Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas
Kandoro na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya wakimwangalia mtoto Baraka Cosmas(6) mwenye
ulemavu wa ngozi(albino) aliyelazwa katika hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya
baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiofahamika walipomtembelea jana.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya wakisali pamoja na viongozi wa Chama Cha watu wenye ulemavu wa Ngozi(albino) katika wadi ya watoto walipofika kumjulia hali mtoto Baraka Cosmas.
Mama wa mtoto Baraka, Priscar Shaban(28)akielezea namna alivyovamiwa nyumbani kwake na kisha mwanaye huyo kukatwa kiganja
HABARI KAMILI
WAKUU wa mikoa ya Mbeya
na Rukwa,Abbas Kandoro na Stella Manyanya jana walimtembelea mtoto Baraka
Cosmas(6) mwenye ulemavu wa ngozi(albino) aliyelazwa katika hospitali ya Rufaa
kanda ya Mbeya baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu
wasiofahamika.
Mtoto huo mkazi katika
kijiji cha Ikonda kata ya Chitepa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alihamishiwa
katika hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kiganja chake akitokea kituo
cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba.
Kwa mujibu wa mama wa
mtoto huyo Prisca Shaban(28) tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa saba usiku
ambapo alipokuwa anarudi ndani akitokea nje kujisaidia alivamiwa na mtu ambaye
hakumfahamu na kisha akamsukumia ndani kabla ya kumpiga kichwani kwa rungu na kisha
kupoteza fahamu.
Mama huyo alisema akiwa
amepoteza fahamu mtu aliyekuwa amemvamia ndipo alipata nafasi ya kuingia ndani
na kutekeleza adhma yake ya kumkata kiganja mmoja wa watoto watatu wenye
ualbino katika familia hiyo na kuondoka nacho.
Alisema wakati hayo
yakitokea mumewe aliyemtaja kwa jina la Cosmas Lusambo alikuwa amekwenda kulala
nyumbani kwa mke mdogo kwani ilikuwa zamu ya kwenda kulala huko kwa usiku huo
lakini baada ya kusikia mayowe ya kuomba msaada alikwenda kuungana na familia
yake na kumpeleka mtoto kituo cha afya cha Kamsamba kwani ndicho kilichopo
jirani na kijiji chao.
Akizungumza bada ya
kumtembelea mtoto Baraka katika wodi ya watoto kwenye hospitali ya rufaa kanda
ya Mbeya,Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Manyanya alioneshwa kusikitishwa na
tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi ili wahusika wapatikane na kuchukuliwa
hatua.
“Ni tukio ambalo
kwakweli linasikitisha mno.Nchi yetu inazidi kuendeleza vitendo vya aibu kwa
kuwafanyia ukatili wa kinyama albino kwa ujinga wa watu wachache wanaowadanganya
watu kuwa viungo vyao ni bahati ya kuleta utajiri” alisema
Mhandisi Manyanya
ambaye pia aliongoza sara fupi ya kuwaombea albino hospitalini hapo alionesha
pia kusikitishwa na mwenendo wa mashitaka ya watu waliofanya ukatili dhidi ya
albino akisema mahakama zimekuwa na milolongo mirefu inayokatisha tama wadau wa
kupinga ukatili huo.
Alitolea mfano kwa
tukio lililotokea mwaka juzi ambapo
mkazi wa kijiji cha Miangalua wilayani Sumbawanga Mary Chambanenge alikatwa
mkono na baadaye wahusika walikamatwa lakini hadi leo hukumu haijatolewa.
Alihoji kwa nini
mahakama iendelee kutoa visingizio vya kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha
ilikhali wahusika walikwenda kuonesha mahali walikokuwa wameufukia mkono
uliokatwa.
Mkuu huyo wa mkoa
alishauri pia kuangaliwa upya kwa sheria inayohusu masuala ya hukumu za kifo
akisema ikibidi inapaswa kubadilishwa ili iweze kutoa haki kwa watu wanaofanya
ukatili dhidi ya wenzao.
Alisema sheria ya sasa
kumtaka rais pekee kuwa mtu wa mwisho kutoa uamuzi kunyongwa kwa mtu aliyehukumiwa
inakosa nguvu ya kutekelezwa kutokana na majukumu mengi aliyonayo na kushauri
kuwa ni vyema vyombo vya sheria vipewe mamlaka ya mwisho ya kutekeleza adhabu
hiyo.
Kwa upande wake Kandoro
alisisitiza jamii kuendelea kushirikia katika ulinzi wa albino badala ya
kuviachia vyombo vya sheria pekee huku pia akivitaka vyombo vya habari
kuendelea kutoa elimu badala ya kuishia kuripoti matukio yanapotokea.
Aliwataka pia wakazi
mkoani Mbeya kutobweteka kwakuwa matukio kama hayo hayajatokea,badala yake wachukue
tahadhari na kuongeza ushirikiano wa ulinzi na pale wanapokuwa na shaka juu ya
uwepo wa watu flani kwenye maeneo yao watoe taarifa.
No comments:
Post a Comment