Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, December 19, 2017

MAHAFALI YA 16 CHUO KIKUU MZUMBE YALIVYOFANA

Afisa Mauzo wa Kampuni ya Tanzania Standard Newepaper (TSN)  Kanda ya Nyanda za juu kusini,Dickson Ishengoma(kulia) na wenzake wakifurahi pamoja baada ya kuhitimu Shahada ya Umahiri katika uendeshaji uongozaji wa Mashirika katika Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Mbeya yaliyofanyika jijini Mbeya.


UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya umesema bado una nia ya kukipanua zaidi chuo hicho ili kiweze kukidhi mahitaji ya wakazi wa Nyanda za juu kusini na pia nchi jirani za Zambia,Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


Mwenyekiti wa Baraza la Chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya, Prof Mathew Luhanga alibainisha hayo kwenye mahafali ya 16 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Mbeya.

Prof Luhanga alisema bado chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa miundombinu hususani kumbi za mihadhara,majengo ya madarasa,nyumba za watumishi na pia Hosteli.

Alisema jitihada zinazofanywa na chuo kwa kushirikiana na wadau ili kutatua changamoto hizo ndizo zitawezesha chuo kupata hadhi ya kuwatumikia wahitaji kwa kiwango kinachohitajika.

Aliipongeza Uongozi wa Serikali Kuu,Serikali ya mkoa wa Mbeya na Halmashauri ya jiji akisema umekuwa ukishirikiana kwa karibu na uongozi wa chuo katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zilizopo.

“Serikali imetusimamia kupata mkopo wa zaidi ya  bilioni moja lakini pia yenyewe katika mwaka huu wa fedha imetenga bajeti ya shilingi bilioni moja ili kutusaidia katika ujenzi wa jengo la utawala” alisema Prof Luhanga.

Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo hicho Prof Lugano Kusiluka alisema Chuo pia kinatarajia kuongeza udahili wa wanafunzi sambamba na kuongeza programu zaidi ya 11 zinazotolewa hivi sasa katika tawi hilo.

Kwa mujibu wa Prof Kusiluka katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 734 walihitimu katika ngazi za Astashahada,stashahada na Shahada kati yao wanawake wakiongoza kwa asilimia 50.1 na wanaume asilimia 49.9.

Mmoja wa wahitimu,Afisa Mauzo wa Kampuni ya Tanzania Standard Newepaper (TSN)  Kanda ya Nyanda za juu kusini,Dickson Ishengoma aliahidi kuitumia taaluma aliyoipata kwa weledi na kwa manufaa ya Taifa hususani wakati huu wa kuelekea uchumi wa viwanda.

Ishengoma aliyehitimu Shahada ya Umahiri katika Biashara na uendeshaji wa Makampuni aliwasihi wahitimu wenzake kutobweteka na badala yake kufikiri ni kwa jinsi gani wanaweza kuisaidia Serikali kufikia hatua ya uchumi wa viwanda.

No comments:

Post a Comment