SERIKALI mkoani
Mbeya imetishia kukatisha mikataba ya madaktari watakaoendeleza mgomo mpaka
siku ya kesho(Juni 27) ikiwa ni siku tano mfululizo hawajaingia kazini.
Kaimu mkuu wa mkoa
wa Mbeya Dk.Norman Fegi ameyasema hayo leo (Juni 26) katika kikao chake na
waandishi wa habari ikiwa ni siku ya nne mfululizo tangu baadhi ya madaktari
katika hospitali ya Rufaa kuanza mgomo.
Dk.Fegi amesema tangu
kuanza kwa mgomo huo serikali ya mkoa kupitia mkuu wa mkoa ambaye kisheria
ndiye mwenyekiti wa bodi ya hospitali inayoingia mkataba na madaktari wa
mafunzo imeshawaandikia barua za kuwaita ili wafanye mazungumzo lakini jana(Juni
25) hawakufika.
Amesema baada ya
kutofika huko mkoa ukawaandikia tena barua kwa kila mmoja wao kujibui ni kwa
nini asiwajibishwe na kusisitiza kuwa iwapo mpaka siku ya tano hawatafika
kazini mkoa utavunja mkataba na kuwarudisha kwa muajiri yaani wizara husika.
Amesema kwa sasa
wamelazimika kuchukua baadhi ya madaktari kutoka vituo vya afya vilivyopo
jijini Mbeya na ndiyo wanaendelea kutoa huduma hususani katika kitengo cha
upasuaji cha hospitali ya Rufaa ambacho ndicho kimeathiriwa zaidi.
Kwa upande wake
mkurugenzi wa hospitali ya mkoa Dk.Eliuter Samky alisema madaktari waliogoma ni
45 waliopo katika mafunzo na 19 waliosajiriwa lakini wameajiriwa hivi karibuni
lakini madaktari bingwa 19 wanaendelea na kazi kama kawaida.
Samky amesema
wateja wote waliofika hospitalini hapo tangu kuanza kwa mgomo wameathirika kwa
namna moja ama nyingine ikiwa ni kwakupata huduma isiyo katika kiwango ama muda
wa kawaida au kisaikolojia.
Amesema tangu
kuanza kwa mgomo huo haijatokea kifo lakini wagonjwa 250 wamefikishwa na kulazwa
wakati wagonjwa wan je jumamosi walifika 53,jumapili 42 na jumatatu 283.
Amesema siku ya
jumapili pia ilitokea ajali ya gari na majeruhi 16 wakafikishwa hospitalini
hapo na wote walipata huduma japo si kwa kiwango kilichozoeleka siku zote.
Naye mganga mkuu
wa mkoa dokta Seif Mhina alisema mgomo wa madaktari katika hospitali ya rufaa
imeongeza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya mkoa hususani akina mama
wajawazito waliokwenda kujifungua katika hospitali hiyo kitengo cha wazazi Meta
na kukosa huduma ndipo wakaamua kukimbilia hapo.
Mhina amesema wajawazito
wanaojifungua katika hospitali ya mkoa wameongezeka kutoka wawili hadi watano
kwa siku na kufikia zaidi ya kumi huku wanaopata huduma ya upasuaji wakiongezeka
kutoka mmoja kwa siku hadi kati ya watano na kumi.
No comments:
Post a Comment