MKUU WA mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amewataka
madiwani na watendaji katika halmashauri za wilaya kila mmoja kujiuliza yupo
katika nafasi yake kwaajili ipi.
Kandoro amesema kwa kufanya hivyo kila mmoja alipo
ataweza kutambua wajibu wake na kuhakikisha anautekeleza akilenga kuyabadili
maisha ya wananchi waliomwajiri.
Mkuu huyo wa mkoa,aliyasema hayo juzi(Oktoba 10)
katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje
kilicholenga kujadili taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa serikali CAG.
Alisema wapo baadhi ya madiwani na watendaji ambao
wamekuwa wakiyasahau majukumu yao na kujikuta wanaendekeza siasa katika kila
wanalofanya pasipo kutambua kuwa kufanya hivyo kunawacheleweshea maendeleo wananchi
katika maeneo yao.
Aliwataka madiwani kuhakikisha wanakuwa na
mshikamano katika kutafuta sukluhu za changamoto zinazowakabili wananchi badala
ya kuendeleza makundi yaliyotokana na kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Kandoro alisema ushirikiano wa pamoja baina ya wadau
hao kwa kushirikiana na wananchi ndio unaoweza kuongeza kipato cha mwananchi
mmojammoja ambaye kwa mafanikio hayo ataweza kuuchangia uchumi wa wilaya hiyo
na kuiondoa katika hali ya utegemezi wa asilimia 98 ya bajeti yake kutoka
serikali kuu.
Alisema ni vema wadau hao wakaona aibu kwa
halmashauri yao kuwa na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia mbili pekee wakati
ambao mkakati wa serikali ni kuona halmashauri zinajitegemea kwa asilimia 50.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo Glads Dyamvunye alisema ukosefu wa vyanzo vya mapato ni changamoto kubwa
kwa halmashauri yake hali inayopelekea kuendelea kuwa tegemezi kwa serikali kuu.
No comments:
Post a Comment