Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, February 20, 2018

MKANDARASI UWANJA WA SONGWE KUFIKISHWA MAHAKAMANI











Chini-Naibu waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi ,Mhandisi Atashasta Nditiye(katikati) akikagua picha za jengo la abiri la uwanja wa ndege Songwe alizopiga kwenye simu yake baada ya kutoridhishwa na kazi ya ujenzi wa jengo hilo
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini(TAA) kuipeleka mahakamani kampuni ya DB Shapraya kwa kushindwa kutekeleza kwa wakati kazi ya ujenzi wa Jengo la Abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe uliopo mkoani Mbeya.

Serikali pia imeagiza TAA kuanza kukata fedha kama adhabu ya kuchelewesha mradi kuanzia Januari 30 mwaka huu kwa kampuni hiyo ambayo licha ya kulipwa fedha zote na Serikali imeshindwa kutekeleza mradi huo.

Naibu waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano,Mhandisi Atashasta Nditiye alitoa maagizo hayo juzi(jumamosi) alipofanya ziara ya kushitukiza katika uwanja wa Songwe na kukuta hakuna kazi yoyote inayoendelea.

Nditiye alisema ni jambo lisilokubalika kuona fedha ya watanzania iliyolipwa ikiendelea kuchezewa kwa miaka mitano huku kazi iliyotarajiwa kufanyika ikiendelea kupigwa danadana.

“Mkataba ulielekeza kwamba hili jengo liishe ndani ya miezi minane.Kulitokea matatizo ya hapa na pale,kubalilisha design na design ikabadilishwa kweli kukawa na delay ya mabadiliko na ilikubalika kwa pande zote mbili.Lakini vile vile kukawa na tatizo la kifedha kutoka Serikalini sababu zikatolewa mkandarasi akazielewa na Serikali ikazielewa.”

“Ikafika mahali 2015 mapema mwezi wa pili pesa flani ya ajabu ajabu ikatoka kwaajili ya kumpatika mkandarasi ajenge amalizie hili jengo lakini tangu kipindi hicho apate hiyo pesa kwanza yeye mwenyewe alikuwa haamini ameipataje pataje!Kwa maneno yao lakini wao wanajua waliipataje kwa sababu kwa bahati mbaya au nzuri kuna ujanja ujanja mwingi sana ulikuwa unatumika hapa siku za nyuma”

“Lakini mpaka saa hizi ninavyoongea ni kwamba hawa watu hawaidai Serikali fedha yoyote .Sasa hivi Serikali ndiyo inawadai kwa hatua iliyofikiwa.Nawashauri waache kufanya kazi kiujanja ujanja na nitataka TAA kuanzia tarehe 31 ambayo ni deadline waliyopewa na waziri waanze kukata hasara inayotokana na kuchelewesha kazi” alisisitiza naibu waziri

Alisema kwa hali aliyoiona baada ya kutembelea mradi huo mkandarasi huyo hata angeongezewa muda zaidi mwaka huu ungemalizika pia pasipo jengo hilo kukamilika na hata mwakani pia hivyo hakuna sababu ya kuendelea na kazi hiyo.

“Nimeingia hapa hakuna shughuli yoyote inayoendelea ninyi wenyewe mmeona. Tulichofanikiwa ni kuvalishwa haya manguo na kupewa makofia lakini hakuna kazi,sehemu yenye kazi ninyi wenyewe mnajua inavyokuwa imechangamka.Hakuna mafundi tumekuta hawa wasimamizi tu ambao nao ni wageni hata hawajui lolote wana miezi mitatu”

“Nimemuona mkandarasi mshauri naye yuko hapa naye amekuja kwakuwa amejua nakuja hana maelezo yoyote kwa ujumla.Ataniambia nini wakati mkandarasi hayupo kwenye site.Taa wajiandae kumpeleka mahakamani”

Nditiye alisema lengo la Serikali ni kuona miradi inayotakiwa na wananchi inafanyika na kumalizika kwa wakati,hivyo kwa mradi huo atatafutwa mkandarasi mwingine tatakayemalizia ujenzi huo ndani ya mwaka huu.

“Tunataka awamu hii kuonyesha kwa vitendo kuwa tunafanya kazi za wananchi.Na tumejipanga kweli kufanya kazi za nchi.Mh Rais halali anatafuta pesa,pesa inalipwa mtu hataki kufanya kazi anakimbia site.Tutahakikisha hizi pesa anazitema na kweli tutahakikisha zinarudi hizi pesa na hili jengo litaisha kwa wakati tunaohitaji sisi”

Naibu waziri huyo alilaumu hatua ya baadhi ya wakandarasi wazawa kutowajibika kwa kazi wanazopewa licha ya Serikali kuwapa upendeleo ikiamini fedha izaowalipa zitabakia hapa nchini na kuwaongezea mitaji watanzania.

Alisema hatua stahiki dhidi ya mkandarasi huyo haitoishi kumfikisha mahakamani na kumtoza adhabu ya fidia ya kuchelewesha mradi bali pia kumshitaki katika bodi ya makandarasi nchini ili nayo ichukue hatua stahiki.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa viwanja vya ndege vya mikoa,Joseph Nyahende alisema mradi huo ulikuwa wa kukamilisha kazi tatu ambazo ni ujenzi wa maegesho ya ndege,barabara na jengo la abiria.

Alisema ulikuwa ni mkataba wa shilingi bilioni 11 na hadi Desemba mwaka jana Bilioni 9.7 zilikuwa zimelipwa kwa mkandarasi hivyo kwa hatua ya kazi iliyofikiwa mkandarasi huyo haidai Serikali bali anadaiwa kazi.

Kwa upande wake Mkandarasi mshauuri kutoka kampuni ya Unitec ya nchini Dubai,Mhandisi  Silanda Dustan alisema kinachoonekana ni mkandarasi kushindwa kutekeleza majukumu ya kazi aliyopewa wakati wananchi wanamatumaini na wanasubiri miundombinu ili wakuze uchumi wao.

“Sisi tumeshauri Serikali kuwa mkandarasi hawezi tena kufanya kazi hii hivyo ni wakati kuchukua hatua zinazostahiki.Hayupo kazini.Kuna hiyo hasara ya kuchelewa kwa mradi.Kama abiria wangekuwa wanapita hapa Serikali ingepata kodi na pesa ya wananchi iliyotolewa kwaajili ya ujenzi huu ingekuwa imeanza kurudi sasa”

Naye mwakilishi wa mkandarasi mhandisi George Ngutoto alisema ana uhakika iwapo Serikali ingewaongeza fedha nyingine hadi juni 30 mwaka huu mradi huo ungekamilika na kukabidhiwa kwa Serikali.


No comments:

Post a Comment