WAZIRI wa Ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi
Willium Lukuvi amewakabidhi mikononi mwa Tasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU) maafisa wawili wa Idara ya Ardhi
wa halmashauri ya jiji la Mbeya na mmoja kutoka ofisi ya wizara yake wanaokabiliwa
na tuhuma za kujimilikisha viwanja 25 kinyume cha sheria.
Agizo la Lukuvi limekwenda mbali zaidi kwa
kuwasimamisha kazi maafisa hao ili kupisha uchunguzi dhidi yao,uchunguzi ambao
pia utahusisha tuhuma zinazowahusu za kubadili matumizi ya Eneo la viwanja la
viwanda la Iyunga jijini hapa na kuwauzia wateja kama viwanja vya makazi.
Lukuvi
ametoa agizo la kukamatwa kwa maafisa hao jana Agosti 5 ambapo
amewataja kuwa ni pamoja na afisa ardhi mwandamizi wa jiji la Mbeya
Ntala Castor na msaidizi wake James Venant Francis huku akimtaja kwa
jina moja
la Mwandoloma afisa ardhi aliyekuwa kwenye halmashauri hiyo kabla ya
kuhamishiwa wizarani.
Waziri huyo amesema uchunguzi unaonesha maafisa hao
walitumia vibaya mazoezi ya ugawaji wa viwanja vilivyopimwa kwenye maeneo ya
Iwambi na Itezi kujinufaisha kwa kujigawia wenyewe viwanja vingi ambapo kati
yao wapo waliojimilikisha zaidi ya viwanja kumi.
Amesema hesabu ya viwanja 25 walivyojigawia maafisa
hao watatu ni vile tu vilivyoandikwa majina yao lakini zipo tetesi kuwa vipo
viwanja vingine ambavyo ni vya kwao lakini walitumia ujanja wa kubadili
majina.
Lukuvi amesema kwa ujumla maafisa ardhi wengi nchini
wamekuwa wakiisababishia lawama serikali kwa wananchi kutokana na wengi wao
kuwa na utendajikazi wenye kuendana na tama ya kujilimbikizia mali jambo ambalo
limekuwa likiwasababishia wananchi adha kubwa.
Amesema suala la maafisa kujigeuza madalali wa
kujimilikisha viwanja na kisha kuviuza viwanja hivyo kwa wateja kwa bei za juu
halikubaliki na wanaobainika kama maafisa hawa wa jijini Mbeya watapewa adhabu
ili kuwa mfano kwa wenzao.
No comments:
Post a Comment