Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, May 23, 2017

UWEZESHAJI MDOGO WA MAAFISA USHIRIKA CHANZO CHA KUDOROLA VYAMA VYA USHIRIKA

UWEZESHAJI mdogo unaofanywa na Halmashauri kwa Ofisi za Maafisa Ushirika umetajwa kuwa chanzo cha Migogoro mingi ya kiutendaji ndani ya Vyama mbalimbali vya ushirika nchini.

Hayo yamebainishwa na Menejimenti na wajumbe wa Bodi ya Chama kikuu cha Ushirika cha wakulima wa Tumbaku Wilayani Chunya(CHUTCU) waliohudhuria Semina ya Programu ya kuwajengea uwezo wa Kitaasisi kwa viongozi na wadau wa ushirika ikiwa ni mwendelezo wa utoaji mafunzo hayo kwa wadau wa zao la Tumbaku.

Meneja mkuu wa CHUTCU,Bakari Kasia alisema vyama vingi vya ushirika vinaingia kwenye migogoro kutokana na usimamizi legelege wa Maafisa Ushirika ambao wengi wamekuwa wakijitokeza pale migogoro inapokuwa mikubwa.

Alisema wengi wa maafisa Uhirika wamekuwa kama watu wanaosubiri mambo yaharibike na kasha wao kuja kuwakamata na kuwaweka mahabusu viongozi jambo linalokinzana na wajibu wa nafasi zao wa kutembelea vyama hivyo  mara kwa mara ili kujua mwenendo mzima wa kiutendaji.

“Tunatambua Maafisa hawa si wakaguzi lakini wanapaswa kuvitembelea vyama hivi mara kwa mara ili panapoonekana kuwepo na dalili za mgogoro basi uthibiti wa haraka ufanyike kabla mambo hayajawa makubwa.Lakini kwa sasa wamebaki kusubiri palipo na mgogoro mkubwa ndipo wanaonekana kuja na kuwakamata viongozi na kuwaweka ndani.Siku zote wasimamizi wakiwa legelege vyama navyo vitakuwa legelege” alisema Kasia.

Hata hivyo Kasia alisema utekelezaji huo legelege wa Maafisa Ushirika unatokana na Halmashauri zao kutowawezesha ipasavyo ili kuvifikia vyama vilivyopo kwenye maeneo yao na hivyo kuwasababishia wabaki ofisini wakiwa hawana kazi za kufanya.

Alisema jambo la kushangaza ni kuwa Waajiri wa maafisa hao wasiowapa hata pikipiki za kutembelea ili kuwafikia wateja kwa urahisi,inapotokea migogoro mikubwa kwenye vyama wamekuwa wakiwaagiza kwa ukali kwenda kufuatilia na ufuatiliaji wenyewe unakuwa wa kamata kamata.

Kwa upande wake Kaimu Mrajisi msaidizi wa mkoa wa Songwe ambao pia una vyama wanachama wa CHUTCU kupitia wakulima wa Tumbaku waliuopo wilayani Songwe,Marton Mtindwa alikiri Ofisi nyingi za Maafisa Ushirika kuwa katika hali ngumu kutokana na Halmashauri zao kutotenga bajeti kwaajili ya utekelezaji majukumu yao.

Mtindwa alisema Halmashauri zinazotoa kipaumbele na kutenga bajeti kwaajili ya maafisa ushirika ni zile tu ambazo zinaona kuna mafanikio makubwa yaliyokwisha patikana kupitia vyama vya ushirika vilivyopo na hasa zile zilizopo kwenye maeneo ya kilimo cha mazao makubwa ya biashara kama Tumbaku na Kahawa.

“Kinachopaswa kufanyika kwa Afisa ushirika anaeona halmashauri haimpi kipaumbele kumtengea bajeti ni yeye mwenyewe kujiongeza.Kama ni kuandaa maandiko na kutafuta fedha sehemu yoyote ikiwemo kwa wadau ni yeye kama ni kumshawishi mwajili kwa kutengeneza hoja zenye mvuto ni yeye.Hata sisi warajisi wasaidizi tunalazimika kufanya hivyo” alisema Mtindwa.

Akifungua Semina hiyo ya siku Mbili,Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini Titto Haule kwa mikoa ya Mbeya na Songwe ni wilaya Mbili pekee za Chunya na Songwe ambazo vyama vya Ushirika walau vinaonekana kuwa na Ustawi mzuri lakini wilaya nyingine zote zinazosalia hali si nzuri na inahitajika jitihada za dhati na za ushirikiano wa pamoja kujenga Ushirika.

Haule alisema mpango wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini ni kuona unafanyika Uhakiki wa vyama vya ushirika vilivyo hai nchini ili kuweka mikakati ya kufufua vilivyo kufa na pia kuanzisha vingine vipya lakini sasa vyama vyote vikiwa katika mtazamo wenye kuleta maendeleo kwa wananchi na si wajanja wachache.

No comments:

Post a Comment