Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, April 17, 2018

RC MAKALLA ATAKA KANISA LA MORAVIAN NA WANANCHI WAKAE WAZUNGUMZE KUMALIZA MGOGORO

SERIKALI mkoani Mbeya imesema ipo haja ya pande mbili kuridhiana ili kumaliza mgogoro wa ardhi uliopo kati ya Kanisa la Moravian Tanzania na wakazi wa kijiji cha Ilolo wilayani Rungwe.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 27 bado haujamalizika kwakuwa pande hizo mbili zinaendelea kuvutana lakini amesema anaimani baada ya jitihada nyingi zinazofanyika unaweza ukamalizika iwapo pande hizo zitaridhiana.

Makalla amebainisha hayo kwenye Kikao cha kusikiliza kero za wananchi kilichofanyika wilayani Rungwe ambapo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ilolo walifika na kuwasilisha kero ya kulitaka kanisa kuwaachia ardhi yao.

Hata hivyo kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe,Bibi Loema Peter amesema ni vema wakazi wa kijiji hicho wakawa watulivu na kufuata maelekezo waliyopeana siku chache zilizopita ili kusaidia kumalizika kwa mgogoro.

Bi Peter amesema yapo mambo ambayo wamekubaliana yatekelezwe kila upande hatua iliyotokana na ushauri uliotolewa na kamati maalumu iliyoundwa na mkoa kufuatilia mgogoro huo.

Kwa upande wake Afisa ardhi mkoa wa Mbeya,Enock Kyando amesema mmiliki halali wa eneo linalogombaniwa ni kanisa la Moravian lakini kwakuwa uongozi wa kanisa uko radhi kutoa sehemu ya eneo lake kwa wananchi ni vema pande hizo zikakaa na kukubaliana.

Kufuatia hali hiyo,Makalla aliwataka wananchi kuwa na subira lakini akawataka pia waone uchu wa kumaliza mgogoro baina yao na kanisa ili kwa pamoja waweze kuishi kwa amani na utulivu.

Makalla ameahidi kufika kijijini Ilolo ili kutangaza maazimio yatakayokuwa yamefikiwa baada ya taratibu za pande zote zinazoshughulika na mgogoro huo kukamilika.

WAKATI HUO HUO

SERIKALI mkoani Mbeya imeagiza maafisa watendaji wa vijiji na Kata wanaoendelea kutumia majengo ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kama Ofisi zao waondoke mara moja na kutafutiwa ofisi zao.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla alitoa agizo hilo kwenye kikao cha Kusikiliza Kero za wananchi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Tukuyu kilichopo Msasani wilayani Rungwe na kuwakutanisha wananchi wa halmashauri za Busokelo na Rungwe.

Makalla alisema halmashauri inapaswa kuwajibika kwa kuwatafutia Maafisa watendaji Ofisi zao ili kuondoka kwenye mfumo wa chama kimoja uliokuwa ukiruhusu maafisa hao kutumia majengo ya chama kufanya shughuli zao.

Alisema kuondoka kwa maafisa hao kwenye majengo ya CCM pia kutawezesha kuondokana kwa sintofahamu za kiutendaji zinazojitokeza hususani wakati wa changuzi ambapo Ofisi hizo lazima zihudumie watu kutoka itikadi za vyama tofauti.

“Wakati wa uchaguzi mtendaji unatakiwa uhesabie kura na utangaze matokeo ofisini kwako sasa pale unapokuwa kwenye ofisi za CCM halamu unatangaza mgombea wa chama hicho hicho ndiyo ameshinda,au mgombea wa chama kingine ameshinda halafu uko ndani ya jengo la CCM lazima itakupa utata.Hii iliwezekana wakati wa mfumo wa chama kimoja lakini kwa sasa nataka Mkurugenzi maafisa hawa watafutiwe ofisi zao waondoke kwenye majengo ya chama”alisisitiza Makalla.

“Najua zipo propaganda kwa baadhi ya watu wasio na uelewa kuwa oooh endeleeni kukaa humo humo kwakuwa ofisi tulijenga wote wakati wa mfumo wa chama kimoja. Hao ni waongo hivi mnapomchangia mtu Harusi siku wakiachana mnakwenda kudai michango yenu?”alihoji.

Makalla aliyasema hayo kufuatia baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM kuwasilisha kero kwenye kikao hicho juu ya uwepo wa Baadhi ya maafisa watendaji wanaoendelea kutumia majengo ya chama hicho kama ofisi zao na kusababisha baadhi ya shughuli za chama kukwama.

No comments:

Post a Comment