KATIBU wa Bodaboda mkoa wa Mbeya, MSUMBA MDESA, akitoa tamko kwa niaba ya waendesha Boda boda mkoa wa Mbeya.
HABARI KAMILI
WAKATI zoezi la kubadili namba
za pikipiki kutoka T kwenda MC likitarajiwa kufika kikomo Machi 31, Mwaka huu,
Madereva na wamiliki Mkoa wa Mbeya wametangaza mgomo wa kuendelea na zoezi hilo
kwa madai kuwa wanatozwa gharama kubwa tofauti na ambazo zilitangazwa na
Serikali.
Wakizungumza wakati wakitoa
tamko kwa vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa
Coffee Garden uliopo jijini Mbeya na kuhudhuriwa na viongozi wa Bodaboda kutoka
Wilaya nane za Mkoa wa Mbeya walisema hawatakuwa tayari kuendelea na zoezi hilo
hadi serikali itakapolitafutia ufumbuzi.
Akisoma tamko hilo, Mwenyekiti
wa Umoja wa Bodaboda Mbeya, Vicent Mwashoma, alisema Serikali ilitangaza kuanza
kubadili namba za pikipiki na bajaji ili kuzitofautisha na magari kwa gharama
ya shilingi 10,000 na kutoa miaezi sita ya kufanya zoezi hilo ikiwa ni kuanzia
mwezi Oktoba mwaka jana hadi Machi Mwaka huu.
Mwashoma alisema lakini wakati
zoezi hilo likiendelea wakaanza kukutana na vikwazo kutoka Mamlaka ya
Mapato(TRA) na kujikuta gharama zinakuwa kubwa tofauti na ile iliyotangazwa na
Serikali ambapo mtu mmoja hulipishwa hadi shilingi 550,000 na kima cha chini
kufikia 120,000.
Alisema kutokana na kuongezeka
kwa gharama hizo kinyume na tangazo la Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha
aliyotangaza bungeni wakaona ni vema kuomba ufafanuzi kutoka kwenye uongozi wa
Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Mbeya katika mkutano uliofanyika Februari 26,
mwaka huu.
Alisema katika Mkutano huo
Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya aliwafafanulia kuwa gharama hizo zinatokana na
malipo ya usajili kuwa 10,000 kama ilivyopangwa lakini mwenye pikipiki anapaswa
kulipia kibaocha kubandikia namba shilingi 19,000, ada ya zima moto shilingi
10,000 na kodi ya kubadili jina la umiliki(Transfer tax) shilingi 50,000.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa
Wanachama wa boda boda Mbeya wako tayari kubadili namba za pikipiki zao kwa
gharama ya shilingi 10,000 na si vinginevyo kutokana na kuwa na mlundikano wa
ushuru anaopaswa kulipia kwa mwaka.
Alifafanua kuwa kwa Mwaka
pikipiki moja kwa mwaka hulipiwa kati ya Shilingi 154000 hadi 204000 ambazo
zinatokana na ushuru wa maegesho shilingi 72,000, Leseni ya Sumatra shilingi
22000,Ada ya zimamoto shilingi 10000 na Bima kati ya Shilingi 50,000 hadi
100,000.
Baadhi ya Wanachama wa Bodaboda
waliohudhuria Mkutano huo wakiwa na mabango mbali mbali walisema Serikali
ilikuwa na mpango mzuri wa kuongeza ajira kwa vijana kwa kuruhusu uendeshaji wa boda boda lakini
jambo hilo linaonekana kuanza kuvurugwa na kupelekea vijana wengi kuachana na
biashara hiyo.
Madereva hao ambao majina yao
hayakupatikana haraka walisema awali kabla ya kuanza kuendesha bodaboda vijana
wengi ndiyo walikuwa wakijihusisha na upigaji wa nondo na uhalifu mkoani Mbeya
hivyo kitendo cha kuanza kuwanyanyasa tena kinaweza kurudisha hali hiyo kama
ilivyokuwa awali.
No comments:
Post a Comment