Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, November 8, 2016

MWANAHABARI GORDON KALULUNGA ALIVYOHOJIWA NA POLISI KWA SAA TANO

Na Joachim Nyambo,Mbeya.

MWANDISHI wa habari wa gazeti la Mtanzania,Gordon Kalulunga Oktoba 24 mwaka huu aliwekwa kizuizini na kuhojiwa kwa muda wa masaa manne katika kituo cha Polisi cha Mbalizi yalipo makao makuu ya Wilaya maalumu ya kipolisi Mbeya vijijini.

Mwandishi wa habari hizi aliyeambatana na Kalulunga walifika kituoni hapo majira ya Saa nane na Nusu mchana ambapo awali majira ya saa tano asubuhi,afisa mmoja wa jeshi la polisi alimpigia simu mwanahabari huyo akimtaka afike kituoni hapo kwaajili ya kuhojiwa.

Kwa mujibu wa Kalulunga wakati akipigiwa simu licha ya kuhoji kulikuwa na tatizo gani hata aitwe kituoni,afisa aliyempigia simu hakumweleza kuna nini na badala yake akamweleza ni masuala ya kiofisi yasiyoweza kuzungumzwa kupitia simu.

“Baada ya kupigiwa simu niliona kabla ya kwenda ni vema niwajulishe ndugu,jamaa na rafiki zangu wakiwemo wanahabari.Ndiyo sababu nimewaiteni ili ikiwezekana kwa walio na nafasi niongozane nao wakajue kuna nini”alisema Kalulunga baada ya kukutana na mwandishi wa habari hizi kabla ya kuelekea kituoni.

Zipo tetesi kutoka ndani ya jeshi hilo kuwa awali maafisa wawili waliagizwa kumtafuta Kalulunga popote alipo ili akamatwe na kufikishwa kituoni hapo lakini mmoja wa askari walioagizwa alishauri mwanahabari huyo aitwe kwani hawezi kukaidi kufika.

Mara baada ya kuwasili kituoni hapo,Kalulunga aliitwa katika chumba cha Ofisi za Upelelezi wa makosa ya jinai huku akiruhusiwa kuingia na mtu mwingine mmoja ambaye ni mtu wake wa karibu ili asikilize mahojiano hayo.

Kikao cha mahojiano kianza saa nane mchana na kumalizika saa 12 jioni,ambapo mara baada ya kutoka Kalulunga alisema amekumbana na tuhuma za kesi tatu miongoni mwa kesi hizo ikiwa ni kwa nini hivi karibuni aliandika habari iliyoonesha mapungufu ya jeshi la polisi.

“Wamenihoji kuhusua habari ya tukio la mtoto aliyesadikika kuzikwa ndani ya nyumba.Baadhi ya maswali ni pamoja na kwa nini niliandika kuwa polisi waliogopa kuingia ndani ya nyumba hiyo”

“Suala la pili wamehoji ni kwa nini kupitia mtandao wa kijamii wa Mbalizi Forum tuliweka mjadala wa risiti bandia za faini zinazotolewa na baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani wanapowakamata madereva wenye makosa”

Alisema kadhalika kesi ya tatu ilihusu Mbalizi Forum kuruhusu mjadala wa uwepo wa baadhi ya askari wanaoendekeza kupokea rushwa hususani wa kitengo cha usalama barabarani huku pia wakimlaumu ni kwa nini kupitia mtandao huo yanayojadiliwa ni mabaya tu yanayofanywa na jeshi la polisi lakini mazuri hayatajwi.

Alisema mara baada ya mahojiano alichoambiwa na afisa aliyekuwa akimhoji ni kuwa jalada hilo litafikishwa juu hivyo binafsi hakujua ni kupelekwa mahakamani au ala.


No comments:

Post a Comment