Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Friday, December 2, 2016

KIKONGWE APONZWA NA FEDHA ZA TASAF,AITWA MCHAWI NA KUTIMULIWA KIJIJINI

KIKONGWE anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 70 na 75  mkazi wa kijiji cha Tindingoma kata ya Chitete wilayani Momba mkoani Songwe amejikuta analazimika kulala porini na kwenye mapagara kwa siku mbili kwa hofu ya kuuawa na wakazi wenzake kwa tuhuma za ushirikina.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, bibi kizee huyo aliyejitambulisha kwa jina la Agness Nakapange alisema kuwa ameamua kulala porini na kwenye mapagala kwa hofu ya kuuawa na wananchi wenzake ambao walimtisha kuwa watamuua endapo ataendelea kukaa katika nyumba yake.

Hata hivyo Nakapange aliyekataa katakata kujihusisha na masuala ya Kishirikina maishani mwake,alisema anachokiona ni wivu kutoka kwa baadhi ya majirani kutokana nay eye kuwa sehemu ya wanufaika wa Mpango wa kuokoa kaya Masikini unaoendeshwa na Mfuko wa jamii wa TASAF III

Nakapange alisema kuwa kuna wakati aliitwa na baadhi ya wananchi kijijini hapo wakimtaka awanunulie pombe za kienyeji walau nusu debe kwa lazima baada ya kumuona amepata fedha za TASAF.

Alisema wakazi hao walifanya hayo wakati wanajua dhahiri ya kuwa yeye ana wajukuu ambao wanamtegemea kwani watoto wake wote walifariki hivyo yeye na wajukuu zake hawana msaada wowote.

Alidai kuwa baada ya vitisho kuzidi nay eye kuona kuwa hali imekuwa mbaya alilazimika kununua pombe kwa kuhofia kuwa atauawa na wananchi hao kwani wakati wanazungumza naye walikuwa wakimzonga yeye ni mchawi na kuwa ndiye aliyeua wanae.

Akizungumzia sakata hilo,Afisa mtendaji wa kata ya Chitete Erasto Simchimba alikiri kumpokea bibi huyo katika ofisi zake jana majira ya asubuhi na kudai kuwa atakuwa naye katika ofisi zake mpaka pale atakapoitisha vikao na wananchi ili kutatua tatizo hilo.

Katika hatua nyingine Simchimba alisema tuhuma za Ushirikina anazopewa kikongwe huyo ni fitina tu na ni kukosa elimu kwa wananchi kwani tangu afike hapo hajawahi sikia kitu chochote kibaya kutoka kwa bibi huyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Tindingoma, Daniel Silungwe alidai kuwa yeye alikuwa hana taarifa hizo hivyo kuahidi kushughulikia tatizo hilo ambapo nae ameahidi kukaa naye nyumbani kwake ili kumnusuru  kutokana na kutishwa na wananchi.

No comments:

Post a Comment