Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, December 17, 2017

MAKALA ATIMIZA AHADI YA MABATI,SARUJI KATA ZA MWASANGA NA IDUDA

 Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akikabidhi msaada wa Mabati 154 kwa viongozi wa kata kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la zahanati inayojengwa kwa ushirikiano wa wananchi wa kata za Tembela na Mwansanga




 Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akikabidhi mifuko 100 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha afya cha kata ya Iduda jijini Mbeya.

MKUU wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla amevitaka vijiji na kata mkoani hapa kuingia katika shindano la kuanzisha Ujenzi wa Zahanati na vituo vya Afya ili Serikali ya mkoa iweze kumalizia ujenzi huo.

Makalla alitangaza Shindano hilo,jana alipotimiza ahadi ya kuchangia Bati 154 kwaajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati inayojengwa kwa ushirikiano wa wakazi wa Kata za Tembela na Mwasanga na pia Mifuko 100 ya Saruji kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Kata ya Iduda jijini Mbeya.

Makalla alisema hilo ni shindano alilolianzisha lengo likiwa ni kutoa msukumo kwa vijiji na kata zote mkoani hapa kuitikia wito wa kutekeleza mpango wa kila kijiji kuwa na zahanati na kila kata kituo cha afya.

“Nijaribuni kwa kuanzisha ujenzi muone kama sintomalizia,nitapeleka kote mabati na saruji kwaajili ya kumalizia ujenzi kwa wananchi watakaoanzisha.Inawezekana kabisa wapo wadau wana utayari wa kutusaidia vifaa”

“Lakini sintotaka kusikia bati ninazotoa zimepotea au kuibwa,sintotaka kusikia saruji ninayotoa imeibiwa au imeganda.Nikitoa kitu kifanye kazi tumalize ujenzi wananchi waache kupata shida ya matibabu”alisisitiza Makalla.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ni jambo lisilowezekana wadau kuendelea kutamka Sera ya hapa kazi tu wakati wananchi wanaumwa au wanapoteza muda mwingi kutembea wakifuata huduma za matibabu.

Alisema iwapo mpango wa ujenzi wa zahanati na vituo vya afya utaendelea kuachiwa Halmashauri itachukua miaka mingi kukamilisha kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbeya,Paul Ntinika aliahidi kuanza kutekeleza Shindano la ujenzi wa zahanati na vituo vya afya wilayani kwake mara moja akisema hiyo ni fursa ya kipekee isiyopaswa kuipoteza.

No comments:

Post a Comment