KATIKA kuonesha kinachopiganiwa si kuwatumikia wananchi bali maslahi
binafsi,aliyekuwa mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)
Modestus Kilufi amejikuta anakuwa mwanachama wa vyama vitatu tofauti katika
kipindi cha wiki moja akitafuta nafasi ya kutetea nafasi ya ubunge.
Safari ya kuhama kwa Kilufi ilianzia katika viwanja
vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya ambapo mbunge huyo aliyemaliza muda wake
aliutumia mkutano wa mgombea wa urais kupitia Chadema Edward Lowasa kutangaza
kuhama rasmi CCM na kuhamia chama hicho baada ya kushindwa katika kura za
maoni.
Hata hivyo makazi ya Kilufi ndani ya Chadema
yakashindikana kuwa ya kudumu kwani pamoja na ushawishi wote alioufanya kwa
uongozi ndani ya chama hicho katika ngazi za Taifa mkoa na wilaya alijikuta
anagonga mwamba baada ya wafuasi wa chama hicho kumzuia kuingia ofisi ya
msimamizi wa uchaguzi alipokwenda kuchukua fomu.
Taarifa kutoka Mbarali zinaeleza kuwa juzi kunako
majira ya jioni(Agosti 20) wanachama wa Chadema walimzuia Kilufi kuingia kwenye
ofisi za msimamizi kwakuwa walitaka nafasi hiyo ibakie kwa mgombea Liberatus
Mwang’ombe ambaye tayari alikuwa amekwishachukua fomu baada ya kushinda kwenye
kura za maoni ndani ya chama ambako Kilufi hakushiriki.
Baada ya kushawishiwa na kundi la wafuasi wake jana(Agosti
21) Kilufi aliiona Chadema si pahala sahihi tena na akajikuta anaangukia
mikononi mwa chama cha ACT Wazalendo na majira ya saa nane mchana alikwenda kuchukua
fomu ya kugombea kupitia chama hicho.
Akiwasiliana kwa njia ya simu na mwandishi wa habari
hizi,msimamizi wa uchaguzi jimbo la Mbarali Adam Mgoi alithibitisha Kilufi kuwa
miongoni mwa wagombea nane waliochukua fomu kugombea ubunge na kubainisha kuwa
amechukua kupitia chama cha ACT Wazalendo.
Akizungumzia kuhama kwa mwanachama aliyedumu naye
kwa takribani siku sita,mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mbeya Josef Mwachembe
China alisema anamuona Kilufi kama msaliti anayeendeshwa na msukumo wa watu
wachache.
China alisema Kilufi ni miongoni mwa wanasiasa wasio
na msimamo na wasio wazalendo kwa taifa lao na ndiyo sababu anapigania maslahi
yake binafsi badala ya maslahi ya watanzania wanyonge.
Mwenyekiti huyo ambaye juzi alionekana kutwa nzima
wakiwa na Kilufi katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mbeya wakifanya mikakati ya
mapinduzi ya mgombea wa ubunge Mbarali kupitia Chadema alikana uongozi
kununuliwa na mbunge huyo ili ushinikize kumkabidhi nafasi ya kupeperusha bendera
ya chama kwenye uchaguzi.
Hata hivyo China alikiri kuwa maagizo ya chama
kumpokea Kilufi yalitokea ngazi ya juu yaani makao na kamwe haikuwa ridhaa ya
wanachadema wilaya wala mkoa na ndiyo sababu hata uongozi wa Chadema ngazi ya
kanda haukuwa na taarifa.
Hata hivyo ujio ndani ya ACT ulionekana kuleta
mkanganyiko kwa uongozi ngazi ya wilaya kwani ulipopigiwa simu ulionekana
kugawanyika ambapo Mwenyekiti Anzuruni Rashid Anzuruni alisema anachojua ni
kuwa mtu aliyechukua fomu kupitia chama hicho ni James Kamanga na Kilufi
hamtambui huku katibu wake Erasto Sanga alithibitisha kumpokea Kilufi na
kutengua uteuzi wa mgombea wa kwanza.
No comments:
Post a Comment