Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, November 15, 2017

TARURA na matarajio ya ukombozi barabara Mbeya

Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makala akizungumza na wadau mbalimbali wa barabara siku ya uzinduzi wa Tarula mkoa(Picha na Joachim Nyambo)


Na Joachim Nyambo.

MKOA wa Mbeya ni moja kati ya mikoa nchini ambayo tayari imezindua rasmi kimkoa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA).Uzinduzi huu ulifanyika Septemba 9 mwaka huu ikiwa ni baada ya uzinduzi wa wakala huo uliofanyika kitaifa mjini Dodoma.

Kwa mkoani Mbeya ujio wa Tarura unaonekana kuwa sawa na wa mkombozi aliyesubiriwa kwa miaka mingi na sasa amewasili.Shujaa huyu alisubiriwa kwa muda mrefu na wadau mbalimbali mkoani hapa kutokana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili katika miundombinu ya usafiri wa barabara.

Changamoto za Uhaba wa miundombinu ya barabara na pia ubovu wa barabara hususani za vijijini zimekuwa zikilalamikiwa kwa miaka mingi kukwamisha maendeleo.Mambo mengi yalikwa si ya kijamii,kisiasa na hata kiuchumi.

Miongoni mwa wadau waliokuwa wamechoshwa na kilio cha barabara hizi ni wakulima.Hawa walishindwa kusafirisha kwa wakati mazao yao kutoka mashambani kuyapeleka mijiji kuliko na masoko.Hapo walijituma kuzalisha kwa wingi mazao lakini uhakika wa kuyafikia masoko haukuwepo.

Mfano mzuri ni uzalishaji wa Mazao ya mifugo hasa maziwa katika wilaya ya Rungwe,Uzalishaji mpunga katika Bonde la Usangu wilayani Mbarali na uzalishaji wa viazi mviringo Mbeya vijijini.Kutokana na kukosekana kwa barabara za uhakika usafirishaji wa mazao haya umekuwa mgumu na kusababisha wakulima au wafanyabiashara wanaoyafuata shambani kupata hasara.
 Kuna wakati mkulima aliyevuna viazi katika vijiji vya Kikondo Mbeya vijijini,Mkulima wa Ndizi vijiji vya Lufilyo Busokelo na Mkulima wa alizeti na ufuta wilayani Chunya alishindwa kusafirisha mazao yake kuyafikisha jijini Mbeya au hata yalipo makao makuu ya wilaya yake kwa kukosa usafiri.Alibaki kusubiri mfanyabiashara mwenye roho ngumu amfikie alipo na hapo ndipo alipokubali pia kunyonywa kwakuwa aliyemfikia ndiye alipanga bei.


Sasa mkombozi wa kweli ameingia.Ni Tarura anayekuja kusimamia barabara na madaraja yaliyopo mijini na vijijini.Huyu ni pacha mwenza wa Wakala wa Barabara nchini(Tanroads) anayeshughulikia barabara za kuunganisha mikoa na wilaya.

Katika Uzinduzi wa Tarura,mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla alisema ana uhakika kama vile Tanroads wanavyofanya vizuri katika kusimamia ujenzi na ukarabati wa barabara kuu ndivyo Tarura nao watafanya kazi.Kwa matawi haya mawili kufanya shughuli zao  kiuweledi ni dhahiri huduma ya usafiri wa barabara mkoani hapa na Tanzania kwa ujumla utakuwa wenye ubora na kuleta tija kwa kila mdau wa maendeleo katika kipindi cha miaka michache tu ijayo. 
“Sote ni mashahidi,tunaona kila kukicha namna Tanroads wanavyofanya vizuri,wanavyoisaidia Serikali kuunganisha mikoa kwa barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami.Hawa nao watafanya hivyo ninaamini”

“Tunaamini kuwa sasa zile changamoto za fedha kuja lakini tija isionekane kwa barabara zilizojengwa au kukarabatiwa sasa itaondoka.Fedha zinakuja mpaka zinavuka mwaka wa fedha hazijatumika kwakuwa vikao vya madiwani havikukaa nayo hatutoisikia”alisema Makalla.

Kwa kuanzia Makalla aliitaka Tarura kuanza na fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 13.2 za miradi ya barabara zinatumika kabla ya kupokea fedha za mwaka wa fedha 2017/2018.Kiasi hiki cha fedha kiliendelea kuwepo katika Halmashauri mbalimbali za mkoani hapa kufuatia kusitishwa kwa miradi yake baada ya kuundwa kwaTarura hivyo kwa sasa fedha hizo zinatakiwa kuiingizwa kwa wakala hiyo ili kazi ziendelee.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na Mameneja wa wakala hiyo wa Halmashauri za wilaya zote,wakuu wa wilaya,wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi watendaji,Makalla aliitaja Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kuongoza kwa kuwa na fedha nyingi zaidi kiasi cha Shilingi Bilioni 5.2 ikifuatiwa na Busokelo yenye shilingi Bilioni 3.8 na Mbeya jiji ina shilingi Bilioni 1.9.

Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ina shilingi bilioni 1.6,Mbeya vijijini shilingi milioni 640,Chunya milioni 15.8 na Halmashauri iliyokuwa imetumia fedha zote kabla ya kubadilishwa kwa utaratibu ni ya wilaya ya Mbarali.

Alitaka Tarura kuanza kutumia fedha hizo mara moja kuendeleza miradi iliyokuwa imeanza ili kuharakisha maendeleo ya wananchi kupitia uimarishaji wa miundombinu ya barabara na madaraja.Iwapo wakandarasi walikuwa hawajalipwa sasa walipwe waendelee na kazi ili wazikamilishe haraka.

“Kusiwe tena na sababu ya wakandarasi kutoendelea na kazi.Walipeni kwa kazi walizokuwa wamekamilisha na pia hakikisheni wanaanza kazi au kuendelea na zile zilizokuwa zimesalia.Lengo hapa ni kuharakisha maendeleo ya wananchi”

Aliwataka Watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha wanayapa kipaumbele maeneo yaliyo na changamoto kubwa ya barabara hususani yaliyo na uzalishaji mkubwa wa mazao lakini waananchi wamekuwa wakipata usumbufu kuyasafirisha hadi barabara kuu na kwenye masoko.
 “Huko nyuma mnajua fedha zilizokuwa zikiletwa mpaka zigawanywe gawanywee kwenye kata zinabakia kidogo.Na kuna baadhi ya maeneo fedha hazikuonesha kabisa kuleta matokeo.Hilii ilikuwa kwa sababu kila mmoja alitaka aridhishwe”

Hata hivyo Makalla alisisitiza ushirikiano baina ya Maafisa wa Tarura,Ofisi za wakuu wa wilaya na Halmashauri akisema pande zote bado zinategemeana katika kutekeleza majukumu hivyo ni muhimu kushirikiana lakini kwa kila upande kuheshimu mwingine.

“Msije mkajiona Tarura mmekuwa ninyi ndiyo ninyi mkapandisha mabega juu.Lazima uwepo ushirikiano,mkuu wa wilaya lazima atakuja kukagua miradi kwakuwa ndiye msimamizi wa shughuli zote za Serikali katika wilaya.Madiwani nao lazima watakuwa na ziara za kukagua miradi yenu ili wawaeleze wananchi.Lakini na ninyi mtakuwa na kazi ya kushauri kitaalamu siyo kwakuwa fedha zimekuja basi kila diwani atake baraba inayokwenda kwake ndiyo itengenezwe”

“Wala hapa Halmashauri msilalamike mkasema wamenyang’anya kazi zenu.Na madiwani msione kuanzishwaTarura basi changamoto za barabara kwenye halmashauri zenu hazitofanyiwa kazi.Ainisheni kupitia vikao vyenu wapeni ili waoa waratibu kitaalamu.Hakuna anayefanya la kwake hapa sote tunamlenga mwananchi.Na ndiyo sababu tunawataka Halmashauri mkabidhiane mali na Tarura bila malumbano”

Makalla anasema matokeo makubwa ya Tarura yanatakiwa yalenge kuleta unafuu kwenye maeneo yenye changamoto ya kusafirisha mazao hasa yale yaliyo na uzalishaji mkubwa

“Uzuri Tarura bado watawajibika katika kikao cha bodi ya barabara ambacho ninyi ni wajumbe.Mtawahoji huko na mtawapima.Kikubwa tunataka Tarura ilete mabadiliko ili kuonesha umuhimu na maana ya kuanzishwa kwake.”

Katibu Tawala mkoa wa Mbeya,Marium Mtunguja alizitaka Halmashauri na Watendaji wa Tarura kuzitendea haki Fedha wanazo pelekewa kwaajili ya miradi badala ya kuona ni sifa kubaki nazo mpaka mwaka wa fedha unamalizika.

“Siyo sifa kubaki na fedha nyingi za miradi wakati wananchi wanapata shida.Ni bora ubakiwe na sifuri lakini kazi ziwe zilifanyika.Jitahidini kutumia fedha kwa kazi zilizokusudiwa.Msione fahari kuziona fedha kwenye akaunti zenu.”anasema Mtunguja.

Mratibu wa Tarura mkoa wa Mbeya,mhandisi Danstan Kishaka,aliwataka mameneja wa wilaya wa wakala hiyo kutambua kuwa kuondolewa kwao katika Halmashauri kunalenga kuboresha kazi hivyo mahitaji ya Serikali ni kuona Utekelezaji wa miradi ya barabara sasa unakuwa wa kiwango kinachohitajika.

“Tunatakiwa tuwe Tai wapya wenye kuona mbali katika kuwatumikia wananchi.Hatupaswi kujenga kiburi na sote tunajua huku hakuna kuazimiwa huku ukiharibu ni barua moja kwa moja hivyo lazima tutambue kuwa tupo kuhakikisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kupitia Barabara.Na lazima kwakuwa tutaendelea kutumia ofisi za Halmashauri kwa muda unapotoka nje ya kituo lazima mkuu wa wilaya yako na Mkurugenzi wajue”alisema Kishaka.

Wenyeviti wa Halmashauri za wilaya mkoani hapa wanasema Tarura imekuja kwa wakati muafaka kwani itapunguza mivutano iliyokuwepo baina ya madiwani na kusababisha pesa iliyotengwa kutoonesha tija.

“Madiwani walikuwa wanabeba mzigo mzito.Ilikuwa hata zikija shilingi laki tano inabidi wazigawane,ili kila mmoja aonekane alifanya kitu kwa watu wake.Muhimu hapa msianze na fedha,anzeni na kuzijua barabara ninyi ni wataalamu lakini wanaozijua barabara ni wananchi,hakikisheni mnawafikia huko waliko.”alisema Mwenyekiti wa wenyeviti wa Halmashauri za mkoani hapa Anyosisye Njobelo ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Busokelo.

“Lakini imefika pia wakati tuachane na wimbo wa kupata taarifa kwenye makaratasi,tunataka kuona barabara.Kilio cha wananchi ni kupunguziwa mzigo wa gharama kubwa ya kusafirisha mazao toka mashambani”aliongeza.

Chalya Julius ni mwenyekiti wa wakuu wa wilaya mkoani hapa,anasema “Sote tunaamini Tarura ni chombo kilichopewa jukumu kwa niaba ya serikali hivyo yote yaliyoamriwa yatatekelezwa”

“Wakuu wa wilaya tutatoa ushirikiano wa kutosha na pia kusimamia mashirikiano baina ya Tarura na Halmashauri.Zaidi tutasimamia viwango vya kazi za barabara”alisema Julius ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Rungwe.

Baadhi ya wananchi kutoka maeneo ya pembezoni,wanasema wanachosubiri ni matokeo chanya na si ubabaishaji.Wanasema kujengwa na kukarabatiwa kwa barabara maeneo ya pembezoni kutainua kipato chao na pia kutarahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii zikiwemo za Afya.

“Watu wanajituma kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi lakini wanakatishwa tama na uhaba wa masoko.Tunaamini hata wawekezaji wanaogopa kuja kuwekeza viwanda maeneo ya pembezoni kutokana na miundombinu duni ya barabara”alisema Mkazi wa Lwangwa Busokelo,Neva Matinya. 

No comments:

Post a Comment