma za kuandaa na kuratibu mkutano wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) uliofanyika Januari 5, mwaka huu katika viwanja
vya Shule ya msingi Hasanga Uyole jijini Mbeya na kuhutubiwa na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini David Kafulila.
Kwa mujibu wa Kapange,tuhuma nyingine
anazotuhumiwa na viongozi wa Chama hicho ni kutoa nafasi fupi ya kusalimia wafuasi
walioshiriki mkutano huo kwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbeya mjini John
Mwambigija kwani alimpa dakika mbili tu kwenye mkutano huo.
Viongozi walipenda Mwambigija apewe
muda mrefu kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye mikutano yote ya Chadema
mjini hapa tofauti na viongozi wengine kutoka vyama mbalimbali vinavyounda
Ukawa ambao pia walikuwa wakipewa dakika mbili mbili kila mmoja kusalimia
wananchi.
Aliongeza kuwa sababu nyingine ni
yeye kama mratibu wa mkutano huo kukaa meza kuu sambamba na mgeni rasmi ambaye
ni Mbunge David Kafulila na kushindwa kumpisha Mwenyekiti wake John Mwambingija
kwa kuwa ndiye mwenye cheo kikubwa kuliko Mratibu wa Mkutano huo wa Ukawa.
Kapange pia hakusita kuwataja
wanachama wengine waliovuliwa uanachama na kikao cha Kamati tendaji ya Wilaya
kuwa ni Agatha John katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema(BAWACHA) Wilaya ya
Mbeya mjini na Mtunza hazina wa Chadema kata ya Igawilo, Stanley Tweve.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la
Vijana wa Chadema(Bavicha) Mbeya mjini Gidion Siame, ambaye ndiye aliyesaini
barua za kuwasimamisha uanachama viongozi hao alipoulizwa kuhusiana na taarifa
hizo alikiri na kufafanua kuwa uamuzi huo umetokana na kikao halali cha chama
ngazi ya wilaya.
Kwa mujibu wa Siame,awali kabla ya
maamuzi ya mwisho wanachama hao waliitwa katika vikao vya Chama kwa ajili ya
kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazowakabili lakini hawakutoa ushirikiano badala yake
walikuwa wakijibu kama wanavyotaka wao na hicho ndicho kilichopelekea maamuzi
hayo ya kamati.
Alifafanua kuwa hatua ya kuwatimua
uanachama makada hao imefikiwa kwa mujibu wa katiba ya Chama Ibara ya
5(3&4) inayohusu kukoma kwa uanachama na kwamba wanayo nafasi ya kukata
rufaa katika vikao vingine ngazi za juu ili kupinga adhabu waliyopewa katika
ngazi ya wilaya.
No comments:
Post a Comment