Na,Christopher Nyenyembe,Mbeya
SHIRIKISHO la vyama vya siasa mkoa wa Mbeya limetoa tamko la
kulaani kitendo cha utovu wa nidhamu kilichoonyeshwa na Mbunge wa Jimbo la
Mbeya mjini,Joseph Mbilinyi cha
kuonyesha ishara ya kidole ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulikosababisha
apewe adhabu ya kutoshiriki vikao 10.
Mwenyekiti wa shirikisho hilo,Godfrey Mwandulusya alitoa
tamko hilo jana kwa niaba ya vyama vingine alipokuwa akizungumza na Wanahabari
kuwa viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo wamefikia uamuzi wa kulaani tukio
hilo kwa misingi ya kuimarisha demokrasia ya kweli na kumtaka Mbunge huyo
awaombe radhi wananchi wa jimbo lake na hususani mkoa huo kwa ujumla wa madai
ameshiriki kuwadhalilisha.
Mwandulusya alisema kuwa kitendo cha ‘Sugu’ kuonyesha kidole
ndani ya bunge ni cha utovu mkubwa wa nidhamu na hakikupaswa kufanywa na mbunge
aliyechaguliwa kwa kura nyingi na wananchi ambao walimuamini kama kiongozi bora
na wa mfano kwa tabia njema kumbe ni kinyume na matarajio yao.
“Kitendo cha kumuonyesha kidole Naibu Spika , Ackson Tulia
kimewadhalilisha wanawake wote,anapaswa kuwaomba radhi wakazi wa jimbo lake
,mkoa anaotoka na watanzania wote hasa ikizingatiwa kuwa ishara hiyo ni tusi
kubwa lisiloweza kutamkwa hadharani” alisema Mwenyekiti wa shirikisho hilo.
Alisema kwa pamoja viongozi wa shirikisho la vyama vya siasa walioketi na kutafakari
adhabu aliyopewa ya kutokushiriki vikao 10 hakutakuwa na maana yoyote kama
mbunge huyo hawezi kujitokeza hadharani na kuwaomba radhi wananchi waliomchagua
kwa lengo la kuwarudishia imani na jinsi walivyokipenda chama anachotoka cha
Chadema.
Alisema kuwa mamlaka iliyomdhamini na kumpa nafasi ya
kugombea ubunge ambayo ni chama chake cha Chadema kinapaswa kuliona hilo kwa
vile sehemu kubwa ya wananchi walioshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walikuwa
na kiu kubwa ya kuhitaji mabadiliko na hawakustahili kuangushwa ndio maana
umoja huo umeamua kutoa tamko.
Licha ya kumtaka Mbunge huyo kuomba radhi pia umoja huo ulipinga
uamuzi wake wa kwenda kulalamika kwa
viongozi wa dini kwa madai kuwa upinzani umekuwa hautendewi haki ndani ya bunge
kumbe alistahili kwanza kujisafisha kwa wananchi kwa kuwaomba radhi ili azidi
kuaminika na si vinginevyo.
Mwenyekiti huyo alivitaja vyama nane vinavyounda shirikisho
hilo katika mkoa wa Mbeya ni APPT-Maendeleo,UDP,TLP,UPDP, NLD,NCCR-Mageuzi,CUF
na DP na kudai kuwa umoja huo umekuwa imara ili kuongeza nguvu ndani ya mkoa
huo licha ya vyama vitatu vya NCCR-Mageuzi,NLD na CUF kujiunga na Ukawa.
No comments:
Post a Comment