UONGOZI wa chuo cha kilimo cha Nice
Dream kilichopo katika mtaa wa Mapelele kata ya Ilemi Jijini Mbeya umetokomea
kusikojulikana na kuwaacha wanafunzi 48 wakiwa hawajui la kufanya wakiwa wametozwa
jumla ya shilingi milioni 26 walizotoa kwaajili ya ada ya masomo chuoni hapo.
Kutokana na kukimbiwa na uongozi wa
chuo na wanafunzi kubaki peke yao chuoni hapo,wanafunzi wamejikuta katika
wakati mgumu kwani sasa licha ya kutojua nini hatma ya maisha yao sula la
kukosekana kwa chakula ni changamoto nyingine inayowaweka kwenye mazingira
magumu zaidi.
Wakati Lyamba Lya Mfipa ikifika
chuoni hapo jana,wapo baadhi ya wanafunzi walioonekana kuzirai na kupoteza
fahamu kwa zaidi ya saa mbili kwa kukosa chakula kabla ya kuokolewa na wakazi
wa maeneo ya jirani na Chuo walioamua kuchangia fedha na kuanza kuwapikia
wanafunzi hao.
Baadhi ya wananchi pia walionekana
chuoni hapo wakiangua vilio kwa kuwahurumia wanafunzi na wazazi wao kwa hasara
kubwa waliyoipata baada ya kutapeliwa na uongozi wa chuo hicho ulioanza kupokea
wanafunzi na kuwatoza ada ingali ukijua chuo hakijasajiriwa.
Joanes Renatus, mwanafunzi kutoka mkoa
wa Kagera amesema alipokea barua na fomu ya kutaarifiwa kujiunga na Chuo hicho
baada ya matokea ya kidato cha nne mwaka jana ikiambatanishwa na gharama za
michango yenye jumla ya shilingi 860,000.
Joanes amesema barua hiyo ilikuwa
ikisisitiza mwanafunzi anaporipoti kufika na karo ya mhula wa kwanza ambayo ni
shilingi 550,000 jambo ambalo lilitekelezwa na wazazi na kufanikiwa kufika
Chuoni Septemba mwaka huu.
Amesema kuwa jambo la kushangaza ni
kuona tangu afike chuoni hapo hali aliyoikuta imekuwa tofauti na matarajio yake
ambapo baada ya yeye na wanafunzi wenzie kutafuta usajili wa chuo kutokana na
muonekano wa majengo na upungufu wa Walimu waligundua kuwa chuo hicho hakina
usajili kutoka Nacte.
Wanafunzi wengine Annaf Habibu
(Kagera), Mtani Ndelekule(Mara) na Joviness Selestine kutoka Karagwe wamefafanua
zaidi wakisema baada ya kuripoti chuoni hapo hawakukuta wananfunzi wengine
jambo walilouliza na kujibiwa kuwa wako kwenye mafunzo ya vitendo lakini kadri
muda ulivyozidi ikabainika kuwa wao walikuwa wanafunzi wa kwanza.
Wanafunzi hao 48 ambao asilimia
kubwa wanatoka mikoa ya kanda ya Ziwa wamesema hadi sasa hawajui hatima ya maisha
yao kutokana na baadhi yao wazazi kuuza mifugo na mashamba ili kuwagharamia
nauli na ada na ndipo wakaweza kufika chuoni hapo.
Wamesema hivi sasa maisha yao yako
hatarini kutokana na kutokuwa na chakula jambo linalowalazimu majirani na
baadhi ya wazazi kuwachangia kitu chochote ili mradi wapate mlo wa siku.
Wameiomba Serikali kuingilia kati
sakata hilo na ikiwezekana iwatafutie chuo kingine ili waweze kuendelea na
masomo ili waweze kutimiza adhma yao na kuwaridhisha wazazi kwa kuwa
wakirudishwa makwao wengi wao hawatapokelewa wala kuaminiwa tena.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Ilemi(Chadema)
Furaha Mwandalima baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachuo hao na kufika
Chuoni hapo na kujionea hali halisi alionesha kushangazwa kuona kuna chuo
mahali hapo akisema hakuwahi kukisikia katika maisha yake.
Mwandalima alisema taarifa za kuwepo
kwa Chuo hicho alizipata baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Ubalozi na
wanafunzi wenyewe hivyo aliamua kuchukua hatua za haraka za kumtafuta Mstahiki
Meya ambaye alimshauri kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya ili kupata mustakabali
wa suala hilo.
Diwani huyo alisema muafaka
uliofikiwa ni kutolewa kwa agizo la kuorodheshwa kwa majina ya wanafunzi na
mahali wanakotoka ili kuwarudisha makwao na Chuo kifungwe kutokana na Chuo
hicho kutosajiliwa rasmi na kwamba kilikuwa kinaendeshwa kijanja na wanachuo
hao wamelipa malipo ya awali zaidi ya shilingi laki tano na kufikia zaidi ya
shilingi Milioni 26 zilizotapeliwa na uongozi wa Chuo.
Balozi wa mtaa wa Mapelele jijini
hapa Geophrey Mwalupindi na mkazi mwenzake Fanuel Kisanga walipoulizwa kama
wamewahi kusikia kuwepo kwa Chuo hicho walionesha kushangaa na kudai kuwa awali
kilikuwa ni kituo cha kufundishia masomo ya ziada(Tution) na masomo ya awali(chekechea)
lakini kuhusu Chuo wamesikia baada ya kutokea utapeli.
Kati ya wanafunzi waliotapeliwa,43
wanatokea Mkoa wa Kagera,wawili mkoani Mara,wawili wilayani Kyela mkoani Mbeya
na mmoja akitokea Dar es Salaam.
Juhudi za kuupata uongozi wa Chuo
hicho haukufanikiwa kupitia namba za simu za Mkononi walizoandika kwenye bango
la chuo ambazao ni 0765659079 na 0684423849 kwani hazikupatikana hewani.
Uchunguzi pia uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa malipo ya karo
chuoni hapo yalikuwa yakipokelewa kwa ujanjaujanja na mtu aliyefahamika kama Samwel
Daud ambaye ni mmiliki wa chuo hicho na njia anazotumia kukusanyia ada kutoka
kwa wanafunzi ambao hupeleka kwa katibu mukhtasi wake na kutoa stakabadhi
isiyokuwa na namba za usajili wa chuo wala namba za TRA( tin number).
Njia nyingine ambayo wanafunzi
waliambiwa walipie ada zao ni kupitia njia ya Mpesa ambapo mzazi alilazimika
kutuma kwa wakala mwenye namba 98369 tofauti na kupokelewa kwa njia ya Benki au
simu ya uongozi.
Kama vile haitoshi,mmiliki wa Chuo
hicho alitumia mbinu zaidi ili kuwaaminisha wanafunzi na wazazi kuwa Chuo hicho
kimesajiliwa baada ya kuchora kibao kikionesha Chuo hicho kilifunguliwa rasmi
na waziri kuu wa Mstaafu, Frederick Sumaye.
No comments:
Post a Comment