Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, April 27, 2014

WAWILI AKIWEMO MWANAFUNZI WAHOFIWA KUFA MTO KIWIRA

WATU wawili akiwamo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mwigo ya wilayani Kyela mkoani Mbeya wanahofiwa kufa maji katika Mto Kiwira. Hofu ya kufa maji watu hao inakuja baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kusafiri mtoni humo wakitokea kijiji cha Ibungu kwenda kitongoji cha Ndandalo kilichopo Kyela kati kupitia mto Kiwira uliojaa maji kutokana na mvua nyingi zilizoinyesha ukanda wa juu na kusababisha mafuriko katika mto huo. Hofu ya vifo hivyo vya watu wawili inaweza kufikisha idadi ya watu waliopoteza maisha tangu kutokea kwa mafuriko ya kihistoria wilayani hapa kufikia saba. Akizungumza na waandishi wa habari juzi mara baada ya kutokea ajari hiyo Mwenyekiti wa kitongoji cha Ndandalo Rameck Mbembela maarufu kwa jina la Mwinama alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 10.30 jioni baada ya watu watano kupanda katika mtumbwi mmoja wakivuka kutoka kijiji cha Ibungu kwenda Kyela mjini. Mwenyekiti huyo alisema kuwa wakiwa katikati ya mto huo mtumbwi uliyumba kutokana na udogo wake ikilinganishwa na uwingi wa maji yaliyokuwa pia na kasi kubwa na ndipo watu hao walipotumbukia mtoni na kuwa katika harakati za kujiokoa watu watatu akiwemo mwongozaji walifanikiwa kujiokoa na kushindwa kuwaokoa wenzao ambao wanadaiwa hawakujua kuogelea. Mbembela aliwataja watu hao waliozama kuwa ni Mzee Akupenda (70) mkazi wa kijiji cha Ibungu na kijana Stevin Stivin (15)mkazi wa Kyela aliyekuwa anasoma kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Mwigo aliyepata kadhia hiyo alipokuwa anavuka mto kwenda kumsalimia shangazi yake anayeishi kitongoji cha Kyela kati kilichopo ng’ambo ya mto huo. Aliongeza kuwa juhudi za kuitafuta miili ya watu hao bado zinaendelea na kwamba aliwataka wananchi wanaotumia njia hiyo ya mitumbwi waache na badara yake watumie njia kuu ambayo lipo daraja kubwa la kijiji cha Ipyana hadi pale serikali itakapo jenga daraja ili kunusuru madhara makubwa yasitokee. Alisema kuwa katika sehemu hiyo ya kivuko lilikuwepo daraja dogo (kityepu tyepu)ambalo lilibomolewa na serikali baada ya kuonekana kuwa ni hatarishi kwa wananchi waliokuwa wakivuka kwa kutumia daraja hilo na kufanya zoezi la kuvuka kuwa gumu hasa kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule zilizopo nga”ambo ya mto huo. Mbembela aliitaka serikali kupitia halmashauri ya wilaya kuliangali kwa jicho la tatu tatizo hilo hasa kufanya haraka kujenga daraja katika mto huo ambao hutumiwa na watu wengi ambao hufuata huduma za msingi Kyela mjini na wengine hufuata huduma nga”mbo ya pili hasa wanafunzi,wakulima pamoja na wafanyabiashara hivyo kutokuwepo kwa daraja ni tatizo kubwa ambalo hupunguza uchumi kwa wananchi na serikali kwa ujumla. Mwenyekiti huyo pia aliitaka Serikali wilayani humo kufanya tathimi ya uhakika ya maafa yaliyotokea kwa wilaya mzima bila kufanya ubaguzi wowote na si kukimbilia vijijini pekee na kwamba katika kata ya Kyela kati maafa ni makubwa kwa upande wa kitongoji cha Ndandalo pekee kinawahanga 26 waliobomokewa na nyumba zao akiwemo mwenyekiti kufuatia mvua hizo za mafuriko zilizotokea. Aidha Mwenyekiti huyo aliwaasa wanasiasa kuacha kutumia maafa haya kama mtaji wa kisiasa kwao na badara yake watoe misaada ya hali na mali kwa wahanga na kuwa wafanye jitihada za kuboresha miundombinu ya kujenga mifereji itakayotiririsha maji kwenye mito ili kujaribu kunusuru uharibifu wa barabara uliopo wilayani humo.

No comments:

Post a Comment