Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Thursday, January 5, 2017

SAKATA LA KABURI LA ALBINO LAINGIA KATIKA SURA MPYA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

JESHI LA POLISI TANZANIA.






                                                                                                              Ofisi ya Kamanda wa Polisi,                                                                                                                                                                                                                                                                                                   Mkoa  wa  Mbeya,                                                                                    

Namba ya simu 2502572                                                                                               S. L. P. 260,

Fax - +255252503734                                                                                                        MBEYA.


              tanpol.mbeya@gmail.com

                                                       



TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 05.01.2017.



Mnamo tarehe 04.01.2017 majira ya saa 06:00 asubuhi huko maeneo ya Kitongoji cha Songambele kilichopo Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la YELA AMONI [30] mkazi wa Italazya aliuwawa baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali kwa mawe na fimbo wakati akifukuwa kaburi alilozikwa SISTA SISALA mwenye ulemavu wa ngozi (albino) aliyefariki dunia tarehe 28/02/2010 na kuzikwa tarehe 29/02/2010 kwenye makaburi yao ya familia.



Awali majira ya saa 00:30 usiku wa kuamkia tarehe 04.01.2017 marehemu na wenzake wawili walifika kaburini hapo na kuanza kufukua kaburi lakini kabla hawajamaliza wananchi waligundua na kuwazingira lakini wawili walikimbia na kufanikiwa kumkamata JONAS JOHN [28] mkazi wa Chapakazi akiwa ndani ya kaburi akifukua ambaye kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa mahojiano.



Kutokana na hali hiyo, wananchi wa eneo hilo waliendelea kulinda kaburi hilo kwa siri na ndipo marehemu YELA AMONI alirudi kaburini hapo na kutaka kuendelea kufukua na ndipo wananchi hao walipomzingira na kuanza kumshambulia hadi kufariki dunia. Chanzo cha tukio hili ni imani za kishirikina kwani marehemu na wenzake walikuwa wanataka mifupa ya marehemu SISTA SISALA ambaye alikuwa mlemavu wa ngozi [albino]. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule Ifisi. Upelelezi unaendelea.



Mnamo tarehe 05.01.2017 majira ya saa 06:00 asubuhi huko Mikumi, Kata ya Kyela, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la HILDA SIGARA [30] Mkazi wa Mikumi alifariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali kwa matibabu baada ya kupigwa nyundo kichwani na mume wake aitwaye REBSON TWEVE umri kati ya miaka 30 – 35 Mkazi wa Mikumi Wilaya ya Kyela.



Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani inasadikiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.



Mtuhumiwa alitoroka mara baada ya tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea. Eneo la tukio kumekutwa nyundo moja, kisu kimoja na fimbo ya muanzi ambavyo vinasadikiwa kutumika katika tukio hilo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Kyela ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu. Upelelezi unaendelea.



Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na taarifa ya vifo na kujinyonga kama ifuatavyo:-



TAARIFA ZA VIFO:



Mnamo tarehe 05.01.2017 majira ya saa 06:30 asubuhi huko maeneo ya Majengo, Kata ya Nonde, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipokea taarifa kuwa Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la EDWARD PETER [60] Mfanyabiashara na Mkazi wa Majengo amekutwa amefariki dunia chumbani kwake.



Mwili wa marehemu haukukutwa na jeraha lolote. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu. Upelelezi unaendelea.



Mnamo tarehe 04.01.2017 majira ya saa 15:00 alasiri Kijiji cha Kiwanja, Kata ya Mbugani, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ABIUDI COSMAS [18] Mkazi wa Kiwanja Wilayani Chunya alifariki dunia baada ya kuangukiwa Kifusi cha Mchanga wakati anajaribu kuchimba madini ya dhahabu.



Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.



TAARIFA YA KUJINYONGA:



Mnamo tarehe 05.01.2017 majira ya saa 00:20 usiku huko Kijiji na Kata ya Mbugani, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ROBERT MWAISENYE [18] Mkazi wa Mbugani alikutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila akiwa ndani ya nyumba yake.



Chanzo cha tukio hili bado hakifahamika, uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo chake. Upelelezi unaendelea.

WITO:



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii kuacha tamaa mali/fedha kupitia njia zisizo halali kwani Jeshi la Polisi halitaruhusu wala kufumbia macho vitendo kama hivyo na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa lengo la kujipatia kipato halali kuendesha maisha yao. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anaendelea kutoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kosa kisheria na badala yake wawafikishe kwenye mamlaka husika watuhumiwa wanaowakamata kwa tuhuma mbalimbali kwa hatua zaidi za kisheria. 



  

                                                   Imesainiwana:  

[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment