Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, May 23, 2017

UMITASHUMITA ILIVYONOGA KATIKA KATA YA IGALE

Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Idd Omary akikabidhi mipira mitano kwa Mratibu Elimu Kata ya Igale,Ezekia Masebo kwaajili ya Mashindano ya Michezo ya wanafunzi wa Shule za msingi(Umitashumita) kwenye hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo katika ngazi ya kata jana
 Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Idd Omary akizindua kwa kupiga penati Mashindano ya Michezo ya wanafunzi wa Shule za msingi(Umitashumita) ngazi ya kata ya Igale 


Mratibu Elimu Kata ya Igale,Ezekia Masebo akizungumza jambo kabla ya kuzinduliwa kwa mashindano

Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Michezo ya wanafunzi wa Shule za msingi(Umitashumita) kata ya Igale,Mwalimu Atupakisye Jabir.

Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Idd Omary akizungumza na wanafunzi,walimu na wazazi waliofika kushuhudia michezo mbalimbali.



 Afisa biashara wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Yusuf Ahmed Juma akizungumza jambo na kuahidi kuzitembelea shule zote kuzungumza na walimu na wanafunzi juu ya umuhimu wa kuhifadhi fedha benki badala ya kuweka kwenye kibubu. 




MIUNDOMBINU duni na ukosefu wa vifaa vya michezo katika Shule mbalimbali wilayani Mbeya imetajwa kuwa changamoto inayokwamisha jitihada za kuendeleza sekta ya michezo mashuleni.

Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Michezo ya wanafunzi wa Shule za msingi(Umitashumita) kata ya Igale,Mwalimu Atupakisye Jabir alibainisha hayo alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya michezo mashuleni kwenye uzinduzi wa mashindano hayo jana.

Mwalimu jabiri alisema miundombinu ya michezo ni duni na iliyopo haiko katika hali nzuri huku akisema pia vifaa vya michezo kama mipira,sare,nyavu,filimbi,saa za michezo na ngoma havitoshelezi.

Alisema pia kutokana na ukosefu wa usafiri kwaajili ya shughuli za michezo mashuleni,walimu na wanafunzi wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwa miguu pale yanapoandaliwa mashindano au michezo ya kirafiki kati ya shule moja na nyingine au shule za kata moja na nyingine.

“Zipo shule hata baadhi ya viwanja hakuna hasa vya netiboli,wavu na mpira wa mezani.Hata vimiko vya kupigia mpira wa mezani hatuna.Lakini kutokana na ukosefu wa bajeti kwaajili ya usafiri tunalazimika kutembea kwa miguu.Tunapokwenda kwenye mashindano ya tarafa au wilaya tunakosa nauli hata ya daladala kutoka kwenye kata yetu hadi yanakofanyika mashindano husika” alisema Mwalimu Jabiri.

Aliwasihi wadau mbalimbali kuona uwezekano wa kuzisaidia shule katika tasnia ya michezo kwakuwa mashuleni ndiko kuliko na msingi bora wa kuwapata wachezaji wazuri wanaoweza kuliwakilisha taifa katika mashindano mbalimbali kama inavyoonekana hivi sasa kwa timu ya Serengeti Boys ambayo sasa ni gumzo ndani nan je ya nchi.

Akifungua mashindano ya Umitashumita katika ngazi ya kata ya igale inayoshirikisha jumla ya shule tano za msingi,Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Usongwe lililopo Mbalizi Wilayani Mbeya,Idd Omary sambamba na kukabidhi msaada wa mipira mitano aliahidi kuendelea kushirikiana na shule zote wilayani hapa katika suala la michezo lengo likiwa ni kushiriki kuibua na kukuza vipaji vya michezo.

Omary alisema pamoja na faida nyinginezo lukuki za michezo,NMB inatambua kuwa nidhamu ya mtumishi yeyote kazini inatokana na msingi bora uliojengwa tangu angali mdogo hivyo kwa mwanafunzi kushiriki michezo ni sehemu ya kujifunza nidhamu bora.

“Michezo,taaluma na nidhamu vinakwenda pamoja hii ndiyo sababu mwisho wa siku hapa tutakuja kupata viongozi na watumishi na hata wachezaji wakubwa walio na nidhamu.Michezo ni sehemu muhimu sana kwa umri wenu.Wapo wazazi na walezi wasiotaka kutoa fursa kwa watoto kushiriki michezo,hii si sawa tuwape fursa watoto hawa” alisema Omary.

Aliwasihi wanafunzi kutoitumia fursa ya michezo kujiingiza katika masuala ya matumizi ya dawa za kulevya na ulevi kwakuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasababishia kutofikia malengo yako kimichezo na hata kitaaluma.

Kwa upande wake Afisa Elimu Utamaduni wilaya ya Mbeya,Ashanuru Malange alisisitiza umuhimu wa Michezo mashuleni akisema Mwili wenye Afya huleta Akili yenye afya na ili afya ipatikane ni lazima mwili husika ufanye mazoezi.

Shule zinazounda mashindano ya Umitashumita katika kata ya Igale yatakayotoa timu kwaajili ya kushiriki mashindano hayo kwenye ngazi ya wilaya ni pamoja na shule ya msingi Igale,Izumbwe I,Shongo,Itaga na Horongo.

No comments:

Post a Comment