KUTOFANYA kazi kwa umoja kwa watendaji katika
halmashauri ya wilaya ya Rungwe kumetajwa kuwa chanzo cha kudorola kwa utendaji
kazi ndani ya halmashauri hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alisema jana
kuwa taarifa alizonazo ni kuwa watendaji ndani ya halmashauri hiyo hawana
ushirikiano hata kidogo na badala yake kila mmoja anatekeleza majukumu yake
kivyake.
Hali hiyo ilijidhihirisha wazi pale watendaji
walipotakiwa kujibu maswali yaliyohojiwa na mkuuu wa mkoa yaliyotokana na hoja
za mkaguzi na ndipo kila afisa akaonekana kuwa na majibu yake na kuleta
mkinzano ndani ya kikao.
“Inaonekana hamfanyi kazi kama timu.Ninazo habari
kuwa hakuna umoja kati yenu.Kila mmoja anafanya mambo yake ajuavyo yeye.”
Alisema Kandoro kwenye kikao cha kupitia taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi wa
hesabu za serikali(CAG) katika mwaka wa fedha 2013/2014.
Kandoro alisema hali hiyo ndiyo inayochangia kwa
kiasi kikubwa kukwama kwa shughuli za kimaendeleo na kuzalisha hoja nyingi za
kiukaguzi zisizo za msingi ndani ya halmashauri hiyo.
Aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kutambua
kuwa kufanya kazi kama timu ndiyo silaha pekee inayoweza kumwezesha kila mmoja
wao kuonekana anawajibika katika nafasi yake na hivyo maendeleo ya wananchi
kupatikana kwa urahisi.
Alisema anahitaji kuona wanafanya kazi kama timu
kuanzia ngazi ya mkurugenzi mtendaji,menejimenti,watendaji na mpaka kwenye kata
na vijiji huku wakitambua kuwa kilichowakutanisha ni kuwatumikia wananchi wa
Rungwe.
Akizungumzia suala la udhibiti wa mapato ya
ndani,Kandoro alisema bado inaonekana kuwepo kwa mianya ya upotevu wa fedha
hivyo si kiasi chote kinachokusanywa na halmashauri kinakwenda sehemu sahihi na
kuitaka ofisi ya katibu tawala mkoa kulifanyia kazi suala hilo.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliagiza kutafutwa kwa
ufumbuzi wa haraka juu ya malalamiko yaliyofikishwa kwake na watumishi wa
halmashauri hiyo wakiwemo wa idara ya afya wanaolalamikia kukatwa mishahara yao
pasipo sababu za msingi.
Alisema hali hiyo inakwamisha utendaji kazi wa
watumishi na menejimenti kubaki ikitoa visingizio visivyo vya msingi pale
inapobainika wananchi kutopata huduma kikamilifu kwenye idara husika.
No comments:
Post a Comment