Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, June 26, 2012

NAPE AMRUSHIA DONGO LOWASA

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wametakiwa kutochagua viongozi kwa nafasi zao za kifedha wanazozitumia kurubuni wananchi kwa kutoa misaada mingi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye alitoa kauli hiyo leo(Juni 26) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya kauli inayoonekana kumhusu moja kwa moja aliyewahi kuwa Waziri mkuu Edward Lowasa ambaye hivi sasa anaonekana kukimbilia makanisani kwa kuchangia harambee mbalimbali.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo hususani ya kisiasa wamekuwa wakiitaja njia anayoitumia Lowasa kuwa njia ya kujisafisha na kujitengenezea nafasi nzuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Lakini Nape amesema wanaccm wanapaswa wautumie uchaguzi wa chama chao mwaka huu kuhakikisha viongozi wanaomwaga pesa nyingi kwa kutoa misaada wakidhani ni njia nzuri ya kuwashika wapiga kura wanatupwa nje ili kukisafisha chama chao.

Amesema kinachopaswa kufanywa na wanachama ni kuhakikisha wanachagua viongozi walio na uzalendo na chama chao na pia walio na uwezo wa uongozi ili kukijenga chama hicho badala ya kuwapa uongozi watu wanaonyooshewa vidole kila siku na wananchi.

Amewataka vijana hususani walio na elimu kujitosa kupigania uongozi wa chama hicho akisema hatua hiyo itakiwezesha kupata damu change na zilizo na nguvu ya kukiendeleza badala ya kukidumaza.  

Nnauye amekanusha pia kauli za baadhi ya watu wanaokejeli dhana ya Kujivua Gamba wakisema haijafanikiwa kauli aliyosema si kweli kwani dhana hiyo ilibeba mambo mengi ndani yake.

Amesema dhana hiyo ililenga kubadilisura ya chama kwa kuongeza damu change hali inayofanyika hivi sasa ambapo chama kimeanzisha mchakato wa kuwa nam mkoa maalumu kwaajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Amesema pia kuwawajibisha baadhi ya viongozi wasio na sifa tayari mikakati mbalimbali imefanywa na wapo baadhi ya watu walioachia ngazi mbalimbali pamoja na kuivunja kamati kuu iliyokuwa chini ya Yusuf Makamba.

“Kuna watu wamejivua uanachama mpaka ubunge tumeona leo hii mtu anasema dhana ya Kujivua Gamba haijafanikiwa mi nadhani ni uongo.Lakini pia baada ya chama kutoa muda kwa wahusika wajiwajibishe na hawakufanya hivyo sasa tuna vikao mbalimbali vinavyoendelea kpitia kamati za maamuzi na maadili.Huko nako tutatoka na maamuzi mengine” amesema.

Amesema pia katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka huu majina ya wagombea wanaokabiliwa na kashfa mbalimbali hayatarejeshwa hivyo ni vema wanachama hao wasijaze fomu kabisa.

No comments:

Post a Comment