Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, April 29, 2013

TUCTA YALALAMIKIA KATIBA YA SASA

Shirikisho la vyama vya wafanyakazi(TUCTA) mkoani Mbeya limesema kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi mwaka huu ya Katiba izingatie usawa na haki za wafanyakazi inatokana na mapungufu lukuki yaliyopo kwenye katiba ya sasa. Mwenyekiti wa (TUCTA) mkoani hapa Alinanuswe Mwakapala aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao kilichofanyika katika chuo cha wafanyakazi kilichopo Mwanjelwa jijini hapa. Mwakapala alisema zipo changamoto nyingi zinazomkabili mfanyakazi kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye katiba na ndiyo sababu ya kuitumia kaulimbiu hiyo ili iweze kuleta msukumo kwa taifa katika maandalizi ya katiba mpya. Kutothaminiwa kwa wafanyakazi kulitajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa na inayowafifisha moyo wananchi kuendelea kulitumikia taifa lao. Alisema kwa sasa wafanyabiashara wanaonekana kuwa na nguvu kwa serikali tofauti na wafanyakazi na ndiyo sababu wameendelea kuwa watu wa chini wanaonyonywa na wafanyabiashara. Mwakapala pia alisema kupitia sherehe za mei mosi wanataraji kufikisha kilio cha kuomba kupunguzwa kwa kiwango cha kodi kwa mfanyakazi kutoka asilimia 14 ya sasa hadi asilimia tano ya mshahara. Alisema pia watawasilisha ombi la kuomba kupandishwa kwa kiwango cha kima cha chini cha mshahara walau kufikia shilingi laki tano. Mwenyekiti huyo alisema mamombi hayo yanatokana na kupanda kwa gharama za maisha hususani nauli ambapo asilimia kubwa ya mshahara wa mfanyakazi kwa sasa unaishia kwa kugharamia nauli za kwenda na kutoka kazini hivyo kuishi maisha ya kuganga njaa.

No comments:

Post a Comment