UHABA wa wataalamu wa Afya wilayani
Mbozi mkoani Songwe umesababisha wakazi wa kijiji cha Itepula kata ya Igamba
wilayani hapa kukosa huduma za matibabu kwa miezi mitatu sasa kufuatia Muuguzi
katika Zahanati ya kijiji chao kwenda likizo ya Uzazi.
Wakazi wa kijiji cha Itepula
walibainisha hayo kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika kijijini hapo
ukiwakutanisha na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi walioongozwa na
mwenyekiti wao Eliki Ambakisye.
Mmoja wa wakazi hao Sikudhani
Mkondya alisema suala la kufungwa kwa Zahanati kutokana na kukosekana muuguzi
limekuwa kero kwao kwasababu miezi mitatu imepita sasa na wanalazimika kutembea
umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika vijiji vingine.
Mkondya pia alisema kufuatia
kukosekana kwa mtaalamu kijijini hapo baadhi ya wakazi wanalazimika kutumia
dawa pasipo ushauri wa kitabibu hivyo kubaki wakimeza dawa kwa kukisia hata
kama hawajui ugonjwa unaowasumbua.
Alisema hali imekuwa mbaya zaidi
kwakuwa hata wanapokwenda katika zahanati iliyopo kijiji cha jirani cha Igamba
wanafukuzwa na wataalamu wa zahanati hiyo wakiwataka warudi kutpata matibabu
katika zahanati ya kijiji chao
“Inatulazimu kwenda kununua dawa
katika maduka yaliyopo pasipo kujua tunaumwa nini kwani hakuna vipimo.Tunaamini
tunahatarisha maisha yetu kwa kutumia dawa pasipo kujua magonjwa yanayotusumbua
,lakini tutafanya nini nasi hatuna njia mbadala.”alisema Mkondya.
Afisa mtendaji wa kijiji cha
Itepula, Timothy Msukwa alikiri zahanati ya kijiji hicho kufungwa tangu January
mwaka huu hivyo wananchi kuhangaika kupata matibabu kwani walizoea kupata
huduma jirani.
Msukwa alisema chanzo cha kufungwa
kwa zahanati hiyo ni baada ya muuguzi aliyekuwa anatoa huduma katika zahanati
hiyo kwenda likizo lakini akabainisha kuwa tayari wamempata muuguzi mwingine
ambaye tayari ameripoti lakini hajaanza kufanya kazi.
Kwaupande wake mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye aliagiza zahanati kufunguliwa
mara moja huku akimtaka muuguzi aliyepangiwa kituo hicho kufika mara moja na
kuanza kazi ili kutoa hudumia wananchi.
Mwenyekiti huyo alisema ipo haja
kwa serikali kutafuta uwezekano wa kuongeza wataalamu ili kuendana na dhana ya
wanyonge kupata matibabu jirani kwakuwa
walijitoa kujenga zahanati hiyo kwa lengo la kujinasua na adha ya kusafiri
umbali mrefu kufuata matibabu.
No comments:
Post a Comment