HAMASA ndogo juu
ya mfuko wa afya ya jamii(CHF) imetajwa
kuwa sababu kubwa ya wakazi mkoani Mbeya kutotambua umuhimu wa mfuko huo hivyo
hawajiungi.
Hali hiyo
imebainika katika semina elekezi kwa waratibu na waandishi wa habari mkoani
Mbeya kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) iliyofanyika katika ukumbi
wa hospitali ya mkoa.
Meneja wa NHIF
kanda ya nyanda za juu kusini Selestin Muganga alisema hamasa bado hali
inayosababisha wananchi kutojiunga na CHF kutokana na kukosa elimu juu ya mfuko
huo.
Muganga alizitupia
lawama halmashauri kwa kutolipa kipaumbele suala la utoaji elimu hiyo kupitia
kwa waratibu wa mfuko huo na kusema viongozi wengi wa halmashauri hiyo
wanazingatia miradi inayokuwa na maslahi ya moja kwa moja kwao na si ile
inayolenga kuinufaisha halmashauri kama huo.
Alihimiza kuwepo
kwa hali ya ushindani kwa kila wilaya juu ya mafanikio ya mfuko huo akisema
hali hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa halmashauri zilizolala kuona zimebaki
nyuma hivyo kuona aibu na muiga mfano wa wenzao wanaofanya vizuri.
Awali akifungua
semina hiyo ya siku moja mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya Seif Mhina alihimiza
hamasa ya CHF kutolewa katika msimu wa mavuno kama
sasa wakati ambao wananchi wengi hususani wakulima wanakuwa na kipato kizuri
madala ya masika.
Dokta Mhina alisema
wananchi wanatumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya wana familia jambo
linaloashiria kuwa elimu juu ya CHF haijawafikia hivyo hawatambui kuwepo kwa
uwezekano wa wanakaya kupata matibabu kwa shilingi 10,000 tu kwa mwaka mzima.
“Mkielimisha
hakuna mtu atakayebisha.Tatizo ni elimu bado haijawafikia Wananchi wanatumia
pesa nyingi sana
kwa matibabu ya kawaida tu.Tukiwahamasisha kuwa kaya zao zinaweza kutibiwa kwa
shilingi 10,000 kwa mwaka mzima wataridhia tu” alisema
Alisema kujiunga
kwa wingi kwa wananchi mkoani hapa kunaweza kusaidia pia kupunguza kwa kiasi
kikubwa changamoto zinazoikabili huduma ya afya katika zahanati,vituo vya afya
na hospitali zilizopo.
Aliutaja mkoa huo
kuwa na kaya zipatazo laki sita ambazo zikijiunga zote na CHF zitawezesha
kupatikana kwa shilingi bilioni sita na bima ya afya kupitia mpango wa Tele kwa
tele ikichangia bilioni sita mkoa utakuwa na jumla ya shilingi bilioni 12
ukiachilia mbali fedha zitakazotoka serikalini ambazo ni za OC shilingi bilioni
2 na za kapu(Busket Fund) bilioni tano.
Alisema fedha hizo
zinatosha kabisa kutatua changamoto zote zilizopo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa
dawa kwa matumizi ya mwaka mzima,ununuzi wa vifaatiba na ujenzi na ukarabati wa
majengo mbalimbali.
Kwa mujibu wa
takwimu kutoka NHIF kwa mkoani Mbeya zipo kaya 612,216 na kati ya hizo 17,988
sawa na asilimia 2.94 ndizo zilizojiunga na CHF ambapo wilaya ya Kyela iliyo na
kaya 39,542 inaongoza kwa kuwa na kaya 4,447 zilizosajiriwa na Ileje iliyo na
kaya 32,153 ni ya mwisho kwa kuwa na kaya 97 pekee zilizosajiriwa.
No comments:
Post a Comment