Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Wednesday, May 20, 2015

TAS YATOA MSAADA WA TSH.1,000,000 KWA MTOTO ALBINO ALIYEKATWA KIGANJA



 Afisa Mradi wa shirika la watu wenye ulemavu wa ngozi nchini (TAS) Severin Mallya akikabidhi kiasi cha shilingi milioni moja kwa mtoto Baraka Cosmas(6) aliyekatwa kuiganja na watu wasiofahamika na kulazwa katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya.Katikati ni mama wa mtoto huyo Priscar Shaban.Kulia ni mmoja wa viongozi wa TAS Mbeya mjini.


 Afisa Mradi wa shirika la watu wenye ulemavu wa ngozi nchini (TAS) Severin Mallya akikabidhi kiasi cha shilingi milioni moja kwa mtoto Baraka Cosmas(6) aliyekatwa kuiganja na watu wasiofahamika na kulazwa katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya.Aliyesimama ni Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Rukwa Dionisia Njuuli akimsubiri mtoto Baraka ili waanze safari kuelekea Dar es salaam.



 Muuguzi wa zamu akiwa pamoja na mtoto Baraka na mdogo wake Lucy kabla ya Baraka kuanza safari kuelekea Dar es salaam na hatimaye kupelekwa nchini Marekani na shirika la Under the same sun kwaajili ya matibabu ya kutengenezewa kiganja cha bandia.



 Wauguzi wengine pia walijumuika kumuaga Baraka.

                               HABARI KAMILI



SHILINGI 1,000,000 zimetolewa na Chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi nchini(TAS) ikiwa ni msaada kwa familia ya Mtoto Baraka Cosmas(6) aliyekatwa kiganja cha mkono wake na watu wasiojulikana.

Afisa Mradi wa TAS Severin Mallya amekabidhi msaada huo kwa familia ya mtoto huyo iliyopewa hifadhi ya muda katika hospitali ya Rufaa kanda ya nyanda za juu kusini iliyopo mkoani Mbeya.

Akikabidhi msaada huo,Mallya amesema TAS bado inaamini kuwa mapambano dhidi ya vitendo vya kikatili vinavyofanywa na watu dhidi ya jamii ya watu walio na ualbino yatafanikiwa iwapo jamii yote itahusika.

Amesema ni jambo la msingi kila mwanajamii akatambua kuwa anawajibu mkubwa wa kuwalinda watu walio na ualbino sambamba na kushiriki katika utoaji wa elimu yenye kupinga imani potofu kuwa viungo vya watu wa jamii hiyo vinaweza kumtajirisha mtu.

Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto Baraka,alishukuru michango ambayo imekuwa ikitolewa na wadau mbalimbali sambamba na huduma za kiafya alizopewa yeye na mwanaye katika kipindi chote cha uwepo wao katika hospitali ya Rufaa hata mwanaye kuweza kupata unafuu katika jeraha lake.

Wakati TAS wakitoa msaada huo,Mtoto Baraka tayari amesafirishwa kutoka jijini Mbeya hadi Dar es salaam tayari kwa matibabu zaidi ikiwemo kutengenezewa kiganja cha bandia.

Akizungumza na Lyamba Lya Mfipa kabla ya kuanza safari kuelekea Dar es salaam,Afisa ustawi wa jamii mkoa wa Rukwa Dionisia Njuuli alisema mtoto Baraka atakabidhiwa kwa kituo cha shirika la Under the same sun ambao watampeleka Marekani kwaajili ya matibabu zaidi.

Njuuli amesema mama wa mtoto Baraka ataendelea kuishi hospitalini hapo sambamba na wanae wawili walio na ualbino mpaka pale serikali ya mkoa wa Rukwa itakapokuwa imetoa kauli juu ya mahali salama wanapoweza kuishi.

No comments:

Post a Comment