Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, May 20, 2017

SERIKALI YAWAHURUMIA WAKAZI WA YALA WILAYANI MBARALI

 Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akizungumza na wakazi wa kijiji cha Yala

SERIKALI Mkoani Mbeya imeafikiana na Kikosikazi cha kitaifa cha kutathmini  Ikolojia ya Mto Ruaha kuwaruhusu kwa muda wakazi wa kijiji cha Yala kilichopo katika kata ya Luhanga wilayani Mbarali kutumia maji yanayotoa katika shamba la mwekezaji la Kapunga Rice Project ili kunusuru mazao yaliyopo mashambani.

Hivi karibuni Kikosikazi cha kitaifa cha kutathmini  Ikolojia ya Mto Ruaha kilichoundwa na Makamu wa Rais,Samia Suluhu iliipiga marufuku matumizi ya maji yanayochepushwa kiholela na hivyo kumtoza faini ya shilingi milioni 50 kampuni ya Kapunga Rice project.

Uongozi wa Kampuni hiyo,unasema changamoto ya uchepushaji wa maji yanayotakiwa kurejeshwa katika mto Ruaha inatokana na wizi wa maji unaofanywa na wakazi wa vijiji jirani pasipo ridhaa ya uongozi wa kampuni.

Hata hivyo kutokana na agizo la Kikosi kazi,wakazi wa kijiji cha Yala walikuwa hatarini zaidi kwani wasingeweza kuvuma chochote baada ya mazao yao mashambani kuanza kuharibika kutokana na ukame kwani maji pekee waliyokuwa wakiyategermea ni yale waliyokuwa wakiyachepusha baada ya kutumika katika shamba la mwekezaji.

Akizungumza katika mkutano wa Hadhara uliofanyika kijijini Yala juzi,Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla alisema ili kunusuru mazao ya wakazi wa kijiji hicho yaliyokwishaanza kunyauka kwa kukosa maji,wamufanya mazungumzo na kukubaliana na kikosi kazi kuwaruhusu waendelee kuyatumia kwa muda maji hayo.

“Baada ya kupokea malalamiko ya wananchi ilinibidi nizungumze na Kikosi kazi ili tuone kipi kinaweza kufanyika.Tumefikia makubaliano ya busara kuwa kwakuwa mnahitaji maji kwa muda mfupi ili mazao yaliyopo shambani yakomae basi endeleeni kutumia maji yale”

“Lakini msifikiri huu utakuwa utaratibu wa siku zote,hii ni huruma kwakuwa vinginevyo hapa siku ya siku mngekuja kuiomba serikali chakula cha msaada.Mtambue kuwa Katazo la kutochepusha maji lipo kisheria na si amri ya mwekezaji kama wengi mnavyomsema vibaya.Kabla ya msimu mwingine wa kilimo tutakuwa tumewapa utaratibu mwingine wa namna ya kupata maji kwaajili ya kilimo” alisema Makalla.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho Emanuel Mtakasa na Juma Mwashikamile waliishukuru serikali kwa uamuzi huo,huku wakisema pasipo msaada huo wa maji kutoka shamba la Kapunga hakuna mwanakijiji yeyote ambaye angevuna mpunga mwaka huu.

No comments:

Post a Comment