Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, April 21, 2013

MKAZI wa kijiji cha Magamba wilayani Mbozi Elisha Zambi(27) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya akikabiliwa na tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu. Kijana Elisha anadaiwa kutumia nguvu kunyang’anya pikipiki aina ya T.Better yenye namba T 606 CCS yenye thamani ya shilingi milioni 1.7. Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki pikipiki hiyo ilikuwa mali ya Mbungu Kabeja(39) mkazi wa kijiji cha Lwati aliyekuwa akiitumia kusafirisha abiria maarufu kama bodaboda. Kaimu kamanda Masaki alisema jana majira ya saa tisa alasiri mtuhumiwa akiwa na mwenzake ambaye hakufahamika jina wala makazi yake walikodi bodaboda hiyo wakimtaka Kabeja kuwatoa kijijini Lwati na kuwapeleka kijiji cha Mlowo walikodai walitaka kwenda kupata matibabu hospitali. Kinyume na makubaliano wakiwa njiani wateja hao waliobebwa kwa mtindo maarufu wa Mshikaki uliopigwa marufuku na jeshi la polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani walimtaka dereva kusimama na kumtaka awaachie pikipiki yake. Mhanga wa tukio hilo alijitahidi kupambana na wanyang’anyi hao wawili kwa kupigana nao na ndipo alipofanikiwa kumdhibiti kijana Elisha lakini kwa bahati mbaya mtuhumiwa wa pili akafanikiwa ktoroka na pikipiki hiyo. Masaki alisema mtuhumiwa yuko mahabusu wakati uchunguzi wa kumtafuta mtuhumiwa aliyekimbia na pikipiki ukiendelea na kuhakikisha kuwa wakati wowote watuhumiwa wa tukio hilo watafikishwa mahakamani. Alitoa wito kwa raia wema walio na taarifa juu ya uwepo wa mtuhumiwa wa pili ama pikipiki inayosadikiwa kuwa ya wizi kutoa taarifa katika chombo chochote cha sheria kilichopo jirani huku akionya pia watu kutonunua pikipiki yoyote isiyo na vielelezo vya umiliki halali toka kwa muuzaji. Aliwataka pia madereva wa boda boda kutambua kuwa sheria ya kuzuia ubebaji wa abiria zaidi ya mmoja katika pikipiki moja inalenga kuwaweka salama wao hivyo wanapaswa kuizingatia.

No comments:

Post a Comment