Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, December 17, 2017

ILOMBA STAR YAICHAPA JAJOJO FC 5-4



TIMU ya Soka ya Ilomba Star imeinyuka timu ya Jajojo FC goli 5-4 katika mchezo uliochezwa jumapili kwenye viwanja vya Ruandanzovwe jijini Mbeya ikiwa ni Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu mkoani hapa.

Ilomba Star inashiriki ligi ya Mkoa wa Mbeya hatua ya sita bora wakati Jajojo FC wanashiriki ligi daraja la nne Mbeya mjini.

Katika Mchezo wa juzi hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika hakuna timu iliyofanikiwa kupata goli hatua iliyolazimu kuingia katika penati ambapo Ilomba Star walifanikiwa kutingisha nayavu kwa mikwaju yote mitano lakini Jajojo wakapata mikwaju mine na kukosa mmoja.

Kufuatia ushindi huo,Ilomba Star walijinyakulia shilingi 150,000 huku Jajojo wakizawadiwa Shilingi 100,000 kutoka kwa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo iliyoundwa na wajumbe kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuri), Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma na Mdhibiti na Ukaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG).

Awali Afisa Maadili mkuu Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma mkoa wa Mbeya,Anthony Pallangyo alisema lengo la mchezo huo ni kuwashirikisha vijana katika mikakati ya kujenga maadili ndani ya umma.

“Ninyi kama vijana mna nguvu na mnategemewa ndani ya jamii iwapo ninyi mkitambua umuhimu wa kuzingatia maadili na kukataa rushwa mtakuwa mabalozi wazuri kwa jamii inayowazunguka na kwa pamoja tutaweza kutokomeza matatizo haya”alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mbeya,Emmanuel Kayabo aliwataka vijana kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo akisema milango iko wazi kwa mtu yeyote aliye na malalamiko juu ya rushwa au viashiria vyake.

No comments:

Post a Comment