MBUNGE wa Mbarari Modestus Dickson Kilufi aliyekuwa
anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutishia kuua atafikishwa mahakamani kesho
jumatatu(Oktoba 10) na kwa sasa yupo nje kwa dhamana.
Mbunge Kilufi alikamatwa juzi(Oktoba 7) saa 10 jioni
akiwa ofisini kwake ambapo kwa mujibu wa maelezo yake askari waliofika
kumkamata ofisini hapo walimweliza kuwa alitishia kumuua ofisa mtendaji wa kata
ya Ruiwa Jordan Masweve.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi
alithibitisha kuachiwa kwa dhamana mbunge Kirufi alipozungumza na waandishi wa
habari kwa njia ya simu.
Nyombi alisema mbunge huyo yupo nje kwa dhamana na
atafikishwa mahakamani siku ya jumatatu kusomewa shitaka la kutishia kuua kwa
maneno.
Hata hivyo kamanda huyo hakutaja mbunge atafikishwa
katika mahakama ipi bali alisema ofisi ya mwanasheria wa serikali mfawidhi mkoa
wa Mbeya ndiyo inayotambua mahakama hiyo kwani hata kukamatwa kwake kulilenga
kutekeleza agizo la ofisi hiyo.
“Baada ya askari wetu kumkamata jana,leo hii
tumemfikisha katika ofisi ya mwanasheria wa serikali na wao ndiyo watamfikisha
mahakamani.Lakini hivi sasa yupo nje kwa dhamana na shitaka linalomkabili ni
kutishia kuua kwa maneno” alisema Nyombi
Kwa upande wa Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM
mkoa wa Mbeya umesema hauhusiki na mashitaka yanayomkabili mbunge huyo kwani ni
masuala yake binafsi na si ya chama.
Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Verena Shumbusho alisema
jana kuwa shitaka la kutishia kuua linalomkabili mbunge kirufi chama hakiwezi
kulitolea tamko lolote.
“Kama chama hatuwezi kutoa tamko lolote juu ya
kukamatwa kwake wala shitaka linalomkabili.Hilo ni suala lake binafsi na chama
hatulitambui kabisa” alisema Shumbusho.
No comments:
Post a Comment